Na Ali Issa -Maelezo Zanzibar
Mkuu wa Mkoa Magharibi Ayoub Muhammed Mahmoud, amesema kazi iliyoko mbele kwa sasa ni kutekeleza maagizo yaliyotoolewa na Rais Dk. Ali Mohamed Shein wakati wa ziara yake katika mkoa huo.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Vuga, Mkuu huyo wa Mkoa amesema kuna mambo mengi ambayo Dk. Shein ameagiza yatekelezwe wakati akifanya tathmini ya ziara yake ya siku mbili mkoani humo.
Ameeleza kuwa wajibu wa kutekeleza maagizo hayo si jambo la hiyari na kwamba kila mtendaji katika ngazi zote anapaswa kufanya kazi aliyopangiwa kwa kasi ile ile anayoitaka Mhe. Rais.
“Ni lazima tuhakikishe tunakwenda kwa kasi inayotakiwa na kama kuna mtu asiyeweza kuendana na kasi hiyo ni bora akae pembeni,” amesisitiza Ayoub.
“Sasa ni wakati wa kazi tu na uzembe sasa mwiko, na watakaozembea hatutawafumbia macho wala kuwaonea muhali. Ninafanya hivi kwa kutekeleza agizo la Mhe. Rais ambao ni wajibu wangu kikazi,” ameweka bayana.
Aidha amesema miongoni mwa changamoto atakazozishughulikia ni msongamano wa magari katika maeneo ya Mji Mkongwe, uchangiaji damu kwa hiyari, kutokomeza malaria na kuwakamata watu wanaokaidi marufuku ya kuingiza wanyama maeneo ya mjini.
Kuhusu tatizo la idadi kubwa ya wanafunzi maskulini, alisema ujenzi wa madarasa uliozinduliwa hivi karibuni kupitia kampeni ya ‘Mimi na Wewe’ unatarajiwa kupunguza kwa kiasi kikubwa msongamano uliopo kwa sasa baada ya kukamilika ujenzi huo ambao pia unafanyika katika skuili nyengine ikiwemo Sharifu Msa.
Ameeleza kuwa, wingi wa wanafunzi katika darasa moja ambapo katika baadhi ya skuli hufikia 160, haukumfurahisha Mhe. Rais, ambapo alipongeza juhudi za ujenzi wa madarasa mapya unaofanyika kwa nguvu za wananchi chini ya uongozi wa mkoa huo.
Baadhi ya miradi iliyotembelewa na Dk. Shein katika ziara yake mkoani humo, ni ule wa kuhifadhi mazingira katika bahari ya Kilimani ambapo maji yamekuwa yakipanda hadi katika maeneo ya makaazi ya wananchi.
Aidha amefungua jengo la Chuo cha Utalii Maruhubi, ujenzi wa barabara ya Kinuni, nyumba za kisasa Fumba na Nyamanzi na mradi wa maji safi na salama Bumbwisudi na pia alifungua skuli ya Kihinani.
Dk. Shein pia ametembelea uwanja wa Mao Tse Tung unaofanywa na wataalamu kutoka Jamhuri ya Watu wa China.
Wakati huohuo, Mkuu wa Mkoa amepokea hundi ya shilingi 15,000,000 kutoka kampuni inayotoa huduma za kiufundi mijini na vijijini (Urban and Rural Engeneering Service Company) yenye ofisi zake Mikocheni jijini Dar es Salaam.
Fedha hizo zilizotolewa na Naibu Mkurugenzi wa kampuni hiyo Salum Mussa Omar, ni kwa ajili ya kusaidia upatikanaji wa madawati kwa skuli za msingi Mkoa wa Mjini Magharibi.
No comments:
Post a Comment