Ni katika suala la uanzishaji viwanda ili kukuza uchumi.
WAZIRI
MKUU Mizengo Pinda (Pichani)amesema Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa
Afrika (SADC) haina kuweka mkakati utakaohakikisha kuwa nchi wanachama
zinakuwa na mpango mahsusi wa kuendeleza viwanda kama ambavyo
imekubaliwa kwenye kikao chao kilichomalizika leo.
Ametoa
kauli hiyo leo mchana (Jumanne, Agosti 18, 2015), wakati akizungumza na
waandishi wa Habari mara baada ya kumaliza mkutano wa 35 wa wakuu wa
nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika
jijini Gaborone, Botswana.
“Jumuiya
ya SADC kupitia sekretarieti yake itabidi iweke mkakati maamlu wa
kufuatilia kama nchi wananchama imeandaa mapango wa kuendeleza viwanda
kulingana na makubaliano yaliyofikiwa kwenye kikao cha leo,” alisema
Waziri Mkuu ambaye ameshiriki kikao hicho kwa niaba ya Rais Jakaya
Kikwete.
Alisema
yeye binafsi amefurahishwa na kupitishwa kwa azimio la uendelezaji wa
viwanda katika nchi za SADC kwani unaendana na juhudi za Serikali ya
Tanzania za kukuza uchumi kupitia uendelezaji wa viwanda vya usindikaji.
“Nimefurahi
kwa sababu azimio hili linaendana na mpango wetu wa kuendeleza viwanda
wa mwaka 2015/2016 hadi 2020/2021. Sisi tumelenga viwanda vya kusindika
mazao ya wakulima, wavuvi na wafugaji… kwa hiyo naamnini tutaenda vizuri
na mpango mzima wa Jumuiya hii,” alisema.
Kuhusu
madeni ya michango kutoka kwa nchi wanachama wa Jumuiya hiyo, Waziri
Mkuu alisema Tanzania iko kwenye hatua nzuri ya ulipaji michango hiyo.
“Jana nilipofika niliulizia suala hilo, nikaambiwa kwamba Tanzania
imekwishalipa kwa kiwango cha kuridhisha. Nilitoa wito wakamilishe
kulipa hiyo michango iliyobakia kwenye maeneo husika,” aliongeza.
Mapema,
Waziri Mkuu Pinda alisoma salamu maalumu mbele ya wakuu wa nchi na
washiriki wa mkutano huo zaidi ya 500, zikiwa ni salamu maalum za
kuwaaga zilizotolewa na Rais Jakaya Kikwete. Rais Kikwete anamaliza muda
wake mwishoni mwa mwaka huu na hatapata nafasi nyingine ya kushiriki
kikao cha wakuu wa nchi.
Kikao
kijacho kimepangwa kufanyika Agosti, 2016 nchini Lesotho ambapo Mfalme
Letsie Mswati wa III alitumia fursa hiyo kuwakaribisha wakuu wa nchi
wanachama kwenye mkutano huo.
Katika
hatua nyingine, wakuu wa nchi za Jumuiya ya SADC wamechangua Rais Ian
Khama Seretse Khama kuwa mwenyekiti mpya wa Jumuiya hiyo.
Katika
kikao hicho waliazimia kuendeleza mapambano dhidi ya magonjwa ya Kifua
Kikuu, Malaria na kuazimia kupunguza maambukizi ya virusi vya UKIMWI
kwenye nchi wanachama.
Mbali
na kusisitiza utunzaji na uhifadhi wa mazingira, waliazimia pia kila
nchi itekeleze mpango wake wa kilimo ili kuwa na akiba ya kutosha hasa
ikizingatiwa hali ya ukame ambayo imezikumba nchi za kusini mwa jangwa
la Sahara na kuashiria uhaba mkubwa wa chakula.
Waziri Mkuu anatarajiwa kurejea nchini leo jioni.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMANNE, AGOSTI 18, 2015.
No comments:
Post a Comment