Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Said Meck Sadiki akizungumza katika uzinduzi wa semina
ya mafunzo ya madereva wa mabasi yaendayo haraka (BRT) leo jijini Dar
es salaam, juu ya kuanza kwa kipindi cha mpito cha mradi huo Oktoba
mwaka huu, Semina itakayofanyika Agosti 23 mwaka huu jijini Dar es
salaam.
Waziri
Mkuu, tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na mgeni rasmi Hawa Ghasia
akizungumza katika uzinduzi wa mafunzo ya madereva wa mradi wa mabasi yaendayo haraka (BRT) waliokaa mbele, kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Said Meck Sadiki na kulia ni Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Dk. Didas Masaburi.
Waziri
Mkuu, tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na mgeni rasmi Hawa Ghasia
aliyeshika mkasi akikata utepe kuzindua mafunzo madereva wa mabasi
yaendayo haraka (BRT) jijini Dar es Salaam katika uzinduzi wa mafunzo
yayo ya madereva.
Baadhi ya viongozi wa jeshi la polisi hapa nchini wakiwa na abiria katika basi la mwendo wa haraka jijini Dar es Salaam leo.
Mgeni rasmi na Waziri
Mkuu, tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na mgeni rasmi Hawa Ghasia
akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi katika mradi wa
mafunzo ya madereva wa mabasi ya mwendo wa haraka (BRT) jijini Dar es
Salaam leo.
Moja ya mabasi yaendayo mwendo wa haraka yakiwa barabarani katikati ya jijini Dar es Salaam leo.
Picha na Emmanuel Massaka,Globu ya Jamii.
Na Mwandishi wetu.
SERIKALI imewataka madereva walioanza kupata mafunzo
ya kuendesha mabasi yatakayotumika katika mradi wa mabasi yaendayo haraka (BRT)
kuzingatia mafunzo hayo ya kihistoria hapa nchini.
Mafunzo hayo yaliyoanza jana ni moja ya matayarisho ya
kuanza kwa mradi huo katika kipindi cha mpito mwezi Oktoba mwaka huu.
Akifungua rasmi mafunzo hayo jana jijini Dar es
Salaam, Waziri Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(TAMISEMI), Bi. Hawa Ghasia aliwataka madereva hao kuyapokea kwa bidii na
umakini mkubwa.
“Mafunzo haya yatawapa fursa ya kuweza kufanya kazi
kwenye miradi mingine ya BRT kwani vigezo na mtaala wake ni wa kimataifa,”
alisema wakati wa maadhimisho hayo katika eneo la Ubungo.
Waziri Ghasia aliieleza kwamba mafunzo hayo ni ya
kihistoria hapa nchini kwani kwa mara ya kwanza watapatikana madereva wenye
leseni za kimataifa na kuwa mafunzo hayo yatahusu pia namna ya kuhudumia
wateja.
“Madereva hawa watajengewa weledi na nidhamu katika
kazi yao ambayo kwa sasa inalalamikiwa sana na wananchi wakilalamikiwa kwa
utovu wa nidhamu na kutotii sheria za barabarani,” alisema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw.
Said Meck Sadiki alisema kuzinduliwa kwa mafunzo hayo ni ushahidi wa dhamira ya
serikali kutatua kero ya usafiri na msongamano wa magari jijini humo kupitia
mradi wa BRT.
“Mradi huu wa aina yake nchini na barani Afrika utatoa
fursa mbalimbali za uwekezaji na biashara kwa sekta binafsi ambayo ndio msingi
wa maendeleo ya nchi,” alisema.
Mafunzo hayo kwa madereva wazalendo yanafanyika baada
ya kushinda usaili ulio endeshwa na wataalamu kutoka chuo cha ufundi stadi na
mafunzo (VETA).
Jumapili iliyopita kampuni ya watoa huduma wa ndani wa
mradi huo, UDA-RT iliendesha semina ya mafunzo kwa wahariri wa vyombo vya
habari kuhusiana na huduma za kipindi cha mpito za mradi huo.
Mradi huo wa awamu ya kwanza unahusisha ujenzi wa
kilometa 20.9 za barabara maalum kutoka Kimara hadi Kivukoni; barabara ya
Msimbazi kutoka Faya hadi Kariakoo-Gerezani na sehemu ya barabara ya Kawawa
kuanzia Magomeni hadi eneo la makutano ya Morocco.
No comments:
Post a Comment