Na Haji Nassor, Pemba
KATIBU Mkuu Wizara ya Ujenzi,
Mawasiliano, Uchukuzi na Usafirishaji Zanzibar, Mustafa Aboud Jumbe amesema,
kila mwananchi anaepaswa kufidiwa kwenye ujenzi wa barabara ya Ole –Kengeja
apewa haki yake, ili ujenzi ukianza kusiwe na manun’guniko.
Alisema
hataki kuona ujenzi umeanza na kuna baadhi ya wananchi wakiilalamikia wizara,
kwa kutolipwa fidia kwa kuathiriwa na ujenzi huo, ambao utakuwa wa kiwango cha
lami.
Katibu Mkuu
huyo alieleza hayo, alipokuwa akizugumza na Meneja wa mradi na Mhandisi wa
ujenzi, kwenye barabara hiyo, eneo la Ole Kiyanga wilaya ya Chakechake, ikiwa
ni sehemu ya ziara ya siku mbili, alioambatana na waziri wa ziara hiyo.
Jumbe
alisema, hataki kuona wala kusikia wakati fedha zikiwa tayari kwa ajili ya ujenzi
wa barabara hiyo, na kisha kukajitokeza mwananchi ambae hajafidiwa nyumba yake.
Alisema kuwa,
anakumbuka sana ujenzi wa barabara ya Amani- Mtoni Unguja, ambao uliwahi kusita
kutokana na sababu ya mwananchi mmoja, kudai haki yake ya fidia, hivyo anahofia
na kwenye barabara hiyo, kusijejitokeza kama hilo.
“Mimi
niwaombe Meneja na Mhandisi mjipange vyema na muhakikishe kila kitu kimekaa
sawa, ili mkianza ujenzi hakuna kusita sita na hasa kwa sababu ya kutolipwa
fidia waathirika wa ujenzi’’,alifafanua.
Meneja wa Mradi
wa ujenzi wa barabara hiyo Amina Mohamed Habibu alisema, zipo nyumba 65 ambazo
zinapaswa kulipwa fidia, na tayari 13 katia ya hizo, wahusika
wameshakamilishiwa hazki zao za fidia na 52 zilizobakiwa wanaandaa.
“Ni kweli
wananchi 13 wameshapata haki yao, na waliobakiwa wasiwe na wasiwasi watapewa,
maana fedha zipo ila taratibu ndio hazijakaa sawa sana’’,alifafanua.
Mapema
waziri wa wizara hiyo inayoshughulikia ujenzi, Balozi: Ali Abeid Karume,
alisisitiza mara tu taratibu zitakapokamilika, ujenzi huo uende kwa haraka, ili
kuepuka vifaa kupanda bei.
Alieleza
kuwa, vifaa vinaweza kupanda bei mara maoja na kusababisha gharama iliopangwa
kupanguka, hivyo ni vyema uharaka wa kujenga uwepo.
“Mimi nashukuru
kwa hatua mliofikia, na hasa nimeridhika kusikia fedha zipo, sasa lazima mkaze
mkono mkijenga, maana vifaa kupanda bei ni mara moja’’,alifafanua Waziri.
Mapema Mhandisi
ujenzi wa barabara hiyo inayojengwa kwa ufadhili wa mfuko wa Opec, Amini Khalid,
alisema barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 35 ilianza kutajwa ujenzi wake
tokea mwaka 2007.
Alisema
inasimamiwa na mzalendo na wanatarajia baada ya kukamilika utiaji lami, itakuwa
na upana wa mita7.5, na kuwaomba wananchi washirikiane ili wakamilishe kazi
hiyo kwa wakati.
Wakati huo
huo waziri huyo na ujumbe wake ulishuhudia uchakavu na uchafu uliopo kwenye nyumba
za maendeleo ya Mtemani Wete, ambapo wizara inafikiria kuzifanyia matengenezo.
Kwa upande
wake Mdhamini wa shirika la nyumba Pemba, Suleiman Hamad Omar, amemueleza
waziri huyo kuwa, kumekuwa na hujuma za makusudi zinazofanywa na baadhi ya
wanachi, wanaoishi kwenye nyumba hizo.
“Kuna taka taka
zimetiwa kwenye eneo lenye miundombinu ya umeme na maji, yalioko chini ya
nyumba hiyo, hali ambayo pia inasababisha kukaribisha maradhi ya
miripuko’’,alifafanua.
Ujumbe huo
wa wizara ya Ujenzi, Mawasiliano, Uchukuzi na Usafirishaji ukiongozwa na waziri
wake na katibu mkuu ulitembelea pia barabara ya Mtambwe, Finya, Pandani,
Mgagadu –Kiwani, Ole- Kengeja, bandari za Mkoani na Wete.
No comments:
Post a Comment