Friday, June 19, 2015

MH. LEMA ATAKA SIKU ZA UANDIKISHAJI BVR ZIONGEZWE



MBUNGE wa Arusha Mjini, Godbless Lema ameitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuongeza siku za kujiandikisha kwa Mkoa wa Arusha ili watu wengi waweze kupata nafasi.

Pia amewataka wasimamizi wa uandikishaji kwa njia ya Biometric Voter Registration (BVR) nao kuwa makini ili uandikishwaji huo ufanyike kwa kufuata taratibu.

Lema aliyasema hayo jana wakati akizungumza na Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Juma Idd pamoja na wenyeviti wa Serikali ya Mitaa.

Katika mazungumzo hayo pia kulikuwepo na madiwani wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambao walikwenda Ofisi ya Mkurugenzi huyo kulalamikia jinsi uandikishwaji unavyohujumiwa na baadhi ya watendaji wa kata, waandikishaji wa BVR pamoja na vifaa kuwa duni..........
 
Lema alisema uandikishaji huo umegubikwa na urasimu kwa baadhi ya watendaji wa kata kwani wanaandikisha wananchi kwa kuangalia kama ni wakazi wa eneo hilo au la.

Alisema katika maeneo ambayo yana umeme walikubaliana na Mkurugenzi Idd pamoja na watu wa NEC  uandikishaji wa BVR kuendelea  hadi saa 2:00 Usiku, lakini  wahusika hawafuati utaratibu huo.

Alisema  maeneo mengine yasiyo na umeme wananchi wanajitolea kukodisha jenereta ila waandikishaji wanafunga vituo saa 12:00 jioni na kuwaingiza wengine waliobaki katika daftari la Tume ili asubuhi yake waanze wao wengine wafuate.

Kwa upande wake, Idd alisema kutokana na tatizo la wingi wa watu ambao hawakutegemea kama watajitokeza kujiandikisha, NEC imeongeza mashine nyingine 10 za BVR kutoka jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuongeza kasi ya uandikishaji.

No comments:

Post a Comment