Baadhi ya watumiaji wa dawa za kulevya wakihudhuria moja semina zinazoendeshwa nchini.
………………………………………………………………………………
Na Damas Makangale, Makangale Satellite Blog
“Kila mwaka idadi ya watumiaji wa
dawa za kulevya nchini hasa kwa vijana wenye umri mdogo kabisa kati ya
miaka 15 mpaka 25 inakadiliwa kufika 10,000 hadi 11,000 kila mwaka
nchini ni idadi kubwa na hali inatisha,’ anasema Afisa kutoka Kitengo
cha Kudhibiti dawa za kulevya nchini, Moza Makumbuli
Wiki iliyopita Kitengo cha
Kudhibiti Dawa za Kulevya Nchini ( Drug Control Commission) kiliandaa
semina ya siku moja kwa wadau mbalimbali kutoka kwenye vyombo vya
habari, magereza, Polisi, Mashirika yasiyo kuwa ya Kiserikali, Madaktari
na wizara ya afya na lengo la semina hiyo ilikuwa kuwapa wadau matokeo
ya utafiti ya watumiaji wa dawa za kulevya cocaine na heroin nchini.
Akizungumza na wanasemina hiyo,
Bi Makumbuli amesema kwamba utafiti huo ulifanyika katika mikoa 12 ya
Tanzania bara kwa kufanya mahojiano na watumiaji, waathirika, wananchi
wa kawaida, polisi na watu mbalimbali pamoja na watoa taarifa ikiwemo na
utafiti wa mahali husika.
Amesema kwamba utafiti huo
ulifanyika katika mikoa ya Mtwara, Dodoma, Morogoro, Pwani, Kilimanjaro,
Tanga, Arusha, Mwanza, Mbeya, Shinyanga, Geita na kigoma.
Lengo linguine la utafiti huo wa
kisayansi ni kuongeza uelewa wa athari za matumizi ya dawa za kulevya,
hatari ya watumiaji kupata maambukizi ya virusi vya ukimwi na tatizo la
wagonjwa wa akili nchini inayochangiwa na matumizi ya dawa za kulevya
nchini.
Bi Makumbuli aliongeza kwamba
matumizi ya dawa ya kulevya kwa njia ya kujidunga kwa sindano
imeongezeka maradufu Duniani na Kusini Mwa Jangwa La Sahara ambapo
takribani watu milioni 13 wanatumia dawa hizo za kulevya kati ya heroin
na cocaine duniani na kusini mwa jangwa la sahara takribani watu milioni
1.5 wapo kwenye matumizi ya dawa hizo.
Alifafanua kwamba tatizo la
madawa ya kulevya nchini halikupata nafasi ya kuhifadhi kitakwimu au
taarifa zake nyingi hazijapata nafasi ya kuwekwa vizuri kwenye
kumbukumbu (Well documented) kwa muda mrefu na ndiyo kikwazo kwa
serikali kuamua, kupanga na kuchangua mikakati madhubuti ya kupambana na
ongezeko hilo la uuzwaji na utumiaji wa madawa hayo ya kulevya nchini.
“kwenye utafiti wetu tumegundua
kwamba sehemu nyingi za pwani (Coast Region) na pembezoni mwa barabara
(Along the road corridor) zimeathirika sana kwa vijana wengi kujihusisha
na uuzwaji na utumiaji wa madawa hayo ya kulevya na wengi kazi zao ni
makodakta wa daladala, wapiga debe, wavuvi sehemu za pwani na wengine ni
vibaka na wanawake wanajihusisha na biashara ya ukahaba,” aliongeza.
Kwa upande wake, Mratibu wa
Programu ya kudhibiti dawa za kulevya kutoka kitengo hicho cha serikali,
Bw Joel Ndayongeje amesema kwamba mapambano dhidi ya dawa za kulevya
bado yana safari ndefu hapa Tanzania kutokana na kusongwa na vikwazo
lukuki vikiwamo vya sheria dhaifu, ukosefu wa sera ya Taifa ya udhibiti
na kuendekezwa kwa vitendo vya rushwa katika vyombo vya dola.
Bw Ndayongeje aliongeza kwamba
kwenye utafiti wao waligundua pia mikoa inayoongoza kwa matumizi makubwa
ya dawa za kulevya nchini ni 5,190, Tanga, 3,300 Mwanza, 2,700 Arusha,
1,539 Morogoro, 1,096 Dodoma, 820 Mbeya, 563 Kilimanjaro, 319
Shinyanga, 108 Geita, 100 Kigoma na watu 65 mtwara.
Amesema kwamba katika miaka ya
hivi karibuni matumizi ya dawa za kulevya kwa wanawake yameongezeka mara
ya mwisho ulifanyika na kupata matokeo ya asilimia 6% lakini utafiti wa
hivi karibuni kwa kushirikiana na Kitengo cha Kuzuia na Kupambana na
magonjwa cha wa marekani (US Centres for Disease and Prevention (CDC)
nchini idadi ya wanawake kwenye matumizi ya dawa za kulevya kwa sasa ni
asilimia 20%
Pamoja na mambo mengine Serikali
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliwahi kukiri kuwa tatizo la dawa za
kulevya hapa nchini ni kubwa, linalohitaji nguvu kubwa ya mataifa yote
duniani.
“Mapambano dhidi ya dawa za
kulevya hayatafanikishwa na nchi moja bali nchi zote duniani,” amesema
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, wakati akiliahirisha Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania mjini Dodoma, Septemba 6, mwaka jana.
Kutokana na ukubwa wa tatizo
hilo, Pinda anasema Serikali inafikiria kuanzisha mahakama maalumu ili
kuharakisha mashauri ya dawa za kulevya.
“Nina imani tukijipanga vizuri
inawezekana… tutafika mahala tufikirie mahakama maalumu ya dawa za
kulevya ambayo itakuwa na kazi moja tu ya kusimamia mashauri yanayohusu
dawa za kulevya,” anasema.
Kadhalika, Waziri wa Nchi, Ofisi
ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi,
anasema Serikali inaandaa mapendekezo ya kufuta Sheria ya Dawa za
Kulevya na kutungwa mpya itakayokidhi mahitaji ya kushughulikia ipasavyo
makosa ya dawa za kulevya.
Wakati Serikali ikitangaza
msimamo wake huo, meli iliyosajiliwa Tanzania (upande wa Zanzibar)
iliripotiwa kukamatwa nchini Italia ikiwa imesheheni tani 30 za dawa za
kulevya zenye thamani ya paundi milioni 50, sawa na Sh bilioni 123 za
Tanzania.
Kutokana na mazingira hayo, Tume
ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya nchini (DCC) kwa upande wake,
inaona pia kuna haja ya Serikali kutangaza dawa za kulevya kuwa adui
namba moja kama hatua mojawapo ya kuonesha ukubwa wa tatizo hilo hapa
nchini lakini watafanya hivyo endapo tu kutakuwa na ushahidi wa kitafiti
na kitakwimu ili kuweza kujenga hoja hiyo.
Heroin na madhara yake
Heroin ni aina ya dawa ya kulevya
ya unga inayopumbaza mfumo wa fahamu. Dawa hiyo inatokana na mmea
uitwao ‘opium poppy’. Imekuwa ikiingizwa hapa Tanzania ikitokea nchi za
Mashariki ya mbali.
Mitaani heroin huitwa majina mengi kama vile unga, brown shugar, ngoma, ubuyu, mondo, ponda, dume, farasi, n.k.
Cocaine na madhara yake
cocaine ni dawa ya kulevya
inayotengenezwa kutokana na mmea wa coca ambao hustawi zaidi katika nchi
za Amerika ya Kusini. Kitaalamu mmea huo hujulikana kwa jina la
erythroxylon coca.
Cocaine, kwa mujibu wa watafiti ,
huwa katika unga mweupe au katika hali ya mawe madogo madogo.
Inajulikana kwa majina mengi kama vile snow, star dust, keki, unga, big
c, bazooka, white sugar na unga mweupe.
Hapa Tanzania cocaine hupatikana kwa shida kwa sababu ya bei yake ni nadra sana kupatikana nchini.
Anataja madhara ya cocaine kuwa
ni kuathiri mfumo wa fahamu wa binadamu, kutokwa na damu puani, kuwa na
mafua makali yasiyopona, kukosa hamu ya chakula, kupanuka kwa mboni za
macho, mchafuko wa damu na kupata majipu, kuongezeka kwa mapigo ya moyo
na shinikizo la damu.
Madhara mengine ya cocaine ni mtu
kuchanganyikiwa, kukosa ufanisi kazini, kuwa na hisia za kuwapo kwa
vijidudu mwilini, magonjwa ya ini, kuharibika kwa mishipa ya fahamu,
kuharibika kwa moyo, figo na mapafu, kikohozi cha muda mrefu, kupasuka
kwa mishipa ya damu kichwani kunakoweza kusababisha kiharusi au kifo na
kumweka mtu katika hatari ya kuambukizwa virusi vya Ukimwi
No comments:
Post a Comment