Mbunge wa Jimbo la Ubungo, Saed Kubenea
Vyama vinavyounda umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), vimepinga hatua ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwaleta wabunge wa viti maalum kutoka Zanzibar kushiriki katika vikao vya kuchagua Meya wa Halmashauri za Manispaa ya Kinondoni na Ilala.
Umesema kitendo cha wabunge hao kuapa ili kupiga kura ni kinyume cha Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977 na Sheria ya Serkali za Mitaa.
Akizungumza katika mkutano uliotishwa na vyama hivyo, Mbunge wa Jimbo la Ukonga kwa tiketi ya Chadema, Mwita Waitara, alisema wajumbe hao ni mamluki wenye nia ya kuipa ushindi CCM kwa kiti cha umeya wa Jiji.
Alisema kwa upande wa Ukawa, wajumbe wa halali wanaopaswa kushiriki kwenye uchaguzi huo ni 35 na CCM ni 31 lakini wajumbe wanne waliongezwa kutoka Zanzibar kuja kuapa ili kuongeza idadi.
Alisema mikakati ya ushindi huo imepangwa tangu awali pale ulipotolewa muongozo kutoka Tamisemi kwamba vikao hivyo vitaendeshwa na Katibu Tawala wa Wilaya.
Waitara alisema uhalali wa ushiriki wa mbunge katika vikao hivyo unatokana na tafsiri ya mbunge kuwa ni diwani pale anaposhiriki katika vikao vya halmashauri.
“Suala la serikali za mitaa siyo la Muungano, sifa ya diwani ni lazima uwe mkazi wa halmashauri husika, wabunge hawa wametokea Zanzibar hawawezi kuwa na uhalali wa kutuchagulia Meya Dar es Salaam,” alisema Waitara.
Alisema kwa kuwa suala hilo si la Muungano ndiyo maana halikuingizwa katika rasimu ya Katiba ya Jaji Warioba, Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, katiba ya Tanzania ya 1977 na katiba iliyopendekezwa.
Alisema lengo la CCM ni kumpata Meya wa Jiji na ndiyo sababu wanakesha wakihaha kuongeza idadi ya wapiga kura kwasababu idadi yao ya wajumbe katika halmashairi zote chache kuliko 91 ya Ukawa.
Naye Mbunge wa Ubungo kwa tiketi ya Chadema, Saed Kubenea alisema maelezo ya awali ya wabunge hao katika fomu za maadili, kuomba ujumbe wa kamati za kudumu walielekeza kwamba wao ni wakazi wa Zanzibar.
No comments:
Post a Comment