Matthew
Rycroft, Mwakilishi wa Kudumu wa Uingereza katika Umoja wa Mataifa na
Rais wa Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa, kwa mwezi Novemba,
akizungumza na waandishi wa habari hawapo pichani, mara baada ya
Baraza Kuu la Usalama kumaliza kikao chake kilichojadili hali ya
Burundi, kikao ambacho pia kilipitisha azimio ambalo pamoja na mambo
mengine linamuunga mkono Rais wa Uganda Yoweri Museven ambaye
aliteuliwa na Viongozi wenzie wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuwa
msimamizi na mwezeshaji wa majadiliano kati ya pande zinazopinga
nchini Burundi.
Na Mwandishi Maalum, New York
BARAZA Kuu
la Usalama la Umoja wa Mataifa limelaani vikali hali ya kuendelea
kwa matukio ya mauaji, utesaji na vitendo vingine vya vinavyokiuka haki
za binadamu nchini Burundi.
Pamoja
na kukemea hali hiyo, Baraza Kuu la Usalama limeeleza kusudio la
kuchukua hatua zaidi kwa nchi hiyo ya Burundi. Pamoja na kumwomba
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, katika kipindi cha siku kumi na tano
awasilishe mbele ya Baraza hilo taarifa kuhusu uwepo wa Umoja wa
Mataifa nchini Burundi katika siku za baadaye.
Jana
( Alhamisi) Baraza hilo lilikutana katika kikao chake cha 7557
ajenda ilikuwa ni Burundi ambapo, Baraza kwa kauli moja lilipitisha
Azimio namba 2248 (2015). Kupitia Azimio hilo, Baraza limetoa wito kwa
pande zote nchini Burundi kujiepusha na kukataa fujo ikiwa ni pamoja
na kujiepusha na vitendo vyovyote vinavyoweza kutishia Amani na
utulivu wa taifa hilo.
Vile
Vile Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa ambalo kwa mwezi huu wa
Novemba Rais wake ni Uingereza limekema vikali kauli za uchochezi
zinazotolewa na baadhi ya watu ndani na nje ya Burundi, kauli ambazo
kwa mujibu wa Baraza hilo zinalenga katika kushawishi chuki baina ya
makundi ya watu nchini humo.
Kufuatia
kauli hizo za uchochezi, Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa,
limeitaka Serikali ya Burundi kuheshimu, kulinda na kuhakikisha haki za
binadamu na misingi ya uhuru, kuheshimu utawala wa sheria pamoja na
uwajibikaji wa uwazi dhidi ya fujo na itoe ushirikiano kwa Ofisi ya
Kamisheni ya Haki za Binadamu.
Kupitia Azimio hilo Baraza Kuu pia limeitaka serikali ya Burundi
kuwawajibisha wale wote watakaopatikana na hatia ya ukiukwaji ya Sheria
ya Kimataifa ya haki za binadamu na unyanyasajji wa haki za binadamu.
Aidha
kupitia Azimio hilo, Baraza Kuu la Usalama limetoa wito kwa Serikali
ya Burundi kutoa ushirikiano katika majadiliano yanayoongozwa na
Jumuiya ya Afrika Mashariki na ambayo yameridhiwa na Umoja wa Afrika
na limetaka kuitishwa haraka majadiliano yatakayokuwa jumuishi
yakiwashirikisha wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya Burundi ili
kutafuta muafaka utakaokubaliwa na pande zote.
Baraza
Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa pia kupitia Azimio hilo limesema
linamuunga mkono kwa nguvu zote mwezeshaji wa majadiliano hayo ambaye
ni Rais Yower Museveni wa Uganda aliyeteuliwa na Viongozi wa Jumuiya
ya Afrika Mashariki.
Katika
kusaidia mchakato wa majadiliano hayo, Baraza Kuu la Usalama la Umoja
wa Mataifa limemkaribisha Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kupeleka
timu ya wataalam ambao kwa kushirikiana na Serikali, Umoja wa Afrika
na wadau wengine watabuni mbinu za kushughulikia matatizo ya kisiasa
na kiusalama.
No comments:
Post a Comment