BABA wa mwanamuziki mkongwe na
nguli nchini Tanzania, John Kitime aliyefariki Agosti Mosi, 2015 katika
Hospitali ya Taifa Muhimbili ya jijini Dar es Salaam amesafirishwa
kuelekea mkoani Iringa tayari kwa mazishi.
Marehemu Mzee Francis Raphael Kitime alisafirishwa jana baada ya kufanyika ibada ya kumuombea na kutoa heshima za mwisho kwa ndugu na jamaa wa familia ya marehemu waishio Dar es Salaam, ibada iliyofanyika katika Kanisa Katoliki Parokia ya uruma kwa wagonjwa lililopo ndani ya hospitali ya Muhimbili.
Akisoma historia fupi ya marehemu, mtoto wa marehemu John Kitime alisema Francis Kitime alizaliwa Juni 16, 1931 Tosamaganga, Iringa katika familia ya watoto watatu yaani Joseph, Isabela na Clementina. Alipata elimu yake ya msingi hadi chuo kati ya mwaka 1939 hadi 1950 katika Shule za Misheni na Vyuo vya Elimu Tosamaganga, Iringa na mnamo mwaka 1951 hadi 1963 alifundisha katika shule anuai mkoani hapo.
Kitime alisema mwaka 1964 marehemu alianza kufanya biashara ya kuuza mafuta (caltex) hadi 1970 ambapo alimiliki kituo hicho na kufanya biashara hiyo hadi mwaka 1979, mwaka 1980 aliacha biashara na kuajiriwa kwenye idara ya utawala katika Hospitali ya Ipamba hadi alipostaafu.
Marehemu pia amefanya kazi za kitume takribani miaka 20 kama Mwenyekiti wa Baraza la Walei na Mwenyekiti wa Lions Club katika Mkoa wa Iringa, na pia mtunzi na mwimbaji nyimbo mbalimbali hasa za lugha ya ki-Hehe. Marehemu kaacha watoto sita, wajukuu nane na vitukuu viwili.
No comments:
Post a Comment