Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya
Maendeleo ya Kilimo Tanzania, Thomas Samkyi, akizungumza na waandishi wa
habari jijini Dar es Salaam kuhusu uzinduzi wa benki hiyo utakaofanyika
tarehe 7/8/ 2015. (Kushoto) Mwenyekiti wa Bodi ya Benki hiyo , Bi
Rosebud Violet Kurwijila.
Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya
Maendeleo ya Kilimo Tanzania, Bi Rosebud Violet Kurwijila akizungumza na
waandishi wa habari kuhusu uzinduzi wa benki hiyo. Kushoto kwake ni
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki Thomas Samkyi,
…………………………………………………………
Na Mwandishi wetu- Dar es Salaam
Rais Jakaya Kikwete anatarajiwa
kuzindua rasmi benki ya kwanza ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania, ambayo
inalenga kuanzisha mtizamo mpya wa kukiendeleza kilimo kupitia
kushirikisha wadau mbali mbali, kuangalia kila mnyororo wa thamani kwa
ukamilifu wake, pamoja na kuwa na ubunifu katika kuchangia kifedha
kwenye miradi ya muda mrefu, ya kati na muda mfupi kwenye sekta ya
kilimo. Benki hiyo inatarajiwa kutoa mchango mkubwa katika ukuzaji wa
sekta ya kilimo ambayo imeajiri zaidi ya aslimia 70 ya Watanzania.
Uzinduzi huo unatarajiwa kufanyika
kwa ngazi mbili: ngazi ya kwanza itahusisha uzinduzi wa Makao Makuu ya
TADB jijini Dar es Salaam mnamo tarehe 7 ya mwezi huu; ambapo ngazi ya
pili itahusisha uzinduzi rasmi wa TADB mbele ya wadau wake wakuu ambao
ni Wakulima, kwenye Maonesho ya Nane Nane Mkoani Lindi, katika kilele
cha Siku Kuu ya Wakulima hapo tarehe 8 Agosti 2015.
Akizungumza na waandishi wa habari
kwenye makao makuu ya benki hiyo yaliyoko Barabara ya Kinondoni,
Mkurugenzi Mkuu wa benki, Bwana Thomas Samkyi, alisema dhumuni kuu la
uanzishaji wa benki hiyo ni kuboresha tija katika uzalishaji kwenye
sekta ya kilimo kwa kuunganisha nguvu za wadau mbalimbali ili kuwezesha
uendelezaji wa miundombinu ya kilimo kama miradi ya umwagiliaji,
usafirishaji, uhifadhi, mindombinu ya masoko, n.k. ambayo inachangia
maendeleo ya sekta ya kilimo.
‘Uanzishwaji wa benki hii unalenga
kuziba mianya mikubwa ya ukopeshaji kwenye kilimo ambayo inaachwa na
benki za biashara, ili kuchochea kukua kwa sekta ya kilimo, kwa kutoa
mikopo na huduma nyingizezo za uwezeshaji wa kilimo kwa wakulima, ambao
wengi wao hawana uwezo wa kupata huduma za kibenki’ alisema Bw. Samkyi.
Akieleza zaidi kuhusu uanzishwaji
wa benki hiyo, Bwana Samkyi alisema Benki ya Wakulima itakuwa msitari wa
mbele katika kusukuma shughuli za kilimo pamoja na kuchagiza benki na
taasisi nyingine za kifedha kushiriki katika kuwezesha shughuli za
kilimo.
‘Benki hii imeundwa ili kutoa
mikopo kwa masharti nafuu, pamoja na kutoa huduma nyinginezo
zitakazoongeza uwezo wa wakulima kukopa na kuzalisha. Ili kufanikisha
haya, benki inabidi iwe na vyanzo endelevu vya fedha za kutosha kwani
nchi hii ni kubwa na wadau wa benki ni wengi sana. Lengo kuu ni kubadili
kilimo cha Tanzania kutoka kilimo cha kujikimu kwenda kilimo cha
kibiashara’ alisema Bw. Samkyi.
Benki hii pia inatarajiwa kuwa ni
kiungo muhimu cha utekelezaji wa mageuzi ya awamu ya pili ya sekta ya
kifedha, na vile vile kuboresha maendeleo ya kilimo nchini ikizingatia
Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025 pamoja na mipango mbalimbali ya
maendeleo ya miaka mitano mitano, Mkakati wa Maendeleo wa Sekta ya
Kilimo, na Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini (MKUKUTA),
pamoja na sera mbali mbali za Serikali zinazohusu sekta ya kilimo.
No comments:
Post a Comment