Na Mwandishi Wetu, Mwanza
MTU
mmoja ameuawa na kundi la watu waliojichukulia sheria mkononi kwa kosa la wizi
wa kuku watano wilayani kwimba.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi amesema Agosti 21, mwaka huu saa tatu
kasoro robo asubuhi katika kitongoji cha Busulwa, Kata ya Ngulla Wilaya ya
Kwimba, Leonard Mathias (23), mkazi wa Kijiji cha Ngulla, aliuawa na kundi la
watu waliojichukulia sheria mkononi.
Kamanda
Msangi amesema watu hao walimpiga kwa fimbo na mawe sehemu mbalimbali za mwili
wake kisha kumchoma moto hadi kupoteza maisha kwa kosa la wizi wa kuku watano
mali ya Ester Robert ambaye ni mkazi wa kijiji hicho cha Ngulla.
“Inasemekana kuwa mtu huyo
aliiba kuku watano nyumbani kwa Ester Robert kisha akakimbilia kijiji cha
jirani cha Mwabomba. Inadaiwa kuwa wananchi wa kijiji cha Mwabomba walipomuona
akiwa na kuku hao walipata mashaka kisha walimkamata na baadaye walitoa taarifa
Kijiji cha Ngulla ndipo mwenye kuku alifika na kukabidhiwa kuku wake.
“Inadaiwa
kuwa baada ya marehemu kukabidhi kuku kwa mwenye mali, wananchi walimchukua na
kwenda naye kituo cha polisi, lakini wakiwa njiani walianza kumshambulia kwa
kumpiga fimbo na mawe sehemu mbalimbali za mwili wake na baadaye kumchoma moto.
Polisi walipata taarifa kutoka kwa raia wema ndipo walifanya ufuatiliaji wa
haraka hadi eneo na tukio na kufanikiwa kukamata watu saba ambao wanadaiwa
kuhusika kwa namna moja au nyingine katika mauaji hayo,” ameeleza kamanda huyo.
Aidha,
Kamanda Msangi amesema kwa sasa polisi wapo katika upelelezi na wanawahoji
watuhumiwa saba waliokamatwa kwa kutuhumiwa kuhusika kwenye tukio hilo.
No comments:
Post a Comment