Kwa mujibu wa Sheria ya Sikukuu
za Kitaifa (The Public Holidays Act, Cap 35) pamoja na Sheria zingine zinazompa
mamlaka Rais kutangaza siku yoyote kuwa sikukuu au mapumziko, Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John
Pombe Joseph Magufuli ameamua kuwa maadhimisho ya Sherehe za Uhuru na
Jamhuri zitakazofanyika tarehe 9 Desemba, 2015 yatumike kufanya kazi.
Kwamba maadhimisho ya Uhuru ya
mwaka huu (2015) yatatumika kama kichocheo cha kujenga tabia ya kufanya kazi
(Uhuru na Kazi) katika Taifa letu. Mheshimiwa Rais ameelekeza Watanzania wote
siku hiyo waitumie kwa kufanya kazi mbalimbali kama vile, mashambani, maofisini,
sokoni, viwandani na usafi wa miji yao katika kutimiza dhana ya Uhuru na Kazi
kwa vitendo.
Aidha, kwa kuwa Sherehe za
Uhuru na Jamhuri huendana na Maandalizi mbalimbali ambayo yanatumia fedha, kwa
kuzingatia kuwa siku hiyo itaadhimishwa kwa kufanya kazi , fedha zilizokuwa
zimetengwa kwa ajili ya sherehe hiyo sasa zitumike kwa shughuli zingine za
kijamii ikiwa ni pamoja na kupambana na maradhi hasa kipindupindu, kununulia
dawa za hospitali, vitanda vya hospitali n.k. kadri kamati za maandalizi zitakavyoamua.
Ieleweke kuwa sherehe za Uhuru
na Jamhuri ni muhimu katika kuadhimisha kumbukumbu ya uhuru wan chi yetu.
Hivyo, sherehe hizi zitaendelea kuadhimishwa kila mwaka kama kawaida kuanzia
mwaka 2016.
Gerson
Msigwa
Kaimu
Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
No comments:
Post a Comment