Mwananchi akipita kwa kuikwepa pikipiki yenye namba za usajili T 684 CJZ aina ya Fekon iliyotelekezwa kwa zaidi ya mwaka mmoja katika Kituo cha waendesha bodaboda cha Maganga Veterinary Dar es Salaam.
Mwonekano wa pikipiki hiyo kwa nyuma.
Pikipiki hiyo ikiwa katika kijiwe hicho cha Veterinary Maganga Temeke jijini Dar es Salaam.
Na Dotto Mwaibale
PIKIPIKI yenye namba za usajili T 684 CJZ aina ya Fokon iliyotelekezwa kwa zaidi ya mwaka mmoja katika kituo cha waendesha bodaboda cha Maganga Veterinary Temeke jijini Dar es Salaam inazua hofu kwa wananchi na hata kwa askari polisi ambao wameshindwa kuipeleka kituoni.
Imeelezwa kwamba pikipiki hiyo iliegeshwa katika eneo hilo na mtu mmoja ambaye alifika nayo akiwa akiiendesha mwishoni mwa mwaka jana.
Akizungumza jana na mtandao wa www. habari za jamii.com mmoja wa waendesha bodaboda wa kituo hicho ambaye hakupenda kujitambulisha jina lake alisema pikipiki hiyo inawapa hofu wananchi wa eneo hilo na hata waendesha bodaboda.
"Hata sisi wenyewe tuna hofu na pikipiki hii ndio maana tunaegesha mbalimbali na pikipiki zetu na ndio maana sitaki kutaja jina langu" alisema mwendesha bodaboda huyo.
Aliongeza kuwa awali baada ya pikipiki hiyo kutelekezwa katika kituo hicho mtu yeyote alipokuwa akiisogelea au kuigusa ilikuwa ikijiwasha yenyewe lakini baada ya kupita mwezi mmoja iliacha kujiwasha jambo ambalo limeongeza hofu kwa wananchi.
Mkazi mwingine wa eneo hilo aliyejitambulisha kwa jina moja la Ismail alisema hata walipotoa taarifa kituo cha polisi cha Maganga walishindwa kuichukua pikipiki hiyo kutokana na tabia ya kujiwasha.
Alisema aaskari wa kituo hicho ambacho kipo mita 10 na eneo ambalo ipo pikipiki hiyo walitoa taarifa kwa wenzao wa kituo cha Chang'ombe ambao nao wameshindwa kuichukua na kwenda nayo kituoni kwa ajili ya kumtambua mmiliki wa pikipiki hiyo kupitia namba zake za usajili.
Ismail alisema inawezekana pikipiki hiyo ilifungwa kifaa maalumu cha utambuzi iwapo kama imeibiwa na ndio maana ilipokuwa ikiguswa au kusogelewa inajiwasha yenyewe licha ya baadhi ya watu wanahusisha kujiwasha kwake na imani za ushirikina.
Imeelezwa kuwa pikipiki hiyo wakati inatelekezwa ilikuwa katika hali ya upya lakini hivi sasa imeanza kupoteza upya wake kwa kukosa huduma ya matunzo.
Jitihada za mtandao huu kumpata Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa huo wa Maganga ili kuzungumzia suala hilo zimeshindika baada ya kuelekezwa alikuwa Manispaa ya Temeke kwenye mkutano.
No comments:
Post a Comment