KATIKA kipindi cha sherehe za Krismasi na
Mwaka Mpya watalii wa nje na wa ndani wanaongezeka katika visiwa vya Zanzibar
kutembelea vivutio vya utalii na hasa Jumba la Maajabu ambalo limesheheni
historia kuhusu Zanzibar na ubunifu mkubwa juu ya usanifu wa majengo kwa kutumia
teknolojia ya kipekee.
Jumba hilo maarufu kama Beit-al- Ajaib kwa
lugha ya Kiarabu ni miongoni mwa vitu vya kipekee vinavyopatikana katika visiwa
vya Zanzibar na limehifadhi kumbukumbu na historia ndefu kuhusu ubunifu na maendeleo
ya Zanzibar.
Jumba hilo lipo barabara ya Mizingani katika
ufukwe wa bahari na linaonekana kwa urahisi unapoingia Zanzibar kwa njia ya
bahari.
Jumba hilo lenye zaidi ya miaka 125 ni
sehemu ya kivutio muhimu kwa watalii ambao wanafika Zanzibar kila siku kwa
ajili ya kujifunza tamaduni, mambo ya kale na hatua za maendeleo katika jamii
ya Waafrika.
Kwa mujibu wa taarifa ya Idara ya
Utamaduni Zanzibar, jumba hilo huonekana la ajabu kutokana na ujenzi wake pia
ni la kwanza kutumia maji ya bomba. Lina nguzo zaidi ya 40 zilizojengwa kwa
ustadi mkubwa.
Wajenzi wa jumba hilo walitumia mchanganyiko
wa utaalamu kutoka mataifa mbalimbali ikiwamo Asia na Ulaya ingawa lilisimamiwa
na utawala wa Sultani kutoka jamii ya Waarabu.
Jengo la kwanza kutumia umeme
Jumba hilo limepata umaarufu mkubwa kwa
kuwa lilikuwa jengo la kwanza Afrika Mashariki kutumia umeme. Wakati huo watu
walikuwa wakitumia kandili, vibatari na mishumaa kwa ajili ya kupata mwanga nyakati
za usiku.
Pia wapo ambao walikoka moto mkubwa ili
kupata mwanga wa kukamilisha
shughuli zao kabla ya kulala.
Lakini jumba hilo lilikuwa likiwaka taa
ambazo zilibandikwa ukutani na nyingine zilining’inia kutoka uzi mrefu
uliotundikwa kwenye dari.
Kwa kuwa mwanga wa taa hizo ulionekana kwa
mbali ulisababisha watu wengi kupigwa na butwaa.
Taarifa za kuwepo kwa jumba lenye taa za
ajabu zilisambaa katika ukanda wote wa Afrika Mashariki hivyo watu kutoka
Kenya, Uganda na Tanzania hasa wavuvi walisafiri hadi Zanzibar kushuhudia
maajabu ya jumba hilo.
Kuwa na lifti.
Jumba hilo la ghorofa lilikuwa jengo la
kwanza kuwa na lifti katika ukanda wa Afrika Mashariki. Tofauti na majengo
mengine ambayo ilikuwa ni lazima kupanda ngazi ili ufike ghorofani wageni
waliofika kwenye jengo hilo hawakupanda ngazi bali walitumia lifti.
Lift ni mashine maalum inayokaa katika
chumba kidogo ambapo watu huponyeza kitufe na kisha mashine hiyo huwapandisha
hadi ghorofa ya juu na kumshusha tena ghorofa ya chini pasipo pasipo kutumia
ngazi.
Habari za kuwepo kwa lifti katika jengo
hilo zilizua gumzo na maswali mengi katika Ukanda wa Afrika Mashariki. Wavuvi
na wasafiri waliofika Zanzibar walikwenda kwenye jumba hilo kwa lengo la
kuingia ndani ili waweze kushuhudia maajabu wanayoyasikia.
Mfumo wa maji.
Mfumo wa maji taka na maji safi ya bomba
ni miongoni mwa mambo yaliyosababisha jumba hilo kuonekana la maajabu. Wakati
majengo mengine ya kifahari katika Ukanda wa Afrika Mashariki yalikuwa na vyombo
mbalimbali kuhifadhia maji, Jumba la maajabu lilikuwa la kwanza kuwa na bomba
zinazotiririsha maji ndani ya nyumba.
Jumba hilo lilipata umaarufu zaidi baada
ya kuwekwa mfumo wa maji safi na salama pia mfumo wa maji taka. Pia mfumo huo
ulisababisha baadhi ya watu kujawa wa maswali mengi juu ya uwepo wa maji safi katika
jumba lililopo kwenye kisiwa kilichozungukwa na bahari yenye maji ya chumvi.
Hata wataalamu waliofika katika jengo hilo
walishangazwa na ubora na uzuri wa jengo hilo lililojengwa kwa mtindo wa
kipekee. Kwa mujibu wa historia ya Zanzibar, ubunifu wa jumba hilo ulifanywa na
askari wa meli toka Scottland na lilijengwa na Sultan Barghash bin Said katika mwaka
wa 1883, kwa ajili ya ofisi yake.
Matumizi ya jengo.
Hata hivyo matumizi ya jumba hilo yalikuwa
yakibadilika kadiri miaka ilivyokuwa ikienda na jinsi tawala zilivyokuwa
zikibadilika visiwani humo. Kati ya mwaka 1870 na 1888 jumba hilo lilitumika
kwa ajili ya sherehe za kitaifa chini ya utawala wa kisultani.
Mwaka 1913 utawala wa kikoloni wa
Waingereza ulibadilisha matumizi ya jumba hilo na kulifanya ofisi za Serikali
za Mitaa. Inaaminika kuwa hadi sasa hakuna jengo lolote la ofisi ya Serikali za
Mitaa Tanzania bara na visiwani ambalo linakaribia kuwa na hadhi ya jumba hilo
la maajabu.
Baada ya Zanzibar kupata uhuru matumizi ya
jengo hilo yalibadilishwa na kuwa jumba la kumbukumbu za kihistoria kuhusu
harakati za ukombozi wa Zanzibar. Kati ya mwaka 1964 na 1977 Jumba hilo maarufu
lilitumika kama jumba la kuhifadhi kumbukumbu za chama cha Afro Shiraz Party
(ASP) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) .
Baada ya kuzaliwa kwa chama cha Mapinduzi
(CCM) Mwaka 1977 jumba hilo kumbukumbu nyingine muhimu pia kama ofisi ya CCM,
hali ya jumba haikuwa ya kuridhisha sana pamoja na kuwa na historia ndefu.
Kwa mfano ndio ilikuwa sehemu pekee ya
kuweza kuona magari ya Rais wa kwanza wa Zanzibar marehemu Abeid Amaan Karume.
Jumba hilo lilibadilishwa matumizi na kuwa
sehemu ya hifadhi ya Taifa kwa ajili ya kutunza kumbukumbu za kale hasa zile
zinazohusiana na jumba hilo na maajabu yake.
Uzuri wa jumba hilo umekuwa moja ya hazina
ya historia iliyouwezesha Mji Mkongwe kuwa katika orodha ya urithi wa Dunia
uliyohifadhiwa na Shirika la Kimataifa ya Maendeleo ya Sayansi, Elimu na
Utamaduni (UNESCO).
Katika jumba hilo kuna makumbusho ya
utamaduni wa Jahazi ambapo kuna picha za majahazi ya msimu yaliunganisha
Mwambao wa Mswahili na sehemu nyinginezo za Bahari ya Hindi. Lina michoro na
zana za kale zinazoelezwa shughuli mbalimbali za wenyeji na wageni ambao wameifanya
Zanzibar kuwa kisiwa cha watu wenye asili tofauti.
Katika jumba hilo kuna chombo cha usafiri
maarufu kama Mtepe ambacho kiliundwa bila kutumia misumari.
Pia ukitembelea jumba hilo utaona
kumbukumbu za utaarabu wa Waswahili ambao unawakilishwa na tamaduni mbalimbali
kama vile majengo, mavazi, uchongaji, imani, lugha, nyimbo na ngoma.
Kumbukumbu ya vita.
Jengo hilo limehifadhi kumbukumbu ya vita
vilivyodumu kwa muda mfupi katika historia ya vita duniani.
Vita hii ilitokea Agosti mwaka 1896 na
inadaiwa kuwa vilidumu kwa takribani dakika 32 tu.
Kwa mujibu wa historia, vita hiyo ilitokea
mara baada ya kifo cha ghafla cha Sultani Sayyid Hamid Thuwain bin Said ambaye
alifariki tarehe Agosti 25, 1896. Baada ya kifo hicho kijana machachari Khalid
bin Barghash alijitangaza kuwa mrithi wa Sultani Sultani Sayyid Hamid jambo
ambapo lilipingwa na Waingereza.
Ingawa Barghash alikuwa kipenzi cha
wenyeji wa Zanzibar hakuwa chaguo la Waingereza ambao ndio waliokuwa na jukumu
la kulinda usalama wa Zanzibar kutokana na urafiki wa muda mrefu kati ya utawala
wa Uingereza na utawala wa Kisultan ambao ulianzia Oman.
Waingereza walichukizwa na kitendo cha
Barghash kujitwalia madaraka kwa kuwa walitaka Hamoud bin Mohamed awe mrithi
kwa kuzingatia utaratibu uliokuwepo kwamba mkubwa ndio mwenye dhamana ya
kurithi kiti cha mfalme endapo mfalme atafariki dunia.
Waingereza walimpendelea Hamoud bin
Mohamed ambaye alikuwa mpwa wa aliyekuwa Sultan wa Oman na mtu aliyependelea
zaidi maisha ya kisasa. Waingereza walimuamini angeweza kuwa rahisi zaidi kufanya
naye kazi kuliko Khalid ambaye alikuwa mwerevu na mwenye uwezo wa kujitegemea.
Waingereza walibaini kuwa maslahi yao yatapotea na hivyo walitoa onyo na
kumtaka aachie madaraka vinginevyo wangetumia nguvu za kijeshi kumtoa.
Hata hivyo Barghash hakutishika na
aliendelea kushika ngome zote muhimu kwa ajili ya kuimarisha himaya na utawalawake.
Kuona hivyo Waingereza walijiandaa kwa ajili ya vita.
Serikali ya Uingereza ilimuagiza Mkuu wa
Jeshi katika Bahari ya Hindi kuleta kwa haraka meli za kivita Zanzibar ili
zikaungane na meli mbili za kivita za Kifalme ambazo zilikuwa zimetia nanga
katika bandari wakati Sultan alipofariki.
Amri hiyo iliendelea hadi jioni ya Agosti
tarehe 25, wanaume wa Kizanzibari katika uwa wa Kasri walikuwa na saa 40
kutafakari hatima yao. Ilikuwa kupigana au kukimbia.
Wangekaa? Wangeweza kweli kuendelea kusubiri
tu na kukodoa macho kwa Simba wa Ubereru ambaye alikuwa anakaribia kuachiliwa
dhidi yao?
Mnamo Agosti 26 1896 majeshi yalijiandaa
kwa ajili ya vita ambayo ilifanyika kesho yake na kati ya dakika 37 hadi 45
ambapo Barghash alifanikiwa kuwaponyoka Waingereza na kukimbilia
kusikojulikana.
Vita hiyo iliharibu baadhi ya jengo la
maajabu hasa mnara wa saa hivyo kulifanya umbo la jengo hilo kubadilika kidogo
hasa sehemu ya mbele.
Baadhi ya majengo ya Kisultani
yaliharibika ikiwa ni pamoja na mnara wa saa uliokuwa katika jumba la maajabu.
Baada ya vita hiyo mnara huo ulifanyiwa
matengenezo na hadi leo unatumika kama alama ya kumbukumbu ya vita hiyo
inayoshikilia historia ya dunia ya vita iliyochukua muda mfupi kuliko vita
zote.
No comments:
Post a Comment