Na Eddy Blog, Singida
UJENZI
wa Makao Makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Singida, uko njia panda
baada ya Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mathew Mtigumwe kutengua uamuzi wa
Baraza la Madiwani kuhusu ujenzi huo.
Katika
kikao cha mwisho cha Oktoba 28 mwaka huu, madiwani walikubaliana kuwa
makao makuu mapya ya halmashauri hiyo yajengwe katika kijiji cha
Kinyamwambo, kata ya Merya, tarafa ya Ilongero kutokana na eneo hilo
kuwa katikati ya halmashauri hiyo kijiografia.
Hata
hivyo, Novemba 24 mwaka huu, mkuu wa mkoa huo, alienda katika mji mdogo
wa Ilongero na kuitisha mkutano maalumu wa hadhara ambapo alibatilisha
uamuzi wa Baraza la Madiwani na kuwahakikishia wananchi wa eneo hilo
kuwa, makao makuu mapya yatajengwa hapo Ilongero na si mahali pengine.
Kutokana
na matamshi ya Mkuu wa Mkoa, Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Elia
Digha, alisema kuwa kauli hiyo ya kutengua uamuzi wa kikao halali cha
madiwani ni dharau ya hali ya juu na inalenga kukwamisha ujenzi wa makao
mapya ya halmashauri hiyo.
Mwenyekiti
huyo ambaye pia ni Diwani wa Msange, alisema kutengua uamuzi halali wa
madiwani ni kinyume na Kanuni ya Kudumu ya 3 (3) ya mwaka 2013 ya
Halmashauri za Wilaya.
“Inaelekea
kuna kitu nyuma ya pazia. Iweje mkuu mkoa aende kwenye mkutano huo
muhimu bila kuambatana na mwakilishi yeyote kutoka ofisi ya Mkurugenzi
Mtendaji wa Halmashauri ya Singida?” Alihoji mwenyekiti huyo.
Akizungumza
kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Ilongero hivi karibuni, Mkuu wa
Mkoa aliagiza uongozi wa halmashauri ya Singida kuhamia Ilongero ndani
ya miezi sita .
No comments:
Post a Comment