UTAJUAJE KAMA UNA UPUNGUFU WA MAJI MWILINI?
Umeshawahi kwenda
hospitali kumlalamikia daktari kuwa mwili wako hauna nguvu na unajisikia
kuchokachoka sana na baada ya kukuchunguza, akakwambia huna tatizo
lolote isipokuwa una upungufu wa maji mwilini tu?
Mwili kuishiwa nguvu huwa
ni miongoni mwa dalili za upungufu wa maji mwilini na chanzo kikiwa ni
wewe mwenyewe kutopenda kunywa maji. Ni kawaida kwa baadhi ya watu
kutokunywa maji hadi pale wanaposikia kiu.
Katika makala ya leo,
nitakujuza dalili za mwili kuishiwa maji ambazo hujitokeza na kukuhimiza
kunywa maji hata kabla hujasikia kiu. Uonapo dalili hizo, hupaswi
kuzipuuzia bali kunywa maji kwa wingi tena haraka.
UPUNGUFU WA MAJI MWILINI NI NINI?
Pale mwili unapopoteza
kiasi kingi cha maji kwa njia mbalimbali, ikiwemo jasho na mkojo, mwili
hupungukiwa maji na hivyo mtu huyo huambiwa ana upungufu wa maji.
Tunaelezwa kuwa karibu theluthi mbili ya miili yetu imejaa maji.
Ili mwili uweze kufanya
kazi yake vizuri, kiwango cha maji mwilini hakipaswi kupungua hata
kidogo, hivyo kila mtu ana wajibu wa kunywa maji ya kutosha kila siku
ili kulinda kiwago chake cha maji kisipungue na kinapopungua ndipo hapo
mwili huanza kuonesha dalili za kukaukiwa maji (dehydration).
NINI HUSABABISHA?
Sababu zinazosabababisha mwili kukaukiwa maji huweza kuwa nyingi, lakini zinazojulikana zaidi ni pamoja na:
Kuacha kunywa maji
Kukaa kwenye joto kwa muda mrefu
Kunywa kiwango kikubwa cha pombe,
Ugonjwa wa kisukari ambao husababisha mtu kukojoa mara kwa mara
Kutokwa na jasho jingi,
kwa sababu ya ama kufanya kazi ngumu au mazoezi. Hivyo inashauriwa mtu
anayetokwa jasho jingi kunywa maji mara kwa mara wakati akiendelea na
shughuli inayomtoa jasho.
Kama ukiugua au ukipatwa na homa kali, huweza kupungukiwa na maji mwilini
Kutapika na kuharisha nako huweza kupoteza maji mwilini.
DALILI ZA KUKAUKIWA MAJI KWA WATOTO
Kwa kawaida, dalili za
upungufu wa maji mwilini hujitokeza zaidi kwa watoto wadogo kuliko watu
wazima au wazee. Dalili za upungufu wa maji mwilini kwa watoto huweza
kusabababishwa ama na kuharisha, kutapika, kutokunywa maji au vimiminika
vingine vya kutosha.
Mtoto mwenye dalili za upungufu wa maji huweza kuonesha dalili zifutazo:
Kukojoa mara chache sana
Mtoto kutokuwa mchangamfu
Macho, tumbo au mashavu kubonyea
Mdomo na ulimi kukauka
Mtoto kulia mara kwa mara na anapolia machozi hayatoki.
DALILI ZA UPUNGUFU WA MAJI KWA WAZEE
Dalili za upungufu wa
maji kwa wazee ni tofauti na watu wazima. Wazee wa umri zaidi ya miaka
60 huwa na ngozi iliyosinyaa na hata ukiiminya, hubaki katika hali hiyo
kwa muda na unapoikwaruza alama hubaki.
Halikadhalika, wazee hukosa haja ndogo kwa muda mrefu, hupungukiwa uzito kwa kiasi kikubwa na hupatwa na homa.
DALILI ZA UPUNGUFU WA MAJI KWA WAJA WAZITO
Upungufu wa maji mwilini
kwa waja wazito ni hatari kwa mama pamoja na mtoto. Dalili zinazoweza
kujitokeza kwa waja wazito ni pamoja na:
Kukojoa mkojo wa njano nyeusi
Kuumwa na kichwa
Mwili kukosa nguvu
Kichefuchefu na kutapika
Kukaukwa na mdomo
Ili kujiepusha na
matatizo ya upungufu wa maji na hatimaye kujikuta unakumbwa na dalili
kadhaa zilizoelezewa hapo, ambazo ziko pia kwa watu wazima wengine, ni
kuwa na mazoea ya kunywa maji ya kutosha kila siku. Hata utakapozidiwa
na kukimbizwa hospitali, hakuna dawa nyingine utakayopewa zaidi ya maji (re-hydrating solution). Kwa nini usubiri hali hiyo ikutokee wakati unaweza kuizuia kwa kunywa maji tu
SOURCE: MZIZI MKAVU BLOG
No comments:
Post a Comment