Zaidi ya Dola billioni nne za
Kimarekani ikiwa sawa na Trilioni nane kwa shilingi ya Kitanzania
zimewekezwa katika sekta ya umeme kwenye Miradi yote ya uzalishaji,
usambazaji na usafirishaji wa umeme nchini.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi
Mtendaji wa shirika la ugavi la umeme nchini (TANESCO) Mhandisi
Felchesmi Mramba wakati akizungumza na waandishi wa habari leo jijini
Dar es Salaam.
Amesema kuwa katika kipindi cha
miaka 10 (2005-2015), Serikali imeongeza uwezo wa mitambo ya kuzalisha
umeme katika Gridi ya Taifa kutoka MW 891 hadi kufika MW 1,501.24 sawa
na ongezeko la asilimia 68.5.
“Baadhi ya miradi iliyokamilika
ni pamojaj na mtambo wa kuzalisha umeme MW 100 uliopo Ubungo, na Ujenzi
wa mtambo wa kufua umeme MW 45 uliopo Tegeta jijini Dar es salaam.
Miradi mingine ni mtambo wa kuanzisha umeme MW 60 Mwanza, na mradi wa
umeme wa Somanga Fungu MW 7.5 Mkoani Lindi” amesema Mkurugenzi huyo.
Kwa mujibu wa Mhandisi Mramba,
kukamilika kwa Miradi hiyo kumewezesha upatikanaji wa umeme wa uhakika
nchini na kufanikisha kuondoa mgawo wa umeme hususani kuanzia mwaka 2012
na hivyo kuboresha ufanisi wa utekelezaji wa shughuli mbalimbali za
kiuchumi na kijamii.
Mtendaji huyo Mkuu wa TANESCO
ameeleza kuwa kumekuwa na mikakati mbalimbali ya kuongeza uzalishaji wa
umeme kwenye Gridi ya Taifa na nje ya Gridi ya Taifa ikiwemo utekelezaji
wa Mradi wa Kinyerezi 1 (MW 150) kwa kutumia Gesi asilia, mradi wa
kupeleka umeme katika miji ya Mpanda, Ngara, na Biharamulo.
Aidha Mkurugenzi huyo ametoa ufafanuzi kuhusu kubadilisha mfumo umeme wa LUKU utakaofanyika tarehe 1/8/2015.
“Zoezi la kubadilisha mfumo wa
LUKU litachukua muda wa saa 24 kuanzia usiku wa manane wa Agosti Mosi,
2015 hadi usiku wa manane wa tarehe 2/8/2015 sio siku saba kama
ilivyoenezwa katika mitandao ya kijamii,” amesema.
Lengo la zoezi hili ni kuongeza
kasi na kuwawezesha watu wengi kuunganishwa na mfumo mpya wa LUKU
utakaohudumia idadi kubwa zaidi ya watu tofauti na hali ilivyo sasa.
No comments:
Post a Comment