Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
WAKALA
wa Majengo Tanzania (TBA) umesema tayari umekusanya Sh bilioni 2.6 ikiwa ni
zaidi ya asilimia 40 ya madeni waliyokuwa wakiwadai watumishi wa umma na watu
binafsi waliouziwa na kupanga nyumba za serikali kwa makazi na biashara.
Akizungumza na waandishi wa
habari jana wakati wafanyakazi wa TBA wakifanya usafi katika maeneo mbalimbali
ya Jiji la Dar es Salaam zilizopo nyumba hizo katika kilele cha Wiki ya
Utumishi wa Umma, Mkurugenzi Mkuu wa TBA, Elius Mwakalinga alisema kabla ya
kulipwa kwa fedha hizo, wakala huo ulikuwa ukidai zaidi ya Sh bilioni sita
ambapo baada ya kutolewa kwa notisi ya kulipa tayari wamekusanya Sh bilioni
2.6.
Mwakalinga alisema shughuli
ya kuwatoa wapangaji wengine inaendelea katika mikoa mbalimbali, na mkoani
Dodoma wamewaondoa wapangaji katika nyumba 27 huku Mwanza shughuli hiyo
ikikwama baada ya kuibuka fujo kati ya mpangaji na mfanyakazi wa Kampuni ya
Udalali ya Yono ambao ni wasimamizi katika shughuli hiyo.
“Kazi yetu sisi sio kuleta
vita tunataka fedha irudi ili tuendelee na ujenzi wa nyumba nyingine,
tumesikitishwa na kitendo cha mpangaji wetu Mwanza ambaye aliamua kuleta fujo
na kumshambulia mfanyakazi wa Kampuni ya Udalali wa Yono wakati akiondolewa
tunaomba tu wawe wastaarabu wanapotakiwa kuondoka au wakubali kulipa,” alisema
Mwakalinga.
Alisema ili kuondoa tatizo
la ucheleweshwaji wa ulipaji kodi katika nyumba hizo kuanzia Julai wapangaji
binafsi wataanza kulipa kodi kwa miezi sita huku watumishi wa umma wakiendelea
kulipa kwa miezi mitatu mitatu.
No comments:
Post a Comment