WABUNGE
wawili wa Tarime Vijijini, John Heche na wa Tarime Mjini, Esther Matiko wote
kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wamejikuta mikononi mwa
Polisi kwa tuhuma mbili tofauti.
Tuhuma
hizo ni kudaiwa kuchochea wananchi kulima zao haramu la bangi vile vile
kuwachochea wananchi kuvamia mgodi wa Acacia North Mara.
Kamanda
wa Polisi Kanda Maalumu ya Tarime/Rorya, Henry Mwaibambe amethibitisha kuwa
Polisi imewakamata wabunge hao kwa uchochezi na kwamba wanawahoji.
Kamanda
Mwaibambe alisema Heche na Matiko wote wana makosa mawili kila mmoja;
kuwachochea wananchi kulima zao haramu la bangi na tuhuma ya pili ni
kuwachochea wananchi kuvamia mgodi wa Acacia North Mara.
Alisema
Heche anadaiwa kuchochea wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Sirari,
kulima bangi na kosa lingine kuwachochea wananchi kuvamia mgodi wa Acacia North
Mara uliopo Nyamongo na kusababisha hasara ikiwemo kuharibu mali na kujeruhi
walinzi wakiwemo askari Polisi
“Matiko
anatuhumiwa kwenda Jimbo la Tarime Vijijini katika mkutano wa Heche huko Sirari
na kuwachochea wananchi kulima bangi badala ya kulima miwa. Watuhumiwa
wanahojiwa na hatua zaidi zitachukuliwa dhidi yao,” alisema Kamanda Mwaibambe.
Wabunge
hao walipohojiwa wakiwa katika Kituo cha Polisi Tarime, walikiri kushikiliwa na
kuhojiwa kwa tuhuma hizo, lakini walikana kufanya uchochezi.
“Mimi
juzi (Jumamosi) niliambiwa kuwa ninahitajika hapa Polisi nami nilifika na kisha
kuambiwa ninatuhumiwa kuchochea wananchi kulima bangi na kuchochea wananchi
nikiwa bungeni kuwa wavamie mgodi wa Acacia North Mara.
“Mimi
napinga tuhuma hizo ninazoshitakiwa nazo kwani maswala ya bungeni huishia
bungeni sasa hapa uraiani yanafikaje? Nimekwama hapa mahabusu tangu asubuhi
hadi sasa sijapatiwa dhamana mbali na ndugu zangu hao mnaowaona hapo nje
waliofika kunidhamini, dhamana ni haki ya mshitakiwa kwa tuhuma kama hizo
ambazo hazina ukweli,” alisema Heche akiwa chini ya ulinzi wa Polisi.
Kwa
upande wake, Matiko alihojiwa na kisha kupewa dhamana na kutakiwa kufika leo
kituoni hapo. Aidha, jana katika kituo hicho, Matiko baada ya kuachiwa pamoja
na baadhi ya viongozi na wanachama wa Chadema, walikuwa wakishughulikia dhamana
ya Heche.
No comments:
Post a Comment