Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Kigoma Bw. Daniel Machura akitoa
hotuba ya kufunga mafunzo ya
miradi ya maendeleo kwa ajili ya ufadhili wa washirika wa maendeleo kwa Mkoa wa
kigoma. Kulia ni mmoja wa wakufunzi wa mafunzo hayo, Dkt. Wilhelm Ngasamiaku
kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kushoto ni Mratibu wa mafunzo hayo
Bw. Paul Sangawe kutoka Tume ya Mipango.
Mratibu wa Mafunzo Bw. Paul Sangawe akitoa muhtasari wa kile
kilichojadiliwa katika mafunzo hayo yaliyodumu kwa muda wa siku tano. Katikati
ni Katibu Tawala Msaidizi Mkoa
wa Kigoma Bw. Daniel Machura na kulia ni mmoja wa wakufunzi wa mafunzo hayo, Dkt Wilhelm Ngasamiaku kutoka
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Mchumi kutoka Wizara ya Fedha na Mipango - Tume ya Mipango, Bw. Senya
Tuni akionesha kitabu cha Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano
(2016/17-2020/21) kwa washiriki (hawapo pichani) wakati akiwasilisha mada juu
ya Mpango huo.
Baadhi ya washiriki wakifanya mazoezi ya kanuni zinazotumika kuchagua
miradi sahihi kwa ajili ya kupata ufadhili kutoka kwa washirika wa maendeleo.
Mazoezi hayo yalifanyika mapema kabla ya kuhitimishwa kwa mafunzo hayo.
Na Adili Mhina, Kigoma.
Serikali imewaonya watumishi wasio waaminifu
katika kusimamia na kuratibu miradi inayotekelezwa kwa fedha za washirika wa
maendeleo kuepukana na vitendo vya rushwa na ubadhirifu kwani Serikali ya Awamu
ya Tano haina huruma wala msamaha kwa watu wa aina hiyo.
Onyo hilo limetolewa mwishoni mwa juma na Katibu
Tawala Msaidizi Mkoa wa Kigoma Bw. Daniel Machura wakati akifunga mafunzo ya
maandalizi ya miradi ya maendeleo kwa ajili ya ufadhili wa washirika wa
maendeleo kwa mkoa wa Kigoma yaliyofanyika mjini hapa na kuendeshwa
na Wizara ya Fedha na Mipango kupitia Tume ya Mipango kwa ufadhili wa
Serikali ya Ubelgiji.
Mafunzo hayo yalishirikisha Wakurugenzi wa Mamlaka
za Serikali za Mitaa, Makatibu tawala wa wilaya, Wakuu wa Idara za Mipango,
Wachumi, Maafisa Mipango na Watakwimu ambao wana majukumu ya usimamizi na
uratibu wa miradi katika sekretarieti ya Mkoa wa Kigoma na Halmashauri zake
zote.
Machura alieleza kuwa Serikali ya sasa haina
nafasi ya kuwalea watendaji ambao wanaweka maslahi yao mbele badala ya
kuangalia wananchi katika kutekeleza miradi inayofadhiliwa na washirika wa
maendeleo kitu kinachopelekea miradi mingi kutekelezwa chini ya kiwango bila
kuzingatia thamani ya fedha.
Alieleza kuwa baadhi ya watumishi walifikia
hatua ya kuandaa maandiko ya kuomba fedha za ufadhili wa miradi ya maendeleo ya
wananchi lakini fedha hizo zikipatikana walikuwa wanagawana na kuzitumia
katika shughuli zao binafsi badala ya kuzingatia malengo ya fedha hizo.
“Tulifika pabaya sana, watu walikuwa wanaandika
proposal (andiko) kwa wafadhili ili wapate fedha za kutekeleza miradi ya
wananchi lakini cha ajabu unakuta fedha zikipatikana wanagawana bila aibu kwa
kuwa zimetoka nje, katika serikali ya sasa watu wa aina hiyo hawana nafasi
kwenye utumishi wa umma,” alieleza Bw. Machura.
Alisisitiza kuwa viongozi wa mamlaka za serikali
za mitaa hawana budi kuzingatia mafunzo waliyopata kwa ajili ya kuongeza
ufanisi wa kusimamia miradi na kuleta maendeleo katika maeneo yao ya
utawala ili wafadhili waendelee kuamini kuwa fedha zote wanazotoa zinatekeleza
miradi iliyokusudiwa.
“Tukifanya hivyo Serikali ya Ubelgiji pamoja na
wadau wengine wa maendeleo watakuwa tayari kuongeza michango yao katika
kuusaidia mkoa wetu kujikomboa kutoka katika umaskini hususan kwa kuendelea
kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo”, alisistiza.
Kwa upande wake mratibu wa mafunzo hayo ambaye
pia ni Naibu Katibu Mtendaji anayesimamia Klasta ya Biashara za Kimataifa na
Mahusiano ya Uchumi Tume ya Mipango, Bw. Paul Sangawe alibainisha kuwa kuna
baadhi ya watendaji ambao hawatoi taarifa za matumizi ya fedha za miradi ya
ufadhili kwa wakati, kitu ambacho kinarudisha nyuma jitihada za washirika wa
maendeleo katika kufadhili miradi.
Kutokana na hali hiyo, Sangawe alishauri uongozi
wa Ofisi ya Mkoa wa Kigoma kujiwekea utaratibu wa kukaa na halmashauri zake
mara kwa mara ili kuangalia maendeleo ya miradi inayotekelezwa kwa fedha za
washirika wa maendeleo na kuhakikisha utekelezaji wake unakwenda sambamba na
malengo husika.
Aidha, Sangawe alisisitiza kuwa ni lazima
mamlaka zinazohusika katika kufanya makubaliano ya mikataba na wafadhili kuwa
makini na kuzingatia kuwa miradi inayotaka kufadhiliwa ni ile yenye tija kwa
wananchi na ambayo inaharakisha kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya 2025 ya
kuipeleka Tanzania katika uchumi wa kati.
“Tusisite kukataa miradi ambayo haina tija kwa
wananchi wetu, hata kama fedha ni zao lakini lazima ufadhili wao uendane na
vipaumbele tulivyojiwekea kama Taifa. Tusipo zingatia hilo tutajikuta
tunatekeleza miradi isiyo na faida kwa wananchi na kupelekea Serikali kupata
hasara,” alisisitiza Sangawe.
No comments:
Post a Comment