ALIYEKUWA Mgombea urais wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, amewataka wananchi
kulinganisha ahadi za Rais, Dk. John Magufuli na CCM kuhusu elimu.
Ameyasema hayo siku mbili baada ya Dk.
Magufuli, aagize watendaji wa serikali kushughulikia utekelezaji wa
sera yake ya kutoa elimu bure kuanzia Januari mwakani.
Lowassa, chini ya mwamvuli wa Umoja wa
Katiba ya Wananchi (Ukawa), aliahidi kutoa elimu bure kuanzia shule ya
awali hadi chuo kikuu.
Pia alikuwa ameahidi kufuta michango yote wanayotozwa wanafunzi, kama angepata ushindi wa kuwa rais.
Dk. Magufuli ambaye alikuwa akipeperusha bendera ya CCM, aliahidi kutoa elimu bure hadi kidato cha nne.
Taarifa iliyotolewa jana na ofisi
binafsi ya Lowassa, ilisema ahadi ya elimu bure aliyokuwa akiinadi,
ilikuwa iwaguse hata wanafunzi ambao tayari wako shuleni na siyo
wanaotarajiwa kuanza mwakani pekee.
“Niliahidi watoto wote walioko na
watakaoanza shule kuanzia kindergarten (shule ya awali) hadi chuo Kikuu
serikali yetu ingegharimia.
“Na nilitangaza kufuta michango yote shuleni kumpunguzia mzigo mwananchi,” taarifa hiyo ilimnukuu Lowassa akisema.
Taarifa hiyo ilisema ahadi ya Dk.
Magufuli, “ni kwamba kuanzia Januari hakuna mtoto atakayelipa ada
lakini hajatamka mustakhabali wa wanafuzi walioko shuleni kama wataguswa
na hatua hiyo au laa.”
Kuhusu mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya
juu, taarifa hiyo ilisema, Chadema kupitia Lowassa kilikwisha kuahidi
kuwa elimu ingekuwa bure hadi chuo kikuu.
“Vijana hawa wanahangaika na mikopo nasikia ni asilimia 17 tu kati ya wanafunzi 70,000 ndiyo waliopata mikopo.
CHANZO: Mtanzania
No comments:
Post a Comment