BAADHI ya wananchi na wapenzi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)
wamelazimika kuuzuia msafara wa mgombea mwenza wa nafasi ya urais leo
alipokuwa njiani akitokea Wilaya ya Same kuelekea Wilayani Mwanga mkoani
Kilimanjaro huku wakimuomba awasalimu na kuzungumza nao, kabla ya
kuendelea na safari yake.
……………………………………………………………………………..
Bi. Samia Suluhu alilazimika
kuusimamisha msafara wake baada ya wananchi hao kusogea zaidi barabarani
wakati akipita huku wakinyoosha mikono ya kumuomba asimame ili
azungumze nao eneo la kilometa chache kabla ya kuingia njia panda.
Wananchi hao wengi wakiwa wakinamama walimsimamisha kwa kuingia
pembezoni mwa barabara alipokuwa akipita na hivyo kulazimika kusimama
kwa dakika chache na kuzungumza nao.
Akizungumza aliwaambia amefarijika
na kuwaona na mapenzi makubwa na chama chao hivyo kuwaeleza kuwa yeye
ni mwanamke pia na anajua kwa karibu kero ambazo wanakabiliana nazo
akinamama sehemu mbalimbali na kuahidi endapo watapata ridhaa pamoja na
Dk. John Magufuli atahakikisha anasimamia vizuri utaratibu wa
kuwawezesha akinamama kupitia vikundi vya kijamii ili waweze kujikwamua
kiuchumi pamoja na familia zao.
Alisema yeye ni mwanamke mzazi
anatambua shida wanazokumbana nazo akinamama hasa kwenye wodi za wazazi
hivyo akifanikiwa kuingia madarakani atahakikisha anasimamia ipasavyo
ilani ya chama ambayo imeeleza vizuri juu ya uboreshaji huduma za afya
ikiwemo wodi za akinamama na hali ya upatikanaji madawa.
“…Matatizo ya wanawake nayafahamu
vizuri wala sisimuliwi maana na mimi ni mzazi nimeingia wodi ya wazazi
mkitupa ridhaa na mwenzangu (mgombea urais, Dk. Magufuli) nitahakikisha
nayasimamia haya vizuri,” alisema Bi. Suluhu akizungumza muda mfupi na
wananchi waliomzuia barabarani wakiomba awasalimu.
Alisema kero ya maji imekuwa
inawatesa akinamama kwa kutumia muda mwingi kutafuta maji na kushindwa
kuzalisha uchumi wa familia ipasavyo, hivyo Serikali ya CCM imeanza
mradi wa kutoa maji katika Bwawa la Nyumba ya Mungu na kuyaingiza katika
vijiji vyenye shida ya maji.
Aidha akizungumza katika mkutano
mkubwa wa hadhara Mwanga ameisikia kero ya uhaba wa mabweni kwa
wanafunzi wa kike suala ambalo linachangia kwa kiasi kikubwa mabinti hao
kutiwa mimba na kukatisha masomo eneo hilo na kudai suala hilo lipo
katika ilani ya CCM mwaka huu na litashughulikiwa vizuri endapo watapewa
ridhaa na wananchi, ikiwa ni pamoja na suala zima la kupambana na
kuongeza fursa za vijana ili kukabiliana na uhaba wa ajira.
Alisema Serikali iliyopita
imejitahidi kuongeza huduma za umeme katika vijiji ili kuchochea
maendeleo ya kiuchumi lakini katika awamu hii CCM ikipewa ridhaa
itahakikisha vijiji vilivyobaki kwa baadhi ya maeneo vinawekewa umeme.
Alisema anawapa akinamama kazi kuhakikisha Dk. Magufuli na wagombea wa
CCM eneo hilo wanashinda kwa asilimia 80 kwani wao ndio wenye ushawishi
mkubwa katika familia. Vivyo hivyo kuwataka madiwani wanaogombea
kuhakikisha mgombea uraisi na wengine wanapata kura za kutosha ili
kushinda uchaguzi.
Kwa upande wake Asumta Mshana
aliyekuwa mbunge wa CCM na uchaguzi huu aligombea na kura hazikutosha
alisema anawashangaa wanachama ambao waligombea ndani ya Chama Cha
Mapinduzi na waliposhindwa wakaamua kuondoka ndani ya chama hicho.
Alihoji kwani walipokuwa wakiomba nafasi hizo hawakutambua kuna
kushindwa na kushinda? Aliwafananisha wanaofanya hivyo ni sawa na
akinababa wanaoamua kukimbia familia zao jambo ambalo ni aibu.
“Nawashauri wababi ndani ya chama
na kukijenga chama ili kiweze kufanya vizuri, kama kura hazikutosha
safari hii usikimbie chama kwani mlikuwa hamjui kuna kushinda na
kushindwa unapoomba uongozi,” alisema.
Naye Mwenyekiti wa CCM, Mkoa Idd
Juma Mohamed alimshukuru Bi. Samia kwa kuamua kuanza kampeni katika mkoa
wake na kumuhakikishia watahimiza wapiga kura kwani Kilimanjaro bado ni
ngome ya CCm na watahakikisha wanatwaa majimbo yote, viti vya udiwani.
No comments:
Post a Comment