Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Dkt. Albina Chuwa akielezea majukumu ya ofisi hiyo kwa Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia hapa nchini Bi. Bella Bird (kulia kwake) alipotembelea leo, Makao Makuu ya Ofisi hiyo iliyopo Barabara ya Kivukoni Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Dkt. Albina Chuwa akielezea majukumu ya ofisi hiyo kwa Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia hapa nchini Bi. Bella Bird (kulia kwake), Menejimenti ya NBS na wageni walioambatana na Mkurugenzi Mkazi huyo alipotembelea leo, Makao Makuu ya Ofisi hiyo iliyopo Barabara ya Kivukoni Jijini Dar es Salaam. ( PICHA NA EMMANUEL GHULA)
Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Abina Chuwa akimkaribisha Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia nchini Bi. Bella Bird (kushoto) alipotembelea leo Makao Makuu ya Ofisi hiyo iliyopo Barabara ya Kivukoni Jijini Dar es Salaam.
Na Veronica Kazimoto
BENKI ya Dunia imeahidi kuendelea kuisaidia Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kifedha ili iweze kutekeleza majukumu yake ya utoaji wa Takwimu Rasmi nchini.
Akizungumza leo alipotembelea Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia hapa nchini Ms. Bella Bird amesema kutokana na umuhimu wa takwimu katika kupanga na kupima matokeo ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimaendeleo, Benki ya Dunia itaendelea kuisaidia NBS ili iendelee kutekeleza majukumu yake ikiwa ni pamoja na kutoa takwimu kwa wakati.
“Ili Ofisi ya Taifa ya Takwimu iweze kutoa takwimu kwa wakati, inahitaji kuwekeza katika matumizi ya technolojia ya kisasa ya ukusanyaji wa takwimu, hivyo Benki ya Dunia itaendelea kutoa msaada wa kiufundi na kifedha ili kufikia malengo yaliyoainishwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu ya utoaji wa takwimu rasmi nchini”, amesema Ms. Bella Bird.
Mkurugenzi huyo Mkazi amefafanua kuwa Benki ya Dunia inatambua umuhimu wa takwimu katika maendeleo ya nchi zote duniani ikiwemo Tanzania katika kupanga sera na kutekeleza miradi mbalimbali ya nchi husika.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa ameishukuru Benki ya Dunia kwa misaada mbalimbali ambayo imekuwa ikiisaidia Ofisi ya Taifa ya Takwimu ambayo imeongeza tija katika ukusanyaji na utoaji wa takwimu rasmi nchini.
“Napenda kuchukua fursa hii kuishukuru Benki ya Dunia kupitia ujio wako kuitembelea Ofisi ya Taifa ya Takwimu na kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na ofisi hii ikiwa ni pamoja na ukusanyaji na utoaji wa takwimu rasmi hapa nchini,” amesema Dkt. Chuwa.
Dkt. Chuwa amesema Ofisi ya Taifa ya Takwimu imeendelea kupanua wigo wa uzalishaji wa takwimu nchini ikilinganishwa na karne zilizopita.
Benki ya Dunia inaisaidia Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa kutoa ushauri wa kitalaam pamoja na fedha kupitia Mpango Kabambe wa Kitaifa wa Kuboresha na Kuimarisha Takwimu nchini ambapo awamu ya kwanza itakamilika mwezi Juni, 2018.
No comments:
Post a Comment