RAIS Dk John Magufuli amewataka
Watanzania wa dini zote na viongozi wa dini kutoka madhehebu mbalimbali,
kuendelea kumuombea ili atekeleze ahadi alizozitoa pamoja na kuinua
maisha ya Watanzania.
Dk Magufuli aliyasema hayo kwenye Ibada
ya Mavuno iliyofanyika katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Petro
lililopo Oysterbay jijini Dar es Salaam jana. Aliwashukuru pia wananchi
wote waliomuombea na kufanikisha kuchaguliwa kuwa Rais wa Tanzania wa
Serikali ya Awamu ya Tano.
Katika siku ya nne akiwa ofisini na
Jumapili yake ya kwanza tangu alivyoapishwa kuwa Rais wa Tanzania,
aliwasili kanisani hapo saa 12.50 asubuhi akiambatana na mkewe, Janet.
“Natoa shukurani kwa Watanzania wote wenye imani za kidini tofauti kwa
sala zao.
Nawaomba waendelee kuniombea ili niweze
kutekeleza ahadi nilizotoa, lakini pia niinue maisha ya Watanzania,”
alisema Dk Magufuli alipopewa nafasi ya kuzungumza. Alisema anaamini
kuwa ana deni kubwa kwa Watanzania hivyo aliahidi kufanya kazi kwa bidii
na kuboresha utoaji wa huduma kama njia ya kutimiza wajibu wake kwao.
“Sala zenu ni muhimu sana, zitaniwezesha
kufikisha nchi yetu katika hatua nyingine bora zaidi,” alisisitiza.
Awali, wakati akimkaribisha kanisani hapo, Mwenyekiti wa Parokia ya
Mtakatifu Petro, Dk Adelhelm Meru, alisema kwa kawaida Watanzania na
Waafrika kwa ujumla wana utamaduni wa kutoa shukurani pale wanapopata
mafanikio.
“Huu ni utamaduni tuliorithi tangu
vizazi na vizazi ndio maana nakuomba leo mheshimiwa Rais, uje usalimie
katika mkutano huu,” alisema Dk Meru ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wizara
ya Maliasili na Utalii. Dk Magufuli ni mmoja wa waumini katika parokia
hiyo ya Mtakatifu Petro kama ilivyokuwa kwa Baba wa Taifa, Mwalimu
Julius Nyerere.
Ibada hiyo pia ilihudhuriwa na waumini
wengi ambao pia ni viongozi kama vile Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya
Uchaguzi (NEC), Jaji mstaafu Damian Lubuva, Jaji mstaafu Thomas Mihayo
na aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu.
Tangu aingie Ikulu Alhamisi iliyopita,
Dk Magufuli ameonesha kuwa ni Rais anayechapa kazi ambapo pamoja na
kufanya kampeni nchi nzima kwa muda wa miezi miwili, ameendelea
kuwajibika ofisini hapo bila kupumzika. Alhamisi iliyopita, alimuapisha
Mwanasheria Mkuu George Masaju aliyemteua muda mfupi tu baada ya
kuapishwa.
Lakini pia siku moja tu baada ya kuingia
Ikulu, Rais alifanya ziara ya kushtukiza katika Wizara ya Fedha ambako
aliagiza maofisa wa wizara hiyo kuhakikisha wanaongeza kasi ya
ukusanyaji mapato kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), hususani kwa
wafanyabiashara wakubwa bila kuogopa.
Katika siku yake ya tatu ofisini, Dk
Magufuli pia alikutana na Makatibu Wakuu, Manaibu Katibu Wakuu pamoja na
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Benno Ndulu na Kamishna
Mkuu wa TRA, Rished Bade.
Katika mkutano huo, aliagiza kuwa hakuna
ofisa yeyote wa Serikali atakayeruhusiwa kusafiri nje ya nchi na badala
yake, maofisa wote waelekeze nguvu zao katika maeneo mbalimbali nchini.
No comments:
Post a Comment