Kaimu
Mkurgenzi, Idara ya Maendeleo ya Sanaa, Wizara ya Habari, Utamaduni,
Sanaa na Michezo, Bi. Leah Kihimbi (kulia) akiongea na baadhi ya
Viongozi wa Mashirikisho ya Filamu Tanzania (hawapo pichani) kuhusu
maendeleo ya sekta ya sanaa nchini wakati alipokutana nao hivi karibuni
Wizarani hapo jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Katibu wa Bodi ya Filamu
Tanzania, Bi. Joyce Fissoo.
Kaimu
Mkurgenzi, Idara ya Maendeleo ya Sanaa, Wizara ya Habari, Utamaduni,
Sanaa na Michezo, Bi. Leah Kihimbi (aliyekaa mbele) akiongea na baadhi
ya Viongozi wa Mashirikisho ya Filamu Tanzania (hawapo pichani) kuhusu
maendeleo ya sekta ya sanaa nchini wakati alipokutana nao hivi karibuni
Wizarani hapo jijini Dar es Salaam. Kulia kwake ni Katibu wa Bodi ya
Filamu Tanzania, Bi. Joyce Fissoo.
………………………………………………………………………………………….
Na Benedict Liwenga-WHUSM.
Serikali
imekutana na kufanya mazungumzo na baadhi ya Viongozi wa Mashirikisho
ya Filamu nchini ikiwa ni sehemu ya kubaini changamoto mbalimbali
zinazoyakabili Mashirikisho hayo.
Akiongea jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi Idara ya Maendeleo
ya Sanaa, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bi. Leah
Kihimbi alisema kwamba, Mashirikisho yanayounda Shirikisho la Filamu
nchini hayanabudi kushirikiana kwa karibu na Serikali ili kubaini
changamoto na namna ya kuzitatua kwa manufaa ya Wasanii na Taifa kwa
ujumla.
Alieeleza
kuwa, Wasanii wanapaswa kuzingatia maadili wakati wanapofanya kazi zao
za sanaa ili waweze kujijengea heshima kwao, kwa jamii ambayo ndio mlaji
wa kazi zao za kisanaa na kwa Taifa kwa ujumla.
“Mnapofanya
kazi zenu za sanaa, jitahidini kufuata miiko ya kazi zenu, tumieni
vipaji vyenu vizuri kwa kufuata maadili ya Kitanzania, lakini pia
jitahidini kuwainua wale wasanii wanaochipukia ama wale wadogo ili
waweze kuwa na hamasa ya kuendeleza kazi zao za sanaa”, alisema, Bi.
Kihimbi.
Bi.
Kihimbi aligusia suala la fursa ya kazi za sanaa inayodhaminiwa na
Taasisi ya British Council Tanzania na kuwataka wasanii kuchangamkia
fursa hiyo kwa kuhakikisha kuwa kila msanii au kikundi kinaandika
Pendekezo (Proposal) kuhusu
fursa hiyo ili kujiwekea nafasi kubwa kwa wasanii wa Tanzania kushinda
fursa hiyo na kuweza kupata fedha za kuendesha kazi za sanaa kulingana
na wazo lililobuniwa.
“Kuweni wabunifu katika hii fursa ili mje na wazo zuri ambalo litawawezesha kushinda hii fursa hasa hii ya nAnA (new Arts new Audiences) kwani inamhusu msanii mmoja mmoja au kikundi”, alisema, Bi. Kihimbi.
Aliongeza
kuwa, Serikali itajitahidi kutatua baadhi ya changamoto ambazo
zinaonekana kuwa kero kwa wasanii nchini ikiwemo suala la wizi wa kazi
za sanaa (Piracy) ambalo
kwa sasa tayari Waziri mwenye dhamana katika Wizara hiyo, Mhe. Nape
Nnauye ameonyesha mfano kwa kukamata DVDs feki pamoja na mitambo
ikiyotumika kudurufu kazi hizo za sanaa nchini.
Kwa
upande wake, Katibu wa Bodi ya Filamu Tanzania, Bi. Joyce Fissoo
alisema kwamba Bodi yake inashirikiana vema na wasanii nchini kwa
kuzingatia Sheria za nchi pasipo kumuonea msanii yeyote na kuwataka
wasanii kote kuendeleza uhusiano huo mzuri uliopo kwa manufaa yao na
Taifa kwa ujumla.
Aidha,
aliwataka viongozi wa Shirikisho hilo la Sanaa kuendelea na utaratibu
wa kupeana taarifa kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu sanaa na
kuwahimiza wasanii kupenda kujiendeleza kielimu ili waweze kumudu soko
huku akiwasisitiza kuhakikisha kuwa kazi zao wanazotengeneza zinapata
kibali cha Bodi kwa kuwekewa madaraja na zinakuwa na stika halali ya
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili kuepusha uharamia wa kazi zao.
Naye
Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania, Bw. Simon Mwakifwamba ameiomba
Serikali kuendelea kushirikiana na Wasanii kwa karibu kwa kuzifanyia
kazi baadhi ya changamoto wanazokabiliana nazo na ikiwemo suala la
uharakishaji wa Sera ya Filamu kwani ndiyo kipaumbele chao cha kwanza,
elimu ya namna ya kutengeneza filamu bora, usambazaji wa kazi zao pamoja
na adui yao mkubwa ambaye ni uharamia wa kazi za sanaa.
Ameishukuru
Serikali kwa kuunda Sekta mpya ya Sanaa na kusema kuwa, Sekta hiyo
itakuwa Mkombozi kwao kwani wanajisikia fahari kutambuliwa na kuwa na
kitengo chao cha masuala ya kazi zao huku akiaahidi ushirikiano mzuri
kwa sekta hiyo.
No comments:
Post a Comment