WAZIRI
Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa, Kassim Majaliwa
amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi kufuatilia maendeleo ya
mradi wa umwagiliaji wa Narunyu katika kata ya Kiwalala wilayani Lindi.
Hatua
hiyo imekuja baada ya wananchi wa kata hiyo kusimamisha msafara wa
Waziri Mkuu, Majaliwa katika eneo la Kiwalala jana na kumuomba awasaidie
kuhusu hatma ya mradi wao wa umwagiliaji ambao walitakiwa wakabidhiwe
tangu mwaka 2014.
Awali
muwakilishi wa wananchi hao, Mohammed Bakar alisema kuwa mradi huo
uliogarimu shilingi milioni 600 ulitakiwa uwe tayari umekabidhiwa kwa
wananchi, lakini hadi sasa bado na hata banio halijakamilika, hivyo
wanashindwa kuendelea na kilimo katika eneo hilo.
“Mheshimiwa
Waziri Mkuu mradi huu bado haujaanza ila tulishangaa wakati wa mbio za
mwenge mwaka 2014 ilisomwa taarifa kwamba wakazi wa Kiwalala wananufaika
na mradi wa kilimo cha umwagiliaji wa Narunyu jambo ambalo si kweli
kwani mradi huu haujawahi kufanya kazi na hata banio hakuna,” amesema.
Waziri
Mkuu, Majaliwa amesema malalamiko hayo ya wananchi wa Kiwalala lazima
yafanyiwe kazi, hivyo amemuagiza mkuu wa mkoa wa Lindi, Zambi
kuhakikisha anakwenda kwenye kata hiyo kulipatia ufumbuzi suala hilo.
“Kweli
kuna miradi ambayo inaelekezwa na watu kwa viongozi kuwa imekamilika
wakati bado, namuagiza mkuu wa mkoa kulifanyia kazi jambo hili,”
amesema.
Pia
amesisitiza kwamba serikali hii si ya kuleana, mtu atakayebainika
kukwamisha miradi ya maendeleo watamalizana naye hapo hapo, hivyo
aliwaomba wananchi kuwa na subira kwani taarifa yao imepokelewa na
inafanyiwa kazi.
Kwa
upande wake mkuu wa mkoa huo, Zambi amesema tayari ameshapata taarifa
za tatizo la mradi huo na kwamba atafanya ziara kwenye eneo hilo na mtu
atakayebainika kutafuna fedha za mradi huo atamuwajibisha hapo hapo kwa
sababu yeye hataki kutumbuliwa.
Imetolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu
No comments:
Post a Comment