*Asema haki haikutendeka katika mchakato wa kupata mgombea 2015
*Akerwa polisi kuingia bungeni,amkwepa Dk.Magufuli
JAJI Mkuu mstaafu wa Tanzania, Augustino Ramadhani amesema utaratibu
uliotumiwa na Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CC) wa kukata majina
yao katika uteuzi wa urais haukuwa wa haki.
Amesema hakupata nafasi ya jina lake kuchekechwa katika uteuzi huo, bali kalamu ilipita na majina yao yakakatwa.
Amesema amepanga kwenda kuonana na uongozi wa juu hivi karibuni,
kutokana na kile alichosema hakubaliani na baadhi mambo ndani ya chama
hicho tawala,
Jaji Ramadhani ambaye alikuwa miongoni mwa wagombea waliosaka tiketi
ya urais kupitia CCM, sasa anaungana na waliokuwa wagombea wenzake
kukosoa mchakato huo wa ndani ya chama.
Jaji Ramadhani anaungana na aliyekuwa mgombea urais wa Chadema chini
ya mwamvuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa,
Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye na Profesa Mark Mwandosya ambao
walitoka hadharani na kueleza kutoridhishwa na mchakato huo.
Jaji Ramadhani ambaye hivi sasa ni Rais wa Mahakama ya Afrika ya Haki
za Binadamu, alitoa kauli hiyo katika mahojiano maalumu na MTANZANIA
yaliyofanyika ofisini kwake jijini Arusha juzi.
“Sikupata hata nafasi ya jina langu kuchekechwa kwenye mchakato wa
uteuzi wa urais ndani ya CCM… kalamu ilipitia tu majina yetu
yakaondolewa na tulitumia busara mno kukaa kimya,”alisema Jaji
Ramadhani.
Sababu za kuchukua fomu
Akizungumzia sababu zilizomsukuma achukue fomu ya kugombea urais,
Jaji Ramadhan alisema alitegemea rais wa awamu tano angetoka Zanzibar,
baada ya Bara kuongoza kwa awamu mbili mfululizo.
Alisema sababu nyingine ni kutokana na dhuluma nyingi na haki za binadamu kuvunjwa, hivyo aliamini angeleta mabadiliko.
“Niliamini sasa ni zamu ya Zanzibar baada ya Bara kuongoza kwa awamu
mbili. Kuna siku nilikutana na Kingunge Ngombale Mwiru kwenye mkutano
fulani, nikamwambia kuhusu idadi ya Serikali, yeye anasema kuwa na
serikali tatu inavunja Muungano, nikamwambia je kuwa na marais mara tatu
mfululizo kutoka upande mmoja haina athari…akanijibu ‘you have a point’
kwa hiyo ndiyo hivyo.
Alipoulizwa kuhusiana na namna alivyoshtua watu wengi pale
alipochukua fomu, Jaji Ramadhan alisema hakushtua bali baadhi ya
wanasiasa walikuwa wakieneza propaganda chafu, baada ya kuona rekodi
yake haina shaka katika uongozi.
“Watanzania hawakushtushwa, wengi walifurahi wakaona sasa wamepata
mtu kwa sababu wanajua rekodi yangu katika uongozi, wachache wa kisiasa
ndio walikuwa wanaeneza propaganda chafu kwa sababu wananiogopa.
“Miongoni mwao ni mwanahabari mmoja (anamtaja jina)naye alikuwa
akiandika habari za kunichafua kuwa inakuwaje jaji awe ndani ya chama
cha siasa na agombee urais, lakini nilimpigia nikamwonya,”alisema Jaji
Ramadhani. BOFYA HAPA KUSOMA ZAIDI
No comments:
Post a Comment