![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEiI28lHa-XMg8mN-y2y7gvGUU51h3g6Ak-iXwTue9tSx5cibkdMQxe2RvmdJu9_iv2_Qg8LE85SJfLcagTDY2_xdXOiNjpGatDr_3Cjnv7cfwnHmfOmTfh9fTGSzYC40x2kyOXd8JDVb1mh/s1600/8.jpg)
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jakaya Kikwete amesema kitendo cha kutumia
matajiri kama vyanzo vya mapato,
kunadhalilisha chama hicho na
haiwezi kuendelea kuvumiliwa.
Alisema hayo jana wakati wa uzinduzi wa Kituo
cha Mikutano cha CCM mjini Dodoma.
Alionesha
kukerwa na uwajibikaji wa viongozi wa wilaya na mikoa wa chama hicho
katika kubuni mapato ya chama hicho hivyo kutumia matajiri kama vyanzo vya
mapato.
“Tunavyo
viwanja vingi sana lakini hatuvitumii kuvigeuza mtaji wa kupata kipato. Vipo
viwanja vingine viongozi wanagawana; wanajenga nyumba zao badala ya kujenga
miradi ya chama. Hili tunalisema tunarudia lakini viongozi wetu hawasikii wao
wanakimbilia kwa matajiri kuomba, tunajidhalilisha; lini tutazinduka,” alisema.
Katika uzinduzi huo uliohudhuriwa na viongozi
wa juu wa chama, Kikwete aliagiza viongozi wa chama hicho kubuni mikakati ya
kuhuisha rasilimali za chama hicho ili kukiongezea mapato.
Alisema kituo
kinazinduliwa katika wakati muafaka ambao vikao vya juu vya chama hicho
vinafanyika na kwamba kituo hicho kitaandika historia kwa wajumbe kukitumia ili
kupata uongozi mpya ndani ya chama hicho.
Miongoni mwa waliohudhuria hafla hiyo ya
uzinduzi ni pamoja na Makamu wa Rais, Dk
Mohamed Gharib- Bilal, Makamu Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Zanzibar, Dk Ali
Mohamed Shein, Katibu Mkuu Abdulrahman Kinana, Mwenyekiti wa Bodi ya Udhamini
ya CCM, Anna Abdallah na wajumbe wa Kamati Kuu (CC) ya chama hicho.
Alisema
ujenzi wa jengo hilo lililojengwa na Kampuni ya CRJE ya China kwa siku
212, umewafumbua macho wanaCCM kwani sasa watatambua kuwa inawezekana kutumia
rasilimali mfu za chama hicho katika kuingizia mapato.
Muonekano wa ukumbi huo mpya |
Alisema kwa miaka mingi CCM imekuwa katika
hali ngumu ya mapato huku ikiwa na rasilimali nyingi mfu. Alisema ni lazima sasa rasilimali hizo zikiwemo
utajiri mkubwa wa viwanja na maeneo, zigeuzwe kuwa hai na kukiongezea mapato
chama hicho.
Alisema alipohutubia Mkutano Mkuu mwaka 2012,
alieleza azma yake ya kuhakikisha chama kinajenga jengo jipya na la kisasai
kumaliza kero ya kutumia ukumbi wa kukodi wa Kizota.
Kwa mujibu wa Kikwete, ukumbi huo ni ghala
linalotumika kuhifadhia mahindi na hivyo
huondolewa ili mikutano ya CCM kufanyika, hatua ambayo hugharimu chama
kati ya Sh milioni 800 na Sh bilioni moja.
Alisema pamoja na kupitishwa kwa sera ya
kujitegemea, bado viongozi wa chama
hicho wanashindwa kutekeleza sera hiyo kwa vitendo; badala yake wanaendelea
kukumbatia rasilimali mfu za chama hicho bila kubuni namna ya kuzihuisha na
kuingiza fedha nyingi kwa chama.
Alisema ili kuhakikisha sera ya kujitegemea
inatekelezwa kikamilifu, kuna ulazima sasa kwa CCM kuajiri Mkaguzi atakayepita
kila wilaya na mkoa kuhakiki vitega uchumi vya chama hicho kwa kuvitembelea na
si kupewa taarifa ofisini.
No comments:
Post a Comment