Mwenyekiti wa CCM Jakaya Kikwete akihutubia katika Mkutano Mkuu wa CCM leo katika Ukumbi wa Dodoma Convetion Centre. Ukiwa ni maalum kupitisha jina la Rais Dk. Magufuli kuwa Mwenyekiti mpya wa CCM |
DODOMA, 23 JULAI 2016
Mheshimiwa Dr. John Pombe
Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Dr. Ali
Mohammed Shein, Makamu Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Zanzibar;
Mheshimiwa Philip Mangula,
Makamu Mwenyekiti wa CCM – Bara;
Mheshimiwa Samia Suluhu
Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Kassim
Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Balozi Seif Ali
Idd, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Mheshimiwa Ali Hassan
Mwinyi, Rais na Mwenyekiti Mstaafu wa CCM;
Mheshimiwa Benjamin
William Mkapa, Rais na Mwenyekiti Mstaafu wa CCM;
Mheshimiwa Abdulrahman
Kinana, Katibu Mkuu wa CCM;
Waheshimiwa Makamu Mwenyeviti
Wastaafu wa CCM;
Waheshimiwa Makatibu Wakuu
Wastaafu wa CCM;
Waheshimiwa Mawaziri Wakuu
Wastaafu;
Waheshimiwa Wajumbe wa
Kamati Kuu;
Waheshimiwa Wajumbe wa
Halmashauri Kuu ya Taifa;
Waheshimiwa Wajumbe wa
Mkutano Mkuu wa Taifa;
Wageni wetu waalikwa; Mabibi na Mabwana,
Kama ilivyoada naomba tuanze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi
wa rehema kwa kutujaalia uzima na kutusafirisha salama kutoka makwetu hadi hapa
Dodoma.
Nawapa pole ya safari na karibuni Dodoma na kwenye Mkutano Mkuu Maalum
wa Taifa wa Chama cha Mapinduzi. Kwa niaba yenu napenda kutumia nafasi hii
kutoa pongezi nyingi kwa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa, chini ya
uongozi makini wa Katibu Mkuu wa CCM Ndugu Abdulrahman Kinana kwa maandalizi
mazuri ya mkutano huu. Pongezi maalum tunazitoa kwa Kamati mbalimbali zilizoongozwa na kuratibiwa na Naibu Katibu Mkuu Bara Ndugu Rajab Luhwavi kwa kazi kubwa na nzuri waliyofanya mpaka mambo yamekuwa mazuri kiasi hiki kama sote tunavyoshuhudia. Ni matumaini yangu kuwa tutamaliza salama.
Karibuni Wageni waalikwa
Ndugu Wajumbe,
Katika mkutano huu tumealika wageni mbalimbali. Wapo wazee wa
Chama na marafiki wa CCM. Pia wapo watu mashuhuri, Mabalozi wa nchi za nje na
wawakilishi wa mashirika ya kimataifa waliopo hapa nchini.
Hali kadhalika kuna
wawakilishi wa vyama vya siasa. Wote hawa tunawashukuru sana kwa kukubali
mwaliko wetu na kuja kujumuika nasi kwenye siku hii muhimu katika historia ya
Chama cha Mapinduzi. Kuja kwao ni jambo la heshima na faraja kubwa kwa viongozi
na wanachama wa CCM. Ahsanteni sana, tunaomba muendelee na moyo huo wa
ushirikiano.
Ndugu Wajumbe,
Kama tujuavyo tumekutana hapa siku ya leo kwa ajili ya kubadilisha
uongozi wa juu wa Chama cha Mapinduzi. Hii itakuwa ni mara ya nne katika miaka
39 ya historia ya uhai wa chama chetu.
Mara ya Kwanza ilikuwa Agosti, 1990 wakati
Mwenyekiti wa Kwanza na muasisi wa CCM, Mwalimu Julius Nyerere alipong’atuka na
Mheshimiwa Ali Hassan Mwinyi aliyekuwa Rais wa pili wa Jamhuri ya Muungano
alipochaguliwa kuwa Mwenyekiti wa pili.
Mara ya pili ilikuwa Juni, 1996 wakati
Mheshimiwa Benjamin William Mkapa alipochaguliwa kuwa Mwenyekiti wa tatu wa CCM
kuchukua nafasi ya Mwenyekiti wa pili Mheshimiwa Ali Hassan Mwinyi alipostaafu.
Mara ya tatu ilikuwa tarehe 25 Juni 2006 wakati Mwenyekiti wa tatu Mheshimiwa
Benjamin Wiliam Mkapa alipong’atuka na mimi kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa nne.
Leo imefikia zamu yangu kustaafu na kukabidhi hatamu za uongozi wa juu kabisa
wa Chama chetu kwa Rais wa Tano Mheshimiwa John Pombe Joseph Magufuli kuwa
Mwenyekiti wa tano wa Chama cha Mapinduzi. Raha ilioje ndugu zangu. Nani kama
CCM.
Ndugu Wajumbe,
Niruhusuni kwa niaba yenu na kwa niaba yangu binafsi nitoe pongezi
nyingi kwa Mheshimiwa John Pombe Joseph Magufuli kwa kukubali kubeba dhamana ya
kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi.
Najua haikuwa Rais kwake kukubali na
ilibidi tufanye kazi ya ziada kumshawishi mpaka akakubali. Nakumbuka mara ya
kwanza mwezi February 2016 nilipomuambia kuhusu jambo hili alikataa hata
kulizungumzia.
Akaniambia kuwa yeye hana haraka kwani ana mambo ya kufanya
Serikalini na ndiyo kwanza anaendelea kupanga mambo yake. Jitihada na ufundi
wangu wote haukufanikiwa kumshawishi akubali. Nadhani kwa nia ya kutaka
niachane na mazungumzo yale alinikaribisha chakula. Nikamkubalia tukala
tukaagana.
Baadae nikamsimulia Makamu Mwenyekiti wa CCM Mzee Philip Mangula,
matokeo ya mazungumzo yangu na Rais na kumuomba nae akajaribu. Waswahili
wamesema mzee dawa.
Mwezi mmoja na nusu baadae Mzee Mangula akarudisha jibu
kuwa Rais amesema sawa, tuamue na kupanga siku. Ndipo nikarudi tena kwake na
mapendekezo ya tarehe mbili tatu aangalie kwenye ratiba yake ipi ingemfaa.
Baada ya muda si mrefu tukapata jibu la tarehe ya 23/7/2016 kuwa ingefaa. Ndiyo
maana ya kupanga na kukutana siku ya leo.
Ndugu Wajumbe,
Majibu yale ya Rais wetu hayakunishangaza kwani hata mimi na Mheshimiwa
Benjamin Mkapa ilikuwa hivyo hivyo. Aliponipa wazo la kuniachia Uenyekiti kwa mara
ya kwanza February 2006 nilimkatalia na hoja zangu ni kama hizo hizo
alizoniambia Mwenyekiti wetu mtarajiwa.
Baada ya mazungumzo zaidi nilikubali na
ndipo Mkutano Mkuu Maalum ukafanyika June 25, 2006 na nikachaguliwa kuwa
Mwneyekiti wa Nne wa CCM. Tofauti ya wakati ule na sasa ni kwamba hapakuwepo na
vyombo vya habari na watu waongo, wazushi, wachonganishi na wafitini waliodai kuwa
Mzee Mkapa anang’ang’ania kama ilivyokuwa kwangu kudaiwa ati sitaki kukabidhi Uenyekiti.
Tena wakaongeza ati wapo watu wanaozunguka kushawishi zoezi zima lisifanyike. Sijui
baada ya leo watasema nini au watazua uongo upi mpya! Najua hawataacha maana
inaelekea kuna mitambo mahsusi ya kutunga uongo na kila siku wanazalisha bidhaa
mpya.
Lengo lao ni kuchochea mfarakano ndani ya CCM na wanasikitika kwamba
jitihada zao hazifanikiwi. Ndugu zangu tuendelee kuwa makini.
Ndugu Wajumbe,
Kama kweli ningekuwa sitaki kuachia ngazi baada ya Rais kuniambia
hana haraka nisingekwenda kumtafuta Mzee Mangula akazungumze nae tena.
Nilifanya vile kwa dhamira ya kudumisha mila na desturi nzuri ya kuunganisha
kofia ya Urais wa Jamhuri ya Muungano na Uenyekiti wa Chama cha Mapinduzi.
Pili
ni kutokana na kutambua kuwa kofia hizi mbili kuvaliwa na mtu mmoja ni jambo
lenye maslahi mapana kwa Chama chetu, Serikali yetu na nchi yetu. Ni jambo
muhimu sana kwa utulivu na ustawi wa Chama Cha Mapinduzi, Serikali na Tanzania.
Wazee waliona mbali walipoamua iwe hivyo. Nisingependa “mguu wangu uote tende
kwa kutosikia la mkuu”. Bahati nzuri kwangu wakati inaamuliwa kutenganisha
kofia kwa Wakuu na Makatibu wa Mikoa na Wilaya na kubakisha kwa Rais na
Mwenyekiti ngazi ya Taifa nilikuwepo na nilishiriki kufanya uamuzi. Naelewa
vyema sababu, hekima, busara na mantiki ya uamuzi ule. Sijaiona sababu ya
kwenda kinyume na uamuzi huo.
Shukrani Binafsi
Ndugu Wajumbe,
Kwangu mimi, leo ni siku nyingine muhimu na ya aina yake katika
historia ya maisha yangu. Ni siku ambayo safari yangu ya utumishi na uongozi
katika Chama inafikia ukomo.
Safari yangu hiyo niliianza tarehe 2 April 1975,
nilipowasili Singida kuanza kazi ya Katibu Msaidizi wa TANU Mkoa wa Singida. Mwaka
mmoja baadae nikapelekwa Jeshini na baada ya kuunganisha ASP na TANU na
kuzaliwa Chama Cha Mapinduzi nilihamishiwa Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui,
Zanzibar.
Pamoja na kuwa na jukumu la kumsaidia Naibu Katibu Mtendaji Mkuu wa
CCM Col Ayoub Simba na baadae Capt. Allan Heri nilipewa dhamana kubwa ya kutengeneza
mfumo mpya wa utawala na uendeshaji wa shughuli za Chama Zanzibar.
Hususani
tulifanya kazi ya kuhaulisha mfumo uliokuwa unatumika na ASP na kuwa ule wa CCM kuanzia Afisi Kuu
Kisiwandui mpaka Ofisi za Mikoa, Wilaya na Matawi. Pia nilihusika na kuandaa
mchakato wa uteuzi wa Makatibu Watendaji wa Wilaya na Mikoa, Makatibu Wasaidizi
na watumishi wengine wa Chama.
Mwaka 1980 nilihamishiwa Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Dar es
salaam ambapo nilikuwa Mkuu wa Utawala, Mkuu wa Idara ya Ulinzi na Usalama na
Msaidizi Mahususi wa Katibu Mtendaji Mkuu wa CCM wakati ule Mzee Pius Msekwa na
baadae Mzee Daudi Mwakawago.
Mwaka 1981 nikateuliwa kuwa Katibu Mtendaji wa CCM
Mkoa wa Tabora. Mwaka 1983 nikarejeshwa jeshini na miaka mitatu baadae (1986)
nikateuliwa kuwa Katibu wa CCM Wilaya ya Nachingwea na baadae mwanzoni mwa
mwaka 1988 nikahamishiwa Wilaya ya Masasi. Mwezi Novemba 1988 nilimalizia
utumishi wangu baada ya kuteuliwa kuwa Mbunge na Naibu Waziri wa Nishati na
Madini.
Kwa upande wa uongozi ndani ya Chama nilianza mwaka 1982
nilipochaguliwa kwa mara ya kwanza kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa
kupitia kundi la Vijana. Niliendelea kuchaguliwa kwa nafasi hiyo kwa chaguzi za
miaka ya 1987, 1992, 1997 na 2002 kupitia Kundi la 20 Bara.
Mwaka 1997 na 2002
nilibahatika kuchaguliwa kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa,
na mwaka 2006 nikapata heshima kubwa ya kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Chama
cha Mapinduzi na kuchaguliwa tena mwaka 2007 na 2012 hadi hii leo.
Ndugu Wajumbe,
Leo ninapostaafu Uenyekiti wa CCM nitakuwa nimetumikia Chama kwa
takribani miaka 41 mfululizo kwa maana ya utumishi na uongozi. Na nikijumuisha
muda niliotumia katika uongozi wa Umoja wa Vijana, nimekitumikia Chama hiki kwa
miaka mingi zaidi ya hiyo.
Hata nilipokuwa Jeshini nilikuwa najishughulisha na
mambo ya siasa na Chama. Kwa kweli baada ya kipindi kirefu kiasi hicho kwanza
kwangu mimi sasa kustaafu ni jambo ninalolistahili kabisa.
Nitaendelea kuwa
mwanachama wa kawaida na kutoa mchango wangu kwa uongozi wa Chama pale
nitakapohitajika na kupitia Baraza la Wazee Wastaafu.
Ndugu Wajumbe,
Mtakubaliana nami kuwa ninayo kila sababu ya kutoa neno la
shukrani. Orodha yangu ni ndefu kidogo hivyo naomba mnivumilie maana sijui kama
nitapata fursa nyingine nzuri kuliko hii.
Kwanza kabisa namshukuru Mwenyezi Mungu,
Muumba wetu na mwenye kutoa neema ndogo ndogo na neema kubwa kubwa. Namshukuru
kwa kunijalia uzima na baraka zake zilizoniwezesha kufika hapa nilipofika
maishani. Bila ya yeye nisingefika hapa.
Namuomba aendelee kunilinda na kuniongoza
nipate hatma njema. Pili nawashukuru wazazi wangu Mzee Halfan Mrisho Kikwete na
Bi Asha Bint Jakaya Kalungwana kwa kunizaa, kunilea, kunisomesha na kwa ushauri
na maelekezo yao yaliyonisaidia kupata mafanikio niliyoyapata maishani.
Namshukuru Mzee John Aaron Mhaville aliyekuwa Katibu Mtendaji Mkuu
wa TANU kwa kuniona ninafaa kuajiriwa kuwa mtumishi wa Chama. Yeye ndiye
aliyekuwa Mwenyekiti wa Jopo lililonifanyia usaili nilipoonesha nia ya kupenda
kutumikia Chama wakati nilipokuwa Chuo Kikuu cha Dar es salaam.
Namshukuru Mzee
Pius Msekwa aliyekuwa Katibu Mtendaji Mkuu wa kwanza wa CCM kwa mambo mengi.
Namshukuru kwa kuniamini na kuniteua kwenda kufanya kazi Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui
na kunipa dhamana kubwa nikiwa na umri mdogo wa miaka 26.
Wakati ule nilikuwa
nimekitumikia Chama kwa mwaka mmoja tu. Lakini yeye na waliokuwa Manaibu wa
Katibu Mtendaji Mkuu wakati ule yaani Dr Salimin Amour Juma kwa Tanzania Bara
na Col. Ayoub Simba kwa Zanzibar waliona wanijaribu.
Bahati nzuri kwa malezi na
uongozi wao na majaliwa ya Mwenyezi Mungu sikuwaangusha. Nikafanikisha vyema
kama walivyonitarajia.
Uteuzi ule ulinipa fursa ya kushiriki vikao vyote vya Kamati za
Kudumu za Chama, Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa nikiwa mmoja wa
waandishi wa kumbukumbu za mikutano.
Kwa sababu hiyo basi tangu mwaka 1977
mpaka sasa nimebahatika kuhudhuria vikao vyote vya Halmashauri Kuu ya Taifa CCM
isipokuwa ule mwaka mmoja nilipohamishiwa Tabora kabla ya kuchaguliwa kuwa
Mjumbe wa NEC mwaka 1982.
Nimeyaona na kuyasikia mengi jambo ambalo
limenijengea msingi nzuri wa uongozi katika Chama. Kama kuna kitu nakifahamu
vizuri maishani ni kazi ya Chama.
SHUKRANI
KWA MARAIS WASTAAFU
Ndugu Wajumbe,
Napenda pia, kuwashukuru Mwenyekiti wa Kwanza wa CCM Mwalimu
Julius Nyerere na Katibu Mkuu na Makamu Mwenyekiti wa CCM Mzee Rashid Mfaume
Kawawa kwa kuwa wazazi na walezi wangu wazuri wa kisiasa.
Nawashukuru kwa
kutambua vipaji vyangu na kazi waliyofanya ya kunilea, kuniendeleza na
kuniongoza. Waliniamini na kunipa fursa iliyonijengea msingi mzuri ambao
naamini ndiyo ulionisadia kufika hapa ninapomalizia leo.
Natoa shukrani maalum kwa viongozi wangu wawili muhimu sana katika
maisha yangu ya kisiasa. Wa kwanza ni Mzee Ali Hassan Mwinyi, Rais wa Awamu ya
Pili na Mwenyekiti wa Pili wa CCM.
Namshukuru kwa kuniamini na kunifanya
nijulikane kwa Watanzania. Mimi sikuwa Mbunge, nilikuwa Mjumbe wa Halmashauri
Kuu ya Taifa na Katibu wa CCM Wilaya ya Masasi.
Uamuzi wake wa kuniteua kuwa Mbunge
na Naibu Waziri wa Nishati na Madini Novemba, 1988 na baadae Waziri wa Maji,
Nishati na Madini mwaka (1990) na Waziri wa Fedha (1994) ndivyo vilivyonifanya
nijulikane kwa Watanzania.
Wa pili ni Mzee Benjamin Wiliam Mkapa Rais wa Awamu ya Tatu na
Mwenyekiti wa Tatu wa CCM. Namshukuru kwa kuniamini na kunipa dhamana nzito ya
kuongoza diplomasia ya Tanzania kama Waziri wake wa Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Kimataifa kwa miaka 10 mfululizo.
Hii ilinipa fursa ya kuijua dunia na watu
duniani kunijua. Niliweza kujifunza mambo mazuri na yenye manufaa kwa nchi yetu
na kuwajua viongozi na watu duniani walioweza kuwa wa msaada na manufaa kwa
nchi yetu. Mambo hayo yalikuja kunisaidia sana katika kuliongoza Taifa letu.
Pia
namshukuru kwa kunipa fursa ya kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM katika kipindi
chote cha miaka 10 ya uongozi wake wa Chama chetu. Na jambo jingine muhimu namshukuru
kwa kunilinda kwani kama asingefanya hivyo huenda nisingekuwa hapa leo.
Mzee
Mkapa sitakusahau maishani.
Mzee Mwinyi na Mzee Mkapa sina kitu wala namna ya kuwalipa kwa
ihisani kubwa mliyonifanyia maishani. Nasema ahsanteni na tena ahsanteni sana.
Inshaallah Mwenyezi Mungu atawalipa kwa wema wenu.
Mimi nitaendelea kuwaombea
maisha marefu yenye afya njema, furaha na faraja tele.
SHUKRANI
MAKAMU WA MWENYEKITI
Ndugu Wajumbe,
Katika kipindi cha miaka 10 ya kuwa Mwenyekiti wa Chama nilifanya
kazi na Makamu wa Mwenyekiti wa CCM watano. Kwa upande wa Zanzibar ambako nako
tumekubaliana kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi
anakuwa Makamu Mwenyekiti nilianza na kaka yangu na swahiba yangu Dr. Amani
Abeid Karume.
Ninamalizia uongozi wangu na Dr. Ali Mohamed Shein, Rais wa sasa
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi. Wamekuwa wasaidizi makini wa
shughuli za Chama Zanzibar na bila ya wao sijui mambo yangekuwaje.
Kwa upande wa Tanzania Bara nilianza na Mzee John Samuel Malecela
ambae pia ni Makamu wa Rais na Waziri Mkuu Mstaafu. Pamoja na kunisaidia kwa
mengi yeye alikuwa mpambanaji wa mstari wa mbele kutetea na kupigania maslahi
ya Chama.
Nani asiyejua kazi ya Mzee Malecela kwenye chaguzi ndogo. Wa pili
alikuwa Mzee Pius Msekwa, Spika Mstaafu. Yeye alikuwa kama kamusi na hazina inayotembea
ya kumbukumbu za historia ya Chama na taifa. Alinisaidia sana kwa masuala ya Katiba ya Chama na nchi na Kanuni
mbalimbali za Chama. Wa tatu na wa mwisho ni Mzee Philip Mangula Makamu Mwenyekiti
aliyopo sasa. Yeye amesaidia sana kwa masuala ya maadili, nidhamu na udhibiti
katika Chama. Amekuwa maarufu kama Mzee wa Mafaili.
Ndugu Wajumbe,
Kwa jumla Makamu Mwenyekiti wote wamenisaidia sana kuifanya kazi
yangu ya Uenyekiti wa Chama kuwa rahisi hasa wakati nilipokuwa Rais wa nchi
yetu ambapo nafasi ya kujishughulisha na masuala ya Chama kwa kila siku ilikuwa
ndogo.
Bila ya msaada wao mambo yangekuwa magumu sana. Hivyo basi napenda
kukutoa hofu Rais wetu kwamba ukiwa na Makamu wa Mwenyekiti wazuri na Katibu
Mkuu mzuri na ukiwapa fursa ya kufanya kazi zao na wewe ukasaidia kwa upande wa
uwezeshaji utafanya kazi zako zote mbili vizuri. Hakuna jambo litakalo haribika
upande wowote.
Shukrani
Makatibu Wakuu na Watumishi wa CCM
Ndugu Wajumbe,
Vile vile nimefanya kazi na Makatibu Wakuu watatu. Wa kwanza
alikuwa Lt. Yusufu Rajabu Makamba. Alikuwa mtu wa watu, aliyeweza kuchanganyika
na watu wa makundi yote, rika zote na dini zote.
Alikuwa rasilimali kubwa kwani
kwa uwezo wa kujenga hoja alitusogezea watu wengi kuwa karibu na Chama. Wa pili
alikuwa Ndugu Wilson Mukama, msomi, mwanafalsafa na bingwa wa masuala ya
uchambuzi wa masuala ya kisiasa na kijamii.
Alitusaidia sana katika mchakato wa
kufanya mageuzi ndani ya Chama na kubuni na kupanga mikakati iliyosaidia katika
kuimarisha na ujenzi wa Chama.
Ndugu Wajumbe,
Wa tatu na ambae ndiye Katibu Mkuu aliyepo sasa ni Ndugu Col.
Abdulrahman Omar Kinana. Jembe la kazi. Jembe la Nguvu. Amefanya kazi kubwa na
nzuri isiyokuwa na mfano wake. Amefanya kazi adhimu iliyoleta uhai na mtazamo
mpya na chanya kwa Chama cha Mapinduzi. Juhudi zake zimeleta matumaini mapya ya
Watanzania na wanachama kwa Chama cha Mapinduzi.
Ni mtu wa mikakati, mbunifu wa
hali ya juu na wa mipango yenye tija na
maslahi kwa CCM. Katika miaka yake mitatu ya uongozi ametembelea Mikoa yote,
Wilaya zote na Majimbo yote ya uchaguzi. Amekutana na kuzungumza na wanachama
wa CCM na wananchi. Amefanya kazi ya kulima na ujenzi na kusikiliza shida za
wananchi Kwa ajili hiyo aliwafanya viongozi na wanachama wa CCM wajiamini.
Aidha
aliwafanya wananchi waendelee kuwa na imani na CCM hivyo kupeperusha matumaini
kidogo waliyokuwanayo jamaa zetu wa upande wa pili. Kwa kweli unapozungumzia
utulivu wa CCM baada ya mchakato wa uteuzi wa mgombea Urais mwaka jana uliokuwa
na majaribu mengi na mitihani isiyo na kifani, na unapozungumzia ushindi murua
tulioupata katika Uchaguzi Mkuu, huwezi kushindwa kuona na kutambua mchango
mahsusi wa Katibu Mkuu Ndugu. Abdulrahman Kinana. Ni jembe kweli kweli! Naomba
tumpigie makofi ya nguvu kuelezea pongezi na shukrani zetu kwake.
Ndugu Wajumbe,
Nawashukuru kwa dhati Wanachama, Wenyeviti na Makatibu wa Mikoa, Wilaya,
Majimbo, Kata na Matawi pamoja na Wajumbe wa Vikao vya Chama vya ngazi hizo kwa
ushirikiano na msaada mlionipa katika kipindi chote nilichokuwa Mwenyekiti wa
Chama chetu.
Ushirikiano na msaada wenu ndivyo vilivyofanya kazi yangu kuwa
nyepesi na tukapata mafanikio tuliyoyapata. Maombi yangu kwenu ni kuendelea
kukijenga na kukipigania Chama cha Mapinduzi kwa ari, nguvu na kasi kubwa zaidi
ya mlivyofanya wakati wangu.
Pili naomba mumpe Mwenyekiti mpya ushirikiano na
msaada maradufu zaidi kuliko mlivyofanya kwangu. Umoja na mshikamano ndiyo siri
ya mafanikio na ushindi wa CCM. Umoja ni Ushindi.
Ndugu Wajumbe,
Nawashukuru kwa namna ya kipekee watumishi wa Chama cha Mapinduzi
kwa moyo wao wa kujitolea, uzalendo na upendo kwa Chama chao. Nayasema haya kwa
dhati kwani nafahamu kuwa watumishi wa Chama wanalipwa ujira mdogo sana na
hawana marupurupu mengi.
Kutokana na hali ngumu ya kifedha inayokikabili Chama chetu
hata viposho vilivyokuwa vinasaidia kuleta nafuu havipo. Pamoja na hayo
wamekuwa wanachapa kazi usiku na mchana kujenga na kukipigania Chama cha
Mapinduzi.
Moyo wao wa kujitolea unastahili kutambuliwa na kupongezwa. Siku ile
ya tarehe 25 Juni, 2006 nilipochaguliwa kwa mara ya kwanza kuwa Mwenyekiti wa
Chama chetu niliahidi kuboresha maslahi ya wafanyakazi wa CCM. Nilitimiza ahadi
yangu.
Hata hivyo kwa vile tumeshindwa kuendelea kuboresha mishahara kila wakati
Serikali ilipoongeza kima cha chini cha mishahara kwa wafanyakazi nchini hali
ya watumishi wa Chama imeendelea kuwa ngumu.
Sipendi kumsemea Mwenyekiti mpya na wala kumtaka atoe kauli ya
matumaini siku ya leo. Lakini, ni jambo muhimu ambalo halina budi kutazamwa
mapema iwezekanavyo. Ilikuwa dhamira yangu kabla ya kuondoka tutoe nyongeza ya
mishahara lakini mipango haikwenda kama tulivyotarajia.
Shukrani
kwa Wajumbe wa Mkutano Mkuu
Ndugu Wajumbe,
Niruhusuni nitoe neno la shukrani kwenu, kwa imani kubwa
mliyoionyesha kwangu. Mara zote tatu
yaani 2006, 2007, na 2012 jina langu lilipoletwa mbele yenu kunipigia kura ya
kuwa Mwenyekiti mlinipa kura nyingi mno. Wingi ule wa kura ndiyo ulionidhihirishia
upendo wenu na imani yenu kwangu.
Mambo hayo ndiyo yaliyonitia moyo na kunipa
nguvu ya kukitumikia Chama kwa nguvu zangu zote na kwa kutumia vipaji vyangu
vyote nilivyojaaliwa na Mwenyezi Mungu. Ombi langu kwenu leo tufanye zaidi ya
vile mlivyofanya kwangu kwa ndugu yetu , Rais wetu mpendwa Mheshimiwa John
Pombe Magufuli.
Tumpigie kura zote za Ndiyo. Isipotee hata kura moja. Je tutafanya
hivyo wajumbe wenzangu? Hebu nithibitishieni! Tumekubaliana. Atakayefanya
kinyume ni Mchawi? na wachawi hawapo!
Kuimarisha Chama
Ndugu Wajumbe,
Mtakumbuka kuwa katika hotuba yangu ya kushukuru baada ya
kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Nne wa Chama cha Mapinduzi tarehe 25 Juni, 2006 nilizungumzia
kwa kirefu umuhimu wa kuendelea kufanya kazi ya uimarishaji wa Chama.
Nilikimithilisha
Chama chetu na mwili wa mwanadamu kuwa na viungo. Kama ilivyo mwanadamu kama
kiungo kimoja wapo kikikosekana huitwa mlemavu na kikipata maradhi huitwa
mgojwa. Nilisisitiza umuhimu wa viungo vya Chama kutimia na kufanya kazi
vizuri.
Ndugu Wajumbe,
Nilivitaja viungo vya CCM kuwa sita yaani Wanachama, Viongozi,
Vikao, Watendaji, Rasilimali na Jumuiya. Nilifafanua kwa kina na upana mambo ya
kufanya katika azma yetu ya kuimarisha Chama.
Chini ya uongozi mahiri na makini
wa Katibu Mkuu wa CCM Lt. Yusuph Makamba ulitengenezwa Mradi wa Kuimarisha
Chama Awamu ya Tatu uliozinduliwa Oktoba 2006.
Katika historia ya Chama hii
ilikuwa mara ya tatu kuwa na Mradi wa namna hiyo. Mradi wa Kwanza ilikuwa mwaka
1961, Mwalimu alipojiuzulu Uwaziri Mkuu na kufanya kazi ya kuimarisha Chama.
Wa
pili ilikuwa mwaka 1987 Mwalimu Julius Nyerere Mwenyekiti wa Kwanza wa CCM,
aliobuni na kutekeleza chini ya uongozi wake baada ya kustaafu Urais.
Ndugu Wajumbe,
Leo miaka kumi baadae ninaponga’atuka napenda kutoa taarifa fupi
ya hatua tuliyofikia katika uimarishaji wa Chama.Kufanya hivyo kutamsaidia
Mwenyekiti mpya kujua mahali tulipo na hasa pale pa yeye kuanzia katika kazi
hii mama na ya msingi kwa uhai na ustawi wa Chama chetu.
Kazi ya kuimarisha
Chama ni ya kudumu na ni ya kila siku kwa Viongozi na Wanachama. Ni kazi
endelevu. Tunapoifanya kwa ufanisi mambo yote yanakuwa mazuri na taswira ya CCM
katika jamii inakuwa nzuri. Imani iliyoonyeshwa na Watanzania kwa Chama chetu
katika uchaguzi uliopita ilitokana na Watanzania kuona mafanikio tunayoendelea
kuyapata katika dhamira yetu ya kurekebisha baadhi ya mambo waliyokuwa
hawayapendi kuhusu Chama chetu.
Wanachama
Ndugu Wajumbe,
Kwa upande wa wanachama tumepata mafanikio makubwa. Watanzania
wengi wamejiunga na Chama cha Mapinduzi kuthibitisha kukubalika na kuaminika
kwa Chama chetu. Hivi sasa CCM ina wanachama 8,782,833 ukilinganisha na
5,433,325 waliokuwepo mwaka 2006. Hili ni ongezeko kubwa sana.
Jambo la kutia
faraja kuhusu wanachama wa CCM ni moyo wao wa kukipenda Chama chao na
kukipigania kwa nguvu zao zote. Wamedhihirisha hivi katika chaguzi zote. Wanachama
wa CCM ni rasilimali na mtaji mkubwa
katika uchaguzi.
Wanachama wetu ni kura nyingi za kuanzia. Wanachama wetu wamekuwa
wakifanya kazi kubwa ya kuomba kura kwa wananchi wengine. Hivyo basi, kazi ya
kuingiza wanachama wapya haina budi kuendelea na kuendelezwa kwa bidii na
maarifa zaidi.
Ndugu Wajumbe,
Kuna mambo mawili ambayo wanachama wetu wanatakiwa kujirekebisha
kwa maslahi ya Chama cha Mapinduzi sasa na mbele tuendako. Jambo la kwanza
linahusu ushiriki wao katika vikao kutokuwa wa kiwango cha kuridhisha. Kwa
sababu hiyo wanachama wanakosa au kujinyima fursa ya kuzungumzia mambo yenye
maslahi kwa Chama chao na nchi. Lazima wana-CCM watambue kuwa uhai na vuguvugu
la Chama linakuwepo pale wanachama wanapokutana kuzungumza na kukubaliana jambo
na mambo ya kufanya.
Wasipokutana inakuwa kila mtu na lwake na wengine
kutokushughulika kabisa. Hii haikubaliki na isiachwe kuendelea.
Pia kwamba, kwa vile Serikali ni ya CCM wanachama wanao wajibu wa
kiuongozi katika maeneo yao wanayoishi. Wanapokutana kwenye vikao vya Chama
wanao wajibu wa kuzungumza mambo ya Chama, utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi na
masuala yanayohusu maendeleo na matatizo ya wananchi katika eneo lao. Kwa vile
wao ndiyo Chama tawala ni rahisi kuwasiliana na mamlaka husika za Serikali
kutoa taarifa, kuuliza maswali na kupata majibu.
Wakifanya hivyo na hatua
zikachukuliwa au kuwapatia wananchi majibu na ufumbuzi wa matatizo yao,
wanajenga imani kwa CCM na Serikali yake. Kwa ajili hiyo, inaifanya kazi ya CCM
kuwa nyepesi wakati wa uchaguzi.
Ndugu Wajumbe,
Jambo la pili ni wanachama kutokulipa ada na michango ya
kuimarisha Chama. Kutokufanya hivyo kunakipunguzia Chama chetu uwezo wa
kutekeleza ipasavyo majukumu yake.
Kwa idadi hii ya wanachama CCM haingestahili
kuwa na matatizo ya fedha wakati wote. Ada ya uanachama peke yake ingeipatia
CCM zaidi ya shilingi bilioni 10.5 kwa mwaka.
Zingetuwezesha kufanya mambo
mengi sana. Lakini wanachama wengi hawalipi ada. Kwa mfano, katika bajeti ya
Chama iliyopita ilikadiriwa kupata shilingi 800 milioni kutokana na ada lakini
zilizopatikana ni milioni 500 tu. Hili ni jambo baya ambalo halikubaliki hata
kidogo na hatuwezi kuliacha kuendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti unaesubiri kuthibitishwa, nakuachia kazi
hii. Tumia maarifa na ujuzi wako kupata ufumbuzi wa matatizo ya wanachama
kushiriki vikao vya Chama vinavyowahusu, walipe ada zao na kutoa michango ya
kuimarisha Chama.
Viongozi
Ndugu
Wajumbe,
Kwa upande wa viongozi nafurahi kwamba namaliza ngwe yangu safu ya
uongozi ikiwa imekamilika katika ngazi zote isipokuwa pale ambapo kuna mapengo
yaliyotokana na vifo hivi karibuni. Nafurahi pia, kwamba mapengo yaliyotokana
na baadhi ya viongozi kufariki, kuachishwa uongozi au kuhama Chama na kujiuzulu
siku za nyuma yamekwishazibwa.
Viongozi wa Chama wanastahili pongezi maalum kwa
uongozi wao nzuri. Mwaka jana walithibitisha uhodari na ushupavu wao katika
kuhakikisha CCM imeibuka kidedea kutokana na jinsi walivyowaongoza wanachama na
wananchi.
Pamoja na hayo kuna mambo mawili kuhusu viongozi wa CCM ambayo
ningependa kuyasemea. Kwanza, kwamba viongozi wetu wamekuwa wazito kutoka na
kwenda kwa wanachama na wananchi.
Kwa sababu hiyo kazi ya Chama ndani ya Chama
na kazi ya Chama nje ya Chama ndani ya Umma hazifanyiki ipasavyo. Siasa ni
kufikisha ujumbe kwa watu wakuunge mkono. Hivi usipotoka watu wakakuona na
kukusikia wanakuungaje mkono? Lazima tujirekebishe.
Ndugu Wajumbe,
Siku za nyuma viongozi walilalamikia kukosa magari mazuri, tumewaletea
Toyota Land Cruiser Hardtop kila Mkoa na kila Wilaya. Tena zenye uwezo wa
kubeba viongozi wengi kwa wakati mmoja.
Pia tumesambaza pikipiki na baiskeli
nyingi. Lakini, bado viongozi hawatoki na wengine wamediriki hata kudai hawana
hela ya mafuta au hata ya kununulia matairi na kulipia bima ya magari. Kwa
kweli inaudhi na kukatisha tamaa.
Hivi ndugu zangu mnataka Makao Makuu waliowanunulia
hizo gari ndiyo waje kuwapatia na hela za mafuta, bima, kubadili matairi na
matengenezo ya kawaida. Waswahili wana msemo “ukibebwa shikilia” baadhi yenu
mmejilegeza mno kiasi cha kufanya tuwe tunaulizana swali la kulikoni bila ya
majibu sahihi. Je ni kutokujua wajibu, woga, uzembe au kutokuwa na mapenzi ya
dhati na CCM?
Ndugu Wajumbe,
Jambo baya na la kusikitisha ni kwamba, wakati viongozi wetu wa
CCM hawaendi kwa wanachama na wananchi, wenzetu wa vyama vya watani zetu
wanatoka.
Matokeo yake ni kuwapa fursa ya kujijenga kwa kupotosha wananchi na
kuifanya kazi ya uchaguzi kuwa nzito bila ya sababu. Tunalazimika kutumia nguvu
kubwa kutafuta ushindi isivyokuwa lazima. Kwa huko mbele tuendako lazima
viongozi wa CCM wabadilike.
Tusipobadilika na kufanya kazi na wanachama wetu na
miongoni mwa wananchi mambo yanaweza kutuharibikia, balaa ambalo hatutaki
litokee.
Ndugu Rais na Mwenyekiti mtarajiwa,
Nakuomba uitambue hali hii wakati unapopokea kijiti cha kukiongoza
Chama chetu. Tusiiache ikaendelea. Naomba uchune bongo na kama hapana budi
kufanya kazi ya ziada kuipatia ufumbuzi thabiti. Kwa kweli hapa ndipo
ninaporudia kumpongeza kwa dhati, Katibu Mkuu Ndg. Abdulrahman Kinana kwa
kuonyesha mfano kwa vitendo jinsi viongozi wa Chama wanavyotakiwa kuwa.
Kila
alipotembelea Wilaya na Mikoa alikutana na kuzungumza na wanachama na wananchi
katika maeneo yao. Naambiwa baadhi ya viongozi wa maeneo hayo ilikuwa ndiyo
mara yao ya kwanza kufika.
Wamekuwa wanashangaa jinsi wanachama na wananchi
walivyokuwa wanajitokeza kwa wingi na kufurahia kutembelewa na kusikilizwa.
Jambo la kushangaza ni kwamba badala ya kuendeleza utaratibu wanarudia kutotoka
na kuomba Katibu Mkuu au Katibu wa Itikadi na Uenezi Ndg Nape Nnauye afanye
ziara nyingine.
Vikao.
Ndugu Wajumbe,
Vikao ni kitu muhimu sana katika uhai na ustawi wa Chama cha
Mapinduzi. Vikao ndicho chombo kikuu cha uamuzi na uendeshaji wa Chama kwa
mujibu wa Katiba ya Chama cha Mapinduzi. Mfumo wa Chama umejengeka juu ya vikao kufanya uamuzi na siyo kiongozi binafsi.
Hata Mwenyekiti au Katibu anapotaka jambo lake sharti alifikishe kwenye kikao
kwa uamuzi isipokuwa yale ambayo ni utekelezaji wa maamuzi ya vikao vilivyopita
au Katiba ya Chama imewapa mamlaka ya kufanya hivyo.
Na, kwa vyo vyote vile
hayatakuwa mambo yahusuyo kubadili itikadi na sera za msingi za Chama au
kubadili masharti ya Katiba ya Chama. Mambo ya namna hiyo huletwa kwenye kikao
na wajumbe hupewa fursa na uhuru wa kujadili na kuamua wanavyoona inafaa.
Ndugu Wajumbe,
Kwa sababu ya umuhimu huo wa vikao katika uamuzi na uendeshaji wa
Chama kufanyika kwake kwa mujibu wa Katiba ni jambo la msingi sana. Ndiyo maana
kila mwaka Chama hutoa ratiba ya vikao vya Chama kwa ngazi zote kama mwongozo
kwa wote.
Taarifa zinaonesha kuwa hali ya ufanyikaji wa vikao vya kawaida vya
Chama ni ya wastani na kwa baadhi ya ngazi ni chini ya wastani. Kuna kujitokeza
tabia ya vikao maalumu hasa vile vihusuvyo uteuzi wa wagombea na uchaguzi
hufanyika kama inavyotakiwa.
Hali hii si nzuri kwa ustawi wa Chama. Unakifanya
Chama chetu kiwe hai wakati wa uchaguzi na siyo wakati wote kabla, wakati na
baada ya uchaguzi. Hali hii haifai kuachwa kuendelea kwani inakinyima Chama
chetu fursa muhimu ya kujijenga na kujiimarisha.
Upungufu huu lazima utafutiwe
ufumbuzi kwa maslahi mapana ya Chama chetu. Hatuwezi kusubiri mpaka wakati wa mchakato
wa uchaguzi. Ipo siku tunaweza kujikuta tumezingirwa kila upande tukashindwa
kujinasua au kukosa pa kuchomokea.
Watendaji
wa Chama
Ndugu Wajumbe,
Kwa Chama cha Mapinduzi kuwa na watendaji wazuri ni jambo lenye
umuhimu wa aina yake kwa ustawi na uhai wa Chama. Inatoa uhakika kwamba
kumbukumbu za vikao, fedha na mali za Chama zitaandikwa na kuhifadhiwa vizuri.
Pili kwamba mipango na shughuli za kiutawala za Chama zitaendeshwa vizuri.
Watendaji wa Chama wanapokosekana au wanapokuwa ni wa kiwango cha chini cha
ubora ni hasara kwa Chama. Uwezo wa Chama kutimiza wajibu wake unakuwa
umedhoofika sana. Kwa vile CCM ni Chama cha siasa tena katika mfumo wa vyama
vingi watendaji wake siyo tu wawe hodari kwa kazi zao bali lazima pia wawe
waumini wa dhati wa sera, siasa, imani na madhumuni ya Chama cha Mapinduzi.
Katika kipindi cha miaka 10 iliyopita tumechukua hatua za maksudi
za kuajiri vijana wasomi katika utumishi wa Chama. Msimamo huu ukiendelezwa
baada ya muda si mrefu tutakuwa na watumishi wasomi katika kada zote ngazi za
Wilaya, Mkoa na Taifa.
Jumuiya za Chama nazo zihimizwe kufanya hivyo. Jumuiya
ya Vijana iko mbele ya Jumuiya za Wanawake na Wazazi kwa hili. Lazima,
zisisitizwe kubadilika kwani huko mbele tuendako elimu ya watendaji na viongozi
wetu ni sifa na mtaji muhimu. Pamoja na hayo Chama kiendelee kuelimisha
watendaji wake kuhusu namna ya kufanya kazi ya Chama.
Rasilimali
za Chama
Ndugu Wajumbe,
Nilipozungumzia rasilimali kama moja ya viungo vikuu vya Chama cha
Mapinduzi nilizungumzia Chama kuwa na majengo ya ofisi mazuri yanayolingana na
hadhi ya Chama kikubwa kama CCM.
Pia nilizungumzia Chama kuwa na fedha za
kutosha za kuendesha shughuli zake, vitendea kazi, na miradi ya kiuchumi ya
kukipatia fedha. Leo miaka 10 baadae ninapomaliza kipindi changu cha uongozi
kwa upande wa Makao Makuu tumekamilisha ujenzi wa ukumbi wa mikutano ambao
ndiyo huu.
Tumejenga jengo jipya zuri na la kisasa katika Ofisi Ndogo ya Makao
Makuu, Dar es salaam na ukarabati mkubwa unaendelea kufanyika Afisi Kuu ya CCM
Kisiwandui pamoja na kuweka samani mpya. Kwa hapa Dodoma kazi ambayo
haijakamilika ni ujenzi wa jengo la Ofisi ya Makao Makuu na jengo la kitega
uchumi.
Kazi hiyo sasa namuachia Mwenyekiti mpya na safu ya uongozi atakayoiunda.
Hali kadhalika, majengo mazuri ya Ofisi yamejengwa katika Mikoa, Wilaya,
Majimbo, Kata na Matawi kote nchini. Kila Ofisi ya Wilaya na Mikoa imepatiwa
gari na pikipiki zipo katika baadhi ya Ofisi za Wilaya, na Kata. Matawi mengi
yamepatiwa baiskeli.
Lakini sina budi kusema mbele yenu kuwa tumshukuru na kumpongeza
Katibu Mkuu Ndugu Abdulrahman Kinana kwa ubunifu wake. Ni mtu aliyebobea kwa
mikakati na mipango.
Siyo tu imetuwezesha kujenga huu ukumbi lakini pia
imetuwezesha kupata hayo magari, pikipiki,
baiskeli na mahitaji mengine muhimu ya kuendesha Chama kabla, wakati na baada
ya kampeni za uchaguzi.
Ndugu Wajumbe,
Changamoto yetu kubwa ambayo lazima nikiri sikuweza kuipatia
jawabu la kudumu na endelevu ni Chama kukosa vyanzo vya uhakika vya kujipatia
rasilimali fedha.
Kwa sasa chanzo kikubwa na cha uhakika cha mapato kwa Chama
chetu ni ruzuku ya Ubunge na Udiwani. Aghalab fedha hizo zote hutumika kulipia
mishahara ya watendaji na watumishi wa Chama. Fedha kwa ajili ya kuendeshea
shughuli nyingine muhimu za Chama kama vile vikao au ziara za viongozi
kuhamasisha uhai wa Chama na kuimarisha Chama upatikanaji wake si wa uhakika.
Mara kadhaa imebidi hata Mwenyekiti uingilie kati kutafuta ndipo baadhi ya
shughuli muhimu zifanyike.
Nikuombe Mwenyekiti Mtarajiwa kwamba suala la Chama kuwa na vyanzo
vya uhakika vya mapato ulipe kipaumbele cha juu. Hali kadhalika uendelee kuwabana viongozi wa
Mikoa na Wilaya kutilia maanani uanzishwaji wa mifuko ya uchaguzi.
Utekelezaji
wake unasuasua. Napata shaka kwamba viongozi wetu wengi hawaoni umuhimu wa
kufanya hivyo. Naona kama vile wamejenga dhana potofu ati kuwa yupo mwenye
Chama chake ambae ni Chama ngazi ya Taifa. Wao wanajifanya kana kwamba
hawahusiki.
Hata maagizo ya kuanzisha shughuli za kiuchumi Chama kijitegemee hayatiliwi
maanani. Kama yangelitiliwa maanani CCM isingekuwa katika hali ngumu ya kifedha
iliyopo sasa.
Ndugu Wajumbe,
Chama kina rasilimali nyingi ambazo zikitumika zinaweza kuboresha
sana hali yake ya kifedha. Mkoani Dar es salaam kwa mfano, Chama kina jumla ya
viwanja 279 katika ngazi mbalimbali. Vingeweza kuwa chanzo muhimu cha miradi ya
kiuchumi kama wafanyavyo watu wengine binafsi wenye viwanja.
Umoja wa Vijana
wameonesha mfano mzuri wa kutumia viwanja kujenga majengo makubwa ya
kitegauchumi. UWT nao wamefanya hivyo. Naamini wengine nao wangeweza kuiga
mifano hiyo mizuri.
Jambo lililo muhimu ni kuhakikisha wanakuwa na mikataba mizuri
pale wanapoingia ubia. Mimi naamini tukichangamkia uwekezaji na kuitumia vyema
rasilimali ya viwanja na ardhi tuliyonayo CCM inaweza kabisa kujiondolea
unyonge wa uhaba wa fedha.
Zoezi la uhakiki wa viwanja vya Chama linahitaji
kupewa msukumo maalum linakwenda pole pole mno. Kukamilika kwake ndiko kutatoa
uhakika wa milki ya CCM kwa viwanja hivyo. Isijekuwa watu wameshajimilikisha au
kuviuza viwanja hivyo kinyemela.
Jumuiya za Chama
Ndugu Wajumbe,
Kuhusu Jumuiya za Chama nilifafanua, siku ile na mara kadhaa
kwamba zina jukumu na wajibu maalum kwa Chama. Nao ni kukitafutia Chama
wanachama, marafiki, wapenzi na watu wa kukiunga mkono na kukipigia kura wakati
wa uchaguzi kutoka katika jamii pana ya Watanzania.
Pamoja na kuwepo kwa
changamoto za hapa na pale Jumuiya za Chama zimekuwa zikitimiza vizuri majukumu
yake hayo. Hata Jumuiya ya Wazazi ambayo iliamuliwa ifutwe kwa sababu ya
kutoridhishwa na kazi zake safari hii imejitahidi. Alhaj Abdallah Bulembo
Mwenyekiti wa Wazazi amefanya kazi nzuri sana inayostahili pongezi.
Hata hivyo
wajue kuwa uamuzi ule haujafutwa, hivyo waendelee kujitengenezea uhalali. Na
pengine la haraka zaidi ni lile la Shule za Wazazi ambazo haziendeshwi vizuri.
Chama kiliagiza ziuziwe Serikali Kuu au Halmashauri lakini bado kuna uzito wa
kufanya hivyo. Inatoa sura na sifa mbaya kwa Jumuiya ya Wazazi na Chama chenye
Jumuiya yake.
Ndugu Wajumbe,
Bahati mbaya, Jumuiya bado zimeendelea kuwa tegemezi kwa CCM
kulipa mishahara ya watendaji na watumishi wao. Hata pale walipokuwa na miradi
ya kuwaingizia mapato kama walivyo UWT na UVCCM kwa majengo na Wazazi kwa shule
zake hawakuacha kuomba na kupokea ruzuku kutoka CCM.
Pengine wakati umefika
kusisitiza Jumuiya za Chama ziendelee kuchukua hatua za kujitegemea na kuanza kuchangia
katika mapato ya Chama cha Mapinduzi.
Shirikisho la Wanafunzi wa
Vyuo vya Elimu ya Juu
Ndugu Wajumbe,
Katika kipindi hiki pia
tulianzisha Shirikisho la Wanafunzi wa Vyuo vya Elimu ya Juu. Moja ya sifa ya
Chama makini cha siasa kama CCM, kinachohitaji kudumu katika uongozi, ni
kutayarisha kada ya viongozi wapya, wenye sifa na maono ya nyakati zinazokuja.
Chama chetu kinayo Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa CCM ambao kwa miaka mingi limekuwa
tanuru la kupika viongozi wa Chama chetu na taifa letu. Hata hivyo, kwa
kuzingatia ongezeko kubwa la wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu nchini katika
kipindi cha miaka 10 iliyopita, na kwa kuzingatia kwamba vyuoni ndiko kumekuwa
na harakati kubwa za kisiasa, Ndipo tulipoamua kuanzisha Shirikisho hilo.
Hii ilikuwa
sehemu ya mageuzi ya ndani ya Chama na madhumuni yake ni kuhakikisha kwamba tunapata
wanachama wapya na kuungwa mkono na kundi hili muhimu la wasomi katika nchi
yetu. Pia ni fursa ya aina yake ya kutayarisha viongozi wajao wa CCM na Taifa
kutoka miongoni mwao.
Ndugu Wajumbe,
Faida za kuwepo kwa
Shirikisho hili zimeanza kuonekana. Kwanza kabisa imeondoa dhana potofu iliyokuwepo
zamani eti kwamba wasomi wa vyuo vya elimu ya juu wanapenda upinzani zaidi
kuliko CCM.
Chama chetu kimevuna wanachama wengi zaidi na kina washabiki wengi
zaidi kwenye vyuo. Pili katika uchaguzi uliopita Shirikisho limefanya kazi
kubwa na nzuri ya kuhamasisha jamii kuiunga mkono CCM.
Napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza
viongozi wa Shirikisho na Mlezi wake Ndugu January Makamba, Mjumbe wa
Halmashauri Kuu ya Taifa, kwa kuliwezesha Shirikisho kufika hapo lilipo na
kusimama imara. Sisi viongozi wa Chama tuendelee kuchukua hatua ya kuliwezesha Shirikisho
hilo liendelee kuwalea vijana hawa wa CCM.
Uwezo wa Chama Kutumia
TEHAMA
Ndugu Wajumbe,
Katika mambo yenye tija
ambayo tumeyafanya katika mageuzi ya ndani ya CCM ni pamoja na kujenga uwezo wa
Chama chetu kuingia katika ulimwengu mpya wa teknolojia ya habari na
mawasiliano (TEHAMA).
Pamoja na ukongwe wake, matumizi ya TEHAMA yamefanya
Chama chetu kiende na wakati na kiwafikie watu wengi na hasa vijana. Uwekezaji
wa miundombinu ya kisasa ya TEHAMA katika Ofisi Ndogo ya Lumumba umewezesha
mawasiliano na usambazaji wa taarifa kwa haraka na umekiwezesha Chama chetu
kupambana vyema na kuleta uwiano wa nguvu za mapambano ya kimtandao.
Nyote
mlishuhudia katika uchaguzi mkuu uliopita jinsi nguvu ya CCM ilivyojidhihirisha
mitandaoni. Uwezo huo tumeujenga katika kipindi hiki kifupi. Kwa uwezo wetu
huu, taarifa za Chama chetu zina uwezo wa kuwafikia watu zaidi ya milioni na kuendelea
kwa wakati mmoja, popote walipo. Hii ni zaidi ya watu wanaosoma magazeti
na kuangalia TV hapa nchini.
Vyombo vya Habari vya
Chama
Ndugu Wajumbe,
Ufanisi wa Chama chochote
cha siasa kueneza sera zake, malengo yake, shabaha zake na mafanikio yake kwa
jamii unachangiwa kwa kiasi kikubwa na uwezo wake wa kuwasiliana na umma.
Pamoja
na kutumia TEHAMA, Chama chetu kinavyo vyombo vyake vya habari kwa ajili hiyo.
Tuna magazeti mawili ya Uhuru na Mzalendo na Radio mbili yaani, Uhuru fm na
Bahari Fm. Vyombo vyetu hivyo vimekuwa vinafanya kazi kubwa na nzuri ya kueneza
ujumbe wa CCM kwa umma.
Hata hivyo vimekuwa vinakabiliwa na changamoto
mbalimbali za uendeshaji zinazovifanya visifikie pale tunapopakusudia. Katika kipindi
cha uongozi wangu wa Chama chetu, tumechukua hatua mbalimbali za kuimarisha
vyombo vya habari vya CCM.
Ninayo furaha kuwajulisha
kwamba tunanunua mtambo mpya wa uchapishaji ambao utaimarisha magazeti yetu na
kufanya kazi za watu wengine kibiashara. Radio Uhuru, tumeiongezea uwezo wa
vifaa, fedha na rasilimali-watu ili isikike maeneo mengi zaidi hapa nchini.
Hata hivyo mipango iko mbioni kuijengea uwezo mkubwa zaidi wa kusikika kwa
urahisi zaidi kote nchini. Mwaka jana tumefungua redio mpya inayoitwa Bahari FM
kule Zanzibar ambayo nayo tumedhamiria kuiboresha zaidi.
Sambamba na vyombo hivi,
tumeendelea na mpango wa kufungua Televisheni ya Chama, ambapo hatua mbalimbali
za utangulizi zimekamilika ikiwemo ya kupata leseni ya matangazo. Matayarisho
ya kuiwezesha TV yetu irushe matangazo mapema iwezekanavyo yanaendelea. Sina
wasiwasi kwamba Mwenyekiti ajae atatoa msukumo mkubwa zaidi.
Mafunzo ya Uongozi, Siasa na Itikadi
Ndugu Wajumbe,
Chama imara ni kile chenye makada,
viongozi na watendaji waliopikwa na kufundwa wakaiva vizuri katika elimu ya
siasa, itikadi ya Chama, uongozi na
mbinu na mikakati ya ushindani wa kisiasa.
Katika miaka kumi iliyopita
tumeongeza kwa kiasi kikubwa idadi ya makada na viongozi waliopata mafunzo
ndani na nje ya nchi. Kwa hapa ndani tumekuwa tunatumia Chuo cha Ihemi na
semina na warsha mbalimbali kutoa mafunzo kwa makada wetu. Kupitia ushirikiano
wetu na Chama cha Kikomunisti cha China tumepeleka makada wa Chama 80 kwa
mafunzo nchini China.
Ndugu Wajumbe,
Niliahidi
kwamba nitajitahidi kwa kadri ya uwezo wangu Chama chetu kiwe na Chuo chake
pale Ihemi, kutoa mafunzo kwa viongozi na makada wa Chama. Juhudi za
kukiimarisha Chuo cha Ihemi zinaendelea.
Ninayo furaha kuripoti kwenu pia kwamba
tumekamilisha taratibu za kujenga chuo kikubwa cha kimataifa kwa ajili ya kutoa
mafunzo kwa makada wa Chama.
Chuo hicho kitajengwa Kibaha kwa kushirikiana na vyama rafiki vya ukombozi yaani FRELIMO, MPLA,
ZANU PF, SWAPO, na ANC na marafiki zetu wa Chama cha Kikomunisti cha China.
Makada wetu na wa vyama hivyo watapatiwa mafunzo katika Chuo hicho ambacho
kitakuwa na ubora wa kimataifa.
Hii ni hatua muhimu sana
kwani sasa tutajenga kada ya viongozi na watendaji wa Chama walioandaliwa
vizuri kisiasa , kiitikadi, uendeshaji wa shughuli za Chama, uchaguzi na kwa
mambo mbalimbali ya dunia ya sasa. Kuwepo kwa Chuo hicho kutaimarisha sana
viongozi, watendaji na makada wa CCM na vyama rafiki.
Ushindi Katika Chaguzi
Mbalimbali
Ndugu Wajumbe,
Katika kipindi cha miaka 10 mliyonipa heshima ya kuwa Mwenyekiti,
Chama chetu kimeshiriki Uchaguzi Mkuu mara mbili yaani 2010 na 2015 na marudio
ya mwaka 2016 kwa Zanzibar.
Katika chaguzi zote hizo tumefanikiwa kutimiza madhumuni
ya Ibara 5 (i) kwa kushinda uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Wawakilishi na kupata viti vingi
vya Wabunge, Wawakilishi na Madiwani.
Kwa ajili hiyo tumeweza kuendelea
kukamata dola kwa sehemu zote mbili za Muungano. Katika kipindi hicho pia tulishiriki
katika chaguzi mbili za Serikali za Mitaa kwa upande wa Tanzania Bara na kupata
ushindi mkubwa sana. Katika uchaguzi wa viongozi wa mitaa, vijiji na vitongoji
mwaka 2009 tulipata ushindi wa 91.72% na mwaka 2014 tulipata 80.58%. Nani kama
CCM?
Ndugu Wajumbe,
Katika kipindi hiki pia, tulishiriki katika chaguzi
ndogo za Ubunge katika Majimbo manane ya Kiteto, Tunduru, Tarime, Busanda,
Mbeya Vijijini, Biharamulo Magharibi, Igunga na Arumeru Mashariki. Pamoja na
ushindani mkali uliokuwepo tulishinda katika majimbo sita. Pia tulishiriki
katika chaguzi ndogo za udiwani katika Kata 31, na tulishinda katika Kata 25 kati
ya hizo. Nani kama CCM?
Ndugu Wajumbe,
Ushindi tuliopata katika chaguzi zilizofanyika katika
ya kipindi cha miaka 10 ya uongozi wangu ni ishara tosha kwamba CCM imeongoza
vizuri nchi yetu na Chama chetu kimeendelea kuaminiwa na kukubalika kwa
Watanzania. Pia ni ushahidi wa ubora wa
mikakati na mipango yetu ya uchaguzi pamoja na umahiri na umakini wa Viongozi na Wanachama wa
CCM katika utekelezaji. Napenda kuchukua fursa hii kurudia kuwapongeza
viongozi, wanachama, makada, washabiki na wapenzi wa CCM kote nchini kwa kazi
nzuri waliyoifanya katika kukipigania na kukipatia ushindi Chama chetu. Napenda
pia kuwashukuru Watanzania kwa kuendelea kuonyesha imani kubwa kwa Chama cha
Mapinduzi. Nani kama CCM.
Ndugu Wajumbe,
Kwa kweli, ninaona fahari kwamba, wakati namaliza ngwe
yangu ya uongozi, CCM imeendelea kuwa madarakani sehemu zetu zote mbili za
Muungano. Malengo na madhumuni ya msingi ya kuundwa kwa CCM ya kushinda chaguzi
na kushika dola Tanzania nzima na Zanzibar yametimia. Kazi hii sikuifanya peke
yangu. Tumeifanya wote. Ushindi tulioupata chini ya Uenyekiti wangu, haukuwa
ushindi wangu binafsi bali ni ushindi wa Chama cha Mapinduzi. Ushindi wa
viongozi, wanachama na wapenzi wa CCM. Ni matunda ya kazi nzuri tuliyofanya ya
kujenga viongozi, makada, watendaji na wanachama wenye uwezo na uzoefu wa kuendesha
chaguzi. Tumejenga mikakati, mbinu na miundombinu ya kutafuta ushindi, ambayo
imeweka msingi imara kwa ushindi wa Chama chetu kwa miaka mingi ijayo.
Ilani
ya Uchaguzi
Ndugu Wajumbe,
Ni mazoea ya Chama cha Mapinduzi kushindana
katika chaguzi za dola kwa hoja. Kwa kawaida hoja za Chama chetu huandikwa na kuchapishwa
katika Ilani ya Uchaguzi kwa Uchaguzi Mkuu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Rais wa Zanzibar, Wabunge, Wawakilishi na Madiwani. Kwa uchaguzi wa
Serikali za Mitaa kwa upande wa Tanzania Bara, CCM imekuwa inatoa kijarida
kinachoitwa Tamko la CCM kuhusu Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Maandiko hayo
mawili huelezea nia na makusudio ya Chama cha Mapinduzi kushiriki katika
chaguzi hizo. Aidha Chama hufafanua mambo ambayo kinakusudia kuyafanya kwa
ajili ya maendeleo ya nchi yetu na watu wake iwapo tutapata ridhaa ya kuongoza.
Wagombea wa Chama pamoja na Viongozi, wanachama na wapenzi wa CCM hutumia
maandiko hayo katika kuomba kura kwa wananchi.
Baada ya Uchaguzi, na hasa baada ya
kushinda CCM huwa makini katika kufuatilia utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi na
Tamko la CCM. Katika kufanya hivyo Chama huwataka Viongozi wa Serikali Kuu na
Serikali za Mitaa ambao ndiyo wana dhamana ya utekelezaji kutengeneza mkakati
na mipango ya utekelezaji na kutoa taarifa ya utekelezaji kwenye vikao vya
Chama vya ngazi husika, yaani Wilaya, Mkoa na Taifa.
Ni wajibu wa Serikali katika
ngazi zote husika kutoa taarifa ya utekelezaji. Huo ni wajibu na wala sio
hiyari au ihsani wanayoifanyia CCM. Ni kutokana na wajibu huo ndio maana Rais,
Makamu wa Rais na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano pamoja na Rais wa Zanzibar
na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ni Wajumbe wa Kamati Kuu, Halmshauri Kuu
ya Taifa na Mkutano Mkuu wa Taifa wa CCM. Hali kadhalika, Wakuu wa Mikoa na
Wakuu wa Wilaya ni Wajumbe wa Kamati za Siasa, Halmashauri Kuu za Chama na
Mikutano Mikuu ya Chama katika ngazi zao husika.
Viongozi hao wakuu wa Serikali
ndio makamisaa wa Chama na kiungo kati ya Chama tawala na Serikali katika ngazi
zao husika za uongozi.
Ndugu Wajumbe,
Kuwa na ilani nzuri na utekelezaji mzuri
wa Ilani na ahadi za viongozi wa Serikali na Chama ndio siri kubwa ya CCM
kuendelea kuaminiwa, kukubalika na hivyo kuchaguliwa kuendelea kuongoza nchi
yetu. Wosia wangu kwa Mwenyekiti mpya, Makamu Mwenyekiti Zanzibar pamoja Viongozi na Wanachama wenzangu wa CCM ni
kudumisha na kuendeleza utaratibu huu nzuri wa Chama kufuatilia utekelezaji wa
Ilani ya uchaguzi ya CCM unaofanywa na Serikali zake. Ni jambo lenye manufaa na
maslahi makubwa kwa Chama chetu.
Ndugu Wajumbe,
Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya
Mwaka 2015 – 2020 uko mikononi kwa
Mheshimiwa Dr John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, kwa mambo ya muungano na Tanzania Bara. Kwa mambo yahusuyo Zanzibar
uko mikononi mwa Mheshimiwa Dr Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti
wa Baraza la Mapinduzi ambaye yupo katika kipindi chake cha pili.
Rais wa jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ndiyo kwanza ameanza bahati nzuri ameanza vizuri. Kwa kweli tumembebesha
mzigo mkubwa sana kwenye Ilani hii na hivyo ana kazi kubwa ya kutafuta
rasilimali.
Ninachomshukuru na kumpongeza ni kwamba ameupokea mzigo huo kwa
moyo mkunjufu na anatekeleza kwa ari, nguvu na kasi kubwa. Amefanya uamuzi
sahihi kabisa kwa kutoa msukumo maalum kwa upande wa kuimarisha ukusanyaji wa mapato
ya Serikali kwani bila ya kufanya hivyo utekelezaji wa Ilani utakuwa mashakani.
Wajibu wetu katika Chama ni kuwaunga mkono na kuwasaidia ili wafanye kazi yao
vizuri, kwa moyo na ufanisi. Nawaomba Watanzania wenzangu tuwe na moyo wa subira
na kumpa nafasi Rais wetu kutekeleza malengo aliyojiwekea kwa manufaa ya nchi
yetu na watu wake.
Hitimisho
Ndugu Mwenyekiti Mtarajiwa,
Hiyo kwa muhtasari ndiyo hali ya uhai wa Chama wakati ninapomaliza
ngwe yangu ya uongozi na kukabidhi kijiti kwako. Tulipanga kufanya mengi na tumefanikiwa mengi
ingawaje bado yapo mambo hatukuweza kuyafanya.
Kimsingi, kazi ya ujenzi wa
Chama au nchi haifanani na kazi ya ujenzi wa nyumba au daraja ambayo ina mwanzo
na ukomo. Kazi hii haiishi. Hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa Rais na Mwenyekiti wetu
wa kwanza, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na ndivyo ilivyokuwa kwa Rais
na Mwenyekiti wa Pili Ali Hassan Mwinyi.
Hali ilikuwa hivyo kwa Rais na
Mwenyekiti wa Tatu Benjamin Mkapa aliponiachia. Na ndivyo ilivyokuwa kwangu
nilipomwachia Mhe Dkt. John Pombe Magufuli, Urais na sasa ninapomuachia
Uenyekiti wa CCM. Na ndivyo itakavyokuwa kwako Mheshimiwa Rais utafanya yako na
hutayamaliza yatakayobakia atamwachia
Rais na Mwenyekiti atakayemfuatia, mwaka 2025.
Jambo linalonipa faraja kama
ilivyokuwa kwa viongozi walionitangulia ni kuwa name nimepata fursa ya kutoa mchango
wangu kwa ujenzi wa Chama chetu na maendeleo ya nchi yetu na watu wake. Naamini
historia itahukumu kwa usahihi kuhusu utumishi wangu kwa nchi yetu na Chama
chetu.
Mheshimiwa Rais na Mwenyekiti Mtarajiwa,
Nimezungumzia wewe kumkabidhi mrithi wako mwaka 2025 kwa sababu
naamini utapata kipindi cha pili. Maneno ya magazeti ati CCM mwisho wake 2020
yasikusumbue. Hilo halitatokea. Walinitabiria CCM kufia mikononi mwangu.
Haikutokea na CCM imeendelea kushinda sana na itaendelea kushinda 2020 na 2025.
Tumuunge Mkono Mwenyekiti
Mpya Dkt. Magufuli
Ndugu Wajumbe,
Baada ya maelezo yangu
marefu ya utangulizi na ya kuagana, naomba sasa nizungumzie madhumuni makuu ya
mkutano wetu huu. Agenda yetu ni moja tu: kuchagua Mwenyekiti Mpya wa kuchukua
nafasi yangu. Sisi katika Halmashauri Kuu ya Taifa tumempendekeza Mheshimiwa
Dkt. John Pombe Joseph Magufuli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ashike nafasi
hiyo.
Wapo wenzetu wawili ambao watakuja kuzungumza kwa niaba yetu kuwashawishi
Wajumbe mkubaliane nasi. Nitawaita watu hao wakati wake ukifika, kwa sasa napenda
kuchukua fursa fupi nami kusema kidogo.
Nina imani isiyokuwa na
hata chembe ya shaka kwamba Mheshimiwa John Pombe Joseph Magufuli kazi hii
anaimudu na ataifanya vizuri sana. Mapenzi yake na uaminifu wake kwa CCM hauna
shaka.
Anaipenda CCM kwa dhati ya moyo wake. Ameitumikia CCM na Serikali zake
kwa moyo na uadilifu mkubwa. Anao uzoefu wa kutosha wa uongozi katika Chama.
Amekuwa Mbunge na Waziri kwa miaka 20 yaani kumi katika Awamu ya Tatu na kumi
katika Awamu ya Nne.
Kama Mbunge amekuwa Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Wilaya, Halmashauri Kuu ya
Wilaya , Mkutano Mkuu wa Wilaya, Halmashauri Kuu ya Mkoa na Mkutano Mkuu wa
Mkoa na Mkutano Mkuu wa Taifa kwa miaka yote hiyo ishirini (20).
Amekuwa Mjumbe
wa Kamati ya Wabunge wa CCM kwa miaka 20. Hoja ya yeye kutokukijua Chama haina
msingi wala mashiko. Ni kweli hajafanya kazi ya ukada kama nilivyokuwa mimi.
Lakini hata Mzee Mwinyi na Mzee Mkapa hawakuwa Makada wa Chama lakini walikuwa
Marais wazuri wa nchi yetu na Wenyeviti wazuri wa CCM.
Ndugu Wajumbe,
Mimi naamini Dr. John
Magufuli atakuwa Mwenyekiti nzuri tu wa CCM. Baada ya miezi minane ya kuishikilia
Serikali, ni wakati muafaka wa kuunganisha kofia hizi mbili kama ulivyo utamaduni,
mila na desturi yetu nzuri.
Nawaomba nyote mumuunge mkono kwa kumpa kura zote
za Ndiyo na isipotee hata moja ya Hapana. Nawaomba pia kwamba baada ya
kuchaguliwa mumpe ushirikiano zaidi ya ule mlionipa mimi katika kutekeleza
majukumu yake ya kuongoza Chama chetu.
Naondoka nikiwa naamini bila ya shaka
yoyote kabisa kwamba chini ya uongozi wa Dr. John Pombe Joseph Chama cha
Mapinduzi kiko katika mikono salama na kitapata maendeleo makubwa na haraka.
Mwisho
Ndugu Wajumbe,
Mwanzoni mwa hotuba yangu
nilitoa shukrani kwa watu kadhaa lakini sikuwamaliza wote. Nimeacha salamu
mahsusi mwishoni kwa familia yangu. Namshukuru kwa namna ya pekee mke wangu mpenzi
Bi. Salma. Amekuwa nguzo imara katika familia na maisha yangu ya utumishi wa
umma. Ana mchango mkubwa katika mafanikio yangu. Ndiyo chemchem yangu ya utulivu
na ustahamilivu.
Shukrani zangu pia nazitoa
kwa wanangu na wajukuu zangu kwa kunivumilia pale walipomkosa baba yao na babu
yao. Nawapa pole na kuwataka radhi wanangu na familia yangu kwani wakati
mwingine baadhi yao wamekuwa wahanga (collateral damage) kwenye mambo
yasiyowahusu kwasababu ya maisha yangu ya siasa.
Nirudie tena kuwashukuru
wana-CCM wenzangu kwa heshima kubwa mliyonipa ya kuwa kiongozi wa juu kabisa wa
Chama chetu. Naondoka nikiwa mtu mwenye furaha tele kwamba Chama cha Mapinduzi
kiko salama na kinaendelea kuwa madarakani. Naipenda sana CCM na nitaendelea
kuipenda. Nawapenda sana viongozi na wanachama wenzangu wa CCM na nitaendelea
kuwapenda hadi siku Mungu atakaponiita mbele ya haki.
Mungu Ibariki CCM
Mungu Ibariki Tanzania
Kidumu Chama Cha Mapinduzi
No comments:
Post a Comment