Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akionyeshwa pembe za faru John na Kaimu Mkurugenzi Msaidizi waKitengo
cha Kupambana na Ujangiri wa Wanyamapori(Acting Assistant Director of
Antipoarching, Wildlife Division), Bw. Robert Mande, katika kikao
klichofanyika kwenye Makazi yake jijini Dar es salaam Desemba 9, 2016.
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa
Kitengo cha Kupambana na Ujangiri wa Wanyamapori (Acting Assistant
Director of Antipoarching, Wildlife Division), Bw. Robert Mande (kulia)
na Mkuu wa Hifadhi ya Ikorongo Gurunetya Serengeti, Nollosco Ngowe
wakiwa wamebeba sanduku lenye pembe za faru John baada ya kumwonyesha
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa katika kikao kilichofanyika kwenye Makazi
ya Waziri Mkuu jijini Dar es salaam Desemba 9, 2016. (Picha na Ofisi ya
Waziri Mkuu)
……………..
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amepokea taarifa inayoelezea utaratibu
uliotumika kumhamisha faru John kutoka Hifadhi ya Ngorongoro kwenda
Sasakwa Black Rhino Sanctuary iliyoko kwenye Hifadhi ya Grumeti.
Akizungumza katika kikao kilichofanyika nyumbani kwake Oysterbay leo
mchana (Ijumaa, Desemba 9, 2016) na kuhudhuriwa na Waziri wa Maliasili
na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe na baadhi ya watendaji wa wizara yake,
Waziri Mkuu amesema taarifa hiyo itafanyiwa kazi na wataalamu wa ofisi
yake.
“Nilipokea taarifa yenu jana saa 7 usiku lakini nikaahidi kuwa leo
tukimaliza sherehe za maadhimisho ya Uhuru tukutane na kujadiliana
kuhusu taarifa yenu,” amesema.
Akisoma taarifa hiyo mbele ya Waziri Mkuu, Prof. Maghembe alisema
hadi kufikia Desemba 2015 wakati faru John anahamishwa alikuwa na watoto
26 (sawa na asilimia 70.2) ya faru wote waliokuwepo ndani ya kreta.
“Kati ya faru 37 waliokuwepo ndani ya kreta, watoto wake walikuwa 26
sawa na asilimia 70.2. Uamuzi wa kumuondoa John ulikuwa ni muhimu ili
kuwezesha kuongezeka kwa faru weusi na kupunguza tatizo la ‘inbreeding’
ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro,” alisema Waziri Maghembe.
Baada ya kuhamishiwa Sasakwa, Waziri Maghembe alisema Julai 10, 2016
afya ya faru John ilianza kudorora na alikufa tarehe 18 Agosti, mwaka
huu. Taarifa hiyo iliandaliwa na Kamati ya Taifa ya Kuwalinda Tembo na
Faru. Kamati hiyo inaundwa na Mkurugenzi Mkuu wa TAWIRI, Mkurugenzi Mkuu
wa TANAPA, Mkurugenzi Mkuu wa NCAA na Mhifadhi Mkuu wa Ngorongoro.
Akikabidhi pembe za faru huyo mbele ya Waziri Mkuu, Kaimu Mkurugenzi
Msaidizi wa Kitengo cha Kupambana na Ujangili wa Wanyamapori, Bw. Robert
Mande alimweleza kwamba pembe kubwa ya faru John ilikuwa na uzito wa
kilo 3.6 na pembe ndogo ilikuwa na uzito wa kilo 2.3.
Watendaji wa wizara waliohudhuria kikao hicho ni Kaimu Katibu Mkuu,
Bw. Iddi Mfunda; Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro
(NCAA), Bw. Freddy Manongi; Mkurugenzi Mkuu wa TAWIRI, Bw. Simon Mduma;
Kaimu Mkurugenzi Idara ya Wanyamapori, Bw. Alexander Songorwa na Mkuu wa
Pori la Akiba la Ikorongo/Grumeti, Bw. Nollasco Ngowe.
Desemba 6, mwaka huu, akiwa ziarani mkoani Arusha, Waziri Mkuu
aliuagiza uongozi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), umletee
nyaraka zote zilizotumika kumhamisha faru maarufu kwa jina la ‘John’
kutoka kwenye hifadhi hiyo ifikapo Alhamisi, Desemba 8.
Alitoa agizo hilo alipotembelea ofisi za makao makuu ya NCAA zilizoko
wilayani Ngorongoro, mkoani Arusha na kuzungumza na watumishi wa
mamlaka hiyo pamoja na Wajumbe wa Baraza la Wafugaji ikiwa ni sehemu ya
ziara yake ya kikazi mkoani humo.
No comments:
Post a Comment