Mkuu
wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadiki akiongea na waandishi wa
habari leo jijini Dar Es salaam kueleza uamuzi wa Serikali kuongeza muda
wa Sensa ya Viwanda Tanzania Bara hadi Agosti 31,2015 na hatua
zitakazochukuliwa kufuatia viwanda 366 kushindwa kuwasilisha takwimu za
uzalishaji kwenye Madodoso ya Sensa.
Kaimu Meneja wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Mkoa wa Dar es salaam Bw.
Albert Kapala akitoa ufafanuzi wa lengo la Sensa ya Viwanda na Idadi ya
viwanda vilivyotoa taarifa za Sensa hiyo jijini Dar es salaam.
………………………………………………………………………..
Habari Picha Na.Aron Msigwa-MAELEZO.
Serikali imeongeza muda wa mwisho
wa kukamilisha zoezi la ukusanyaji wa takwimu za Sensa ya viwanda kote
nchini hadi Agosti 31 , 2015 kufuatia viwanda vipatavyo 366 vilivyoko
jijini Dar es salaam kushindwa kuwasilisha taarifa muhimu za uzalishaji
kwenye madodoso ya Sensa hiyo.
Akitoa taarifa ya kuongezwa kwa
muda wa Sensa hiyo leo jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Mkoa wa Dar es
Salaam Saidi Meck Sadiki amesema kuwa Viwanda 366 ambayo ni sawa na
asilimia 20 katika jijini Dar es salaam vimeshindwa kukamilisha na
kurudisha madodoso ya taarifa muhimu za viwanda hivyo.
Amesema Sensa hiyo ilianza Machi 9
mwaka huu na ilitarajiwa kukamilika Juni 8, 2015 lengo likiwa kukusanya
takwimu sahihi zinazohusu Sekta ya Viwanda na mchango wake katika
uchumi wa Tanzania
Amesema Sensa hiyo pamoja na mambo
mengine ililenga kupata viashiria sahihi vya uchumi pamoja na taarifa
muhimu za viwanda zikiwemo orodha ya viwanda kimkoa, anuani na mahali
vilipo, aina ya umiliki na utaifa wa wamiliki.
Takwimu nyingine ni mwaka ambao
viwanda hivyo vilianza uzalishaji, shughuli kuu ya viwanda husika,idadi
ya wafanyakazi waliopo,gharama za malipo mbalimbali kwa wafanyakazi,
mapato yanayotokana na uzalishaj na gharama za uzalishaji.
Ameeleza kuwa mwaka 2013 Serikali
iliamua kuwa ifanyike Sensa ya viwanda nchi nzima ili kubaini viashiria
vya uchumi vitakavyosaidia kuweka mabadiliko ya muundo wa sekta ya
viwanda na mchango wake katika pato la Taifa, kuboresha Sera na Programu
za kukuza ajira, utekelezaji wa Malengo ya Milenia ,Dira ya Maendeleo
ya Tanzania 2025, MKUKUTA na Mpango wa Taifa wa Matokeo Makubwa Sasa
(BRN).
Aidha, ameeleza kuwa jijini Dar es
salaam kazi nzuri imefanyika kwa wenye viwanda kutoa ushirikiano kwa
kukamilisha ujazaji wa madodoso mafupi na marefu na tayari madodoso hayo
yameshawasilishwa Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa uchambuzi.
Mhe. Saidi Meck Sadiki amefafanua
kuwa Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa kushirikiana na Wizara ya Viwanda na
Biashara inaendelea kuhakikisha kuwa asilimia 8 iliyobaki ya viwanda
vyote nchini inawasilisha taarifa husika kabla ya muda uliopangwa.
Amesisitiza kuwa zoezi hilo liko
kwa mujibu wa sheria ya takwimu ya mwaka 2012 na watakaoshindwa
kutekeleza ujazaji wa madodoso hayo hatua kali za kisheria zitachukuliwa
dhidi yao.
“Zoezi hili ni muhimu sana kwa
ukuaji wa uchumi wa taifa letu linatupa picha ya sekta ya viwanda nchini
pamoja na kuongeza uwazi katika mchango wa sekta ya viwanda katika Pato
la Taifa, hili lazima tulisimamie, wenye viwanda lazima watii sheria”
Amesema.
Kwa upande wake Kaimu Meneja
Takwimu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) mkoa wa Dar es salaam Albert
Kapala amesema kuwa Zoezi hilo ni la kitaifa hivyo taarifa zote
zinazokusanywa ni siri na zinatumika kwa matumizi ya kitakwimu tu,
Amesema katika Sensa hiyo
iliyoanza mwezi Machi mwaka huu mkoa wa Dar es salaam ulitarajia kuwa
umekusanya takwimu za viwanda 1840 ifikapo Juni 8 mwaka huu.
Ameeleza kuwa hadi sasa viwanda
vilivyoshindwa kuwasilisha taarifa kwa mujibu wa Sensa hiyo jijini Dar
es salaam ni 366 wakati vilivyowasilisha ni 1474.
No comments:
Post a Comment