VIJANA
wawili wakazi wa kijiji cha Mgungira wilaya ya Ikungi mkoani
hapa,wamenusurika kifo baada ya kuanza kutapika na kuishiwa nguvu katika
shindano la kula chapati 30 pamoja na kunywa vikombe 10 vya chai ya
rangi.
Shindano hilo la aina yake hufanyika kijijini hapo ambapo
liliandaliwa,kuratibiwa na kudhaminiwa na Guhumela Lubadila na vigezo
vya kuwa mshindi ilitakiwa mshiriki ale chapati zote 30 na anywe vikombe
vyote 10 vya chai ya rangi. Vitu vyote hivyo, gharama yake ni shilingi
9,200.
Kwa mujibu wa Afisa Mtendaji Kata ya Mgungira, Hussein Juma Ng’eni,
alisema washiriki walikubaliana mshindi asipewe zawadi yoyote, zawadi
yake ni chapati 30 na vikombe 10 vya chai atakavyokuwa amekula na
kunywa.
Aidha, alisema kuwa endapo vijana hao wakashindwa kufikia lengo la kula
chapati 30 na kunywa vikombe vya chai 10, watapaswa wamlipe mmiliki wa
mgahawa aliyetambulika kwa jina la mama Benja Mgungira.
Afisa mtendaji kata huyo, alisema endapo mshindi angepatikana, mdhamini
wa shindano hilo, Guhumela, angemlipa mmiliki wa wa mgahawa, shilingi
9,200.
Ng’eni alisema vijana hao kama ingekuwa ni shindano la mpira wa miguu,
wangekuwa wametoka suluhu ya kufungana magoli sawa kwani wao kila mmoja
alikula chapati 19 na vikombe vinne vya chai ya rangi.
“Baada ya kufikia hatua hiyo, kila mmoja alianza kutapika mfululizo huku
wakitokwa na jasho jingi na kisha kuishiwa nguvu. Kitendo hicho
kilisababisha wakimbizwe katika zahanati ya kijiji, kupatiwa matibabu
.Hali zao kwa ujumla,zinaendelea vizuri,” alisema.
Alisema kuwa baada ya kushindwa katika shindano hilo, vijana hao
watalazimika kulipa shilingi 9,200 kwa mujibu wa makubaliano ya shindalo
hilo.
No comments:
Post a Comment