TBA YAKUSANYA BILIONI 2.6 - KATUMA BLOG tz.

HABARI ZA HIVI PUNDE

KWA HABARI ZA UHAKIKA NA KUAMINIKA


Post Top Ad

Responsive Ads Here

Friday, June 24, 2016

TBA YAKUSANYA BILIONI 2.6




Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

WAKALA wa Majengo Tanzania (TBA) umesema tayari umekusanya Sh bilioni 2.6 ikiwa ni zaidi ya asilimia 40 ya madeni waliyokuwa wakiwadai watumishi wa umma na watu binafsi waliouziwa na kupanga nyumba za serikali kwa makazi na biashara.

Akizungumza na waandishi wa habari jana wakati wafanyakazi wa TBA wakifanya usafi katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam zilizopo nyumba hizo katika kilele cha Wiki ya Utumishi wa Umma, Mkurugenzi Mkuu wa TBA, Elius Mwakalinga alisema kabla ya kulipwa kwa fedha hizo, wakala huo ulikuwa ukidai zaidi ya Sh bilioni sita ambapo baada ya kutolewa kwa notisi ya kulipa tayari wamekusanya Sh bilioni 2.6.

Mwakalinga alisema shughuli ya kuwatoa wapangaji wengine inaendelea katika mikoa mbalimbali, na mkoani Dodoma wamewaondoa wapangaji katika nyumba 27 huku Mwanza shughuli hiyo ikikwama baada ya kuibuka fujo kati ya mpangaji na mfanyakazi wa Kampuni ya Udalali ya Yono ambao ni wasimamizi katika shughuli hiyo.

“Kazi yetu sisi sio kuleta vita tunataka fedha irudi ili tuendelee na ujenzi wa nyumba nyingine, tumesikitishwa na kitendo cha mpangaji wetu Mwanza ambaye aliamua kuleta fujo na kumshambulia mfanyakazi wa Kampuni ya Udalali wa Yono wakati akiondolewa tunaomba tu wawe wastaarabu wanapotakiwa kuondoka au wakubali kulipa,” alisema Mwakalinga.

Alisema ili kuondoa tatizo la ucheleweshwaji wa ulipaji kodi katika nyumba hizo kuanzia Julai wapangaji binafsi wataanza kulipa kodi kwa miezi sita huku watumishi wa umma wakiendelea kulipa kwa miezi mitatu mitatu.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Responsive Ads Here