Amiri
Jeshi Mkuu Rais Dkt John Pombe Magufuli akiongea na wananchi baada ya
kuweka silaha za jadi katika Mnara wa kumbukumbu ya Mashujaa
alipoongoza Madhimisho ya Siku ya Mashujaa mjini Dodoma leo Julai 25,
2016
………………………………………………………………………………………….
Na: Immaculate Makilika- Dodoma
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli amewaasa
watanzania kudumisha amani iliyopo ambayo ilipatikana baada ya Mashujaa
mbalimbali kuipigania na hata kujitoa uhai wao kwa ajili ya Taifa.
Akizungumza leo,
wakati akihutubia wananchi mara baada ya kumaliza shughuli za
maadhimisho ya Siku ya kumbukumbu ya Mashujaa iliyofanyika katika
viwanja vya Mashujaa vilivyopo mjini Dodoma.
Rais Magufuli
alisema kuwa maadhimisho ya kumbukumbu za Mashujaa ni muhimu kwa vile
watu hao walijotoa kwa ajili ya kulitetea taifa.
“Wakati
tunawakumbuka waliotangulia mbele za haki, sisi tuliobaki tudumishe
amani hii, kama ambavyo wao waliotutangulia hawakujali dini zao bali
taifa hili” alisema Rais Magufuli.
Aliongeza kuwa nchi
ya Tanzania imebaki kuwa kisiwa cha amani, na amani hiyo isichezwe
bali ijengwe na kudumishwa kwa umoja na mshikimamano ili kusaidia
kuitangaza nchi zaidi.
Aidha, viongozi
mbalimbali wa Serikali akiwemo Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar,
Mheshimiwa Dkt.Ali Mohamedi Shein, Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili
Mheshimiwa Alhaji Ali Hassan Mwinyi, Waziri Mkuu Mstaafu Mheshimiwa
John Samweli Malecela nao wapewa fursa ya kuzungumza na wananchi kuhusu
maadhimisho hayo ya kumbukumbu ya siku ya Mashujaa.
Viongozi hao,
wamesisitiza umuhimu wa kudumisha amani iliyopo na kusema kuwa ni jukumu
la wananchi wote kuhakikisha hawashiriki katika vitendo
vitakavyosababisha uvunjifu wa amani.
Ambapo, waliwataka
wananchi kuwaombea Mashujaa wote waliofariki katika vita mbalimbali
wakiwa katika harakati za kulifanya Taifa la Tanzania kuwa huru.
Wakati huo huo,
Waziri Mkuu Mheshimiwa Kassim Majaliwa, alisema kuwa atahakikisha
anasimamia utekelezaji wa agizo la Rais la kuitaka Serikali kuhamia
mjini Dodoma.
“Nahamia Dodoma
mwezi wa tisa,na nitakapohamia mawaziri wote lazima wanifuate. Katika
hili nitasimamia kwa nguvu zote” alisema Waziri Mkuu Majaliwa.
Awali, Mheshimiwa
Rais Magufuli alisema kuwa atahakikisha katika kipindi cha utawala wake,
Serikali inahamia mjini Dodoma, kwa vile Rais wa Awamu ya kwanza Mwl.
Julius Nyerere alionesha nia ya kufanya hivyo.
Aliongeza kuwa
kwa sasa mji wa Dodoma unaweza kukidhi mahitaji hayo ya Serikali kwa
kutumia miundombinu iliyopo, hata hivyo Serikali inaendelea kujenga
miundombinu mipya.
Maadhimisho ya
kumbukumbu za Mashujaa hufanyika Julai 25, ya kila mwaka, kwa kufanya
maombolezo ya Mashujaa waliopigana katika vita mbalimbali katika
harakati za kutetea uhuru wa nchi ya Tanzania.
Maadhimisho ya
mwaka huu yamefanyika kwa mara ya kwanza mjini Dodoma, ambapo Rais John
Pombe Magufuli alikuwa mgeni rasmi, ikiwa ni mara yake ya kwanza
kuhudhuria maadhimisho hayo kama Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania.
No comments:
Post a Comment