KIONGOZI wa upinzani wa
Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC), Moise Katumbi, amehukumiwa kifungo cha
miaka mitatu jela na Mahakama Kuu ya nchi hiyo kutokana na mzozo wa rasilimali,
ardhi na majengo.
Mahakama imedai kuwa Katumbi alimuuzia
mtu nyumba ambayo si yake.
Kiongozi wa muungano wa vyama 15 vinavyomuunga mkono Katumbi
vijulikanavyo kama G7, Kyungu Wa Kumwanza, alisema tukio hilo limepanga
kudidimiza demokrasia nchini humo.
Tukio hilo limekuja katika wakati ambao Katumbi,
anatarajia kugombea urais kwenye uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika mwezi
Novemba, Alhamisi iliyopita alifunguliwa mashtaka ya kuhatarisha usalama wa
Taifa.
Kwenye taarifa iliyotolewa na Mahakama Kuu
ya DRC Katumbi alishutumiwa kwa kutishia usalama wa taifa wa ndani na nje ya
nchi, na alikabiliwa na waranti ya muda wa kukamatwa, Mwendesha Mashitaka wa
Serikali alisema.
Katumbi ni milionea anayemiliki timu
maarufu ya soka ya TP Mazembe ya mjini Lubumbashi na Gavana wa zamani wa jimbo
lenye utajiri mkubwa wa madini la Katanga.
Adhabu ya mashitaka ya kutishia usalama wa
taifa ni kifo, hata hivyo ilibadilishwa na kuwa kifungo cha maisha jela, tangu
Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo ilipoondoa adhabu hiyo.
Kifungo cha Katumbi kinakuja wakati ambapo
kuna ongezeko la wasiwasi kutoka ndani na nje ya nchi hiyo kwamba Rais aliye
madarakani, Joseph Kabila atachelewesha uchaguzi huo uliopangwa kufanyika
mwishoni mwa mwaka huu, wakati muhula wake wa miaka mitano utakuwa unakamilika.
Katumbi mwenye umri wa miaka 51, amekuwa
hasimu namba moja wa Kabila katika kinyang'anyiro hicho cha urais, baada tu ya
kutangaza nia yake ya kugombea nafasi hiyo dhidi ya kiongozi huyo wa nchi
aliyehudumu kwa muda mrefu.
Mnamo
Mei 4, mwaka huu baada ya Katumbi kutangaza kuwania nafasi ya urais,
mamlaka za kimahakama zilimfungulia madai ya kuwaajiri mamluki wa kigeni.
Katumbi aliwahi kuwa swahiba wa Kabila
kisiasa
Katumbi alisema madai hayo, yaliyofuatiwa
na kukamatwa kwa walinzi wake binafsi, ambao ni pamoja na raia wa Marekani
ilikuwa ni hatua iliyoshinikizwa kisiasa.
Alipotakiwa kuzungumzia matamshi hayo ya
Katumbi, Msemaji wa serikali Lambert Mende aliliambia Shirika la Habari la AFP
kwamba, "anaweza kukutwa na kifungo cha nyumbani ama jela".
Wafuasi wa Kabila wanataka Uchaguzi Mkuu wa
urais usogezwe mbele kwa miaka miwili kutokana na madai ya hali ngumu ya fedha
na matatizo ya maandalizi.
No comments:
Post a Comment