Friday, June 19, 2015

BILIONEA DANGOTE WA NIGERIA APANGA KUINUNUA ARSENAL



BILIONEA wa Nigeria Aliko Dangote amepanga kuinunua klabu ya Arsenal. Bilionea huyo anaamini jinsi alivyowekeza kwenye mafuta na majengo nchini mwake anaweza kuwa na fedha za kuinunua klabu hiyo ya England.


Dangote mwenye umri wa miaka 58 ambaye inakadiriwa kuwa na utajiri wa dola za Marekani bilioni 11.5 alisema amekuwa akiishabikia the Gunners tangu miaka ya 1980.

"Nitakapopata nafasi hiyo nitakuwa na vyanzo vya kutosha kuinunua,” alisema alipoulizwa na BBC.

Mmarekani Stan Kroenke ni miongoni mwa mwanahisa wa Arsenal akimiliki asilimia 66.64.

Mrusi Alisher Usmanov anamiliki asilimia 29.11 na nyingine 62,217  zikimilikiwa na watu mbalimbali wakiwemo wachezaji wa zamani na mashabiki wa Arsenal. Dangote anashika nafasi ya 67 katika orodha ya matajiri duniani.

Siku za nyuma alikuwa akitaka kununua asilimia 15.9 ya hisa kwa Kroenke kwa dola za Marekani milioni 123.

"Tulikuwa wengi tuliotaka kununua hisa, lakini watu waliokuwa wakifanya biashara walitangaza dau la kutuua,” aliongeza Dangote.

Dangote anaamini Arsenal inatakiwa kumilikiwa na watu tofauti tofauti ili ipate mafanikio makubwa uwanjani.


Aliongeza: "Wanafanya vizuri, lakini wanahitaji mkakati mwingine zaidi, wanahitaji mkakati wa kimwongozo kuliko ilivyo sasa ambapo wanaendeleza vipaji na kuuza”.

No comments:

Post a Comment