Na Mwandishi wetu
MGOMBEA
Ubunge wa Jimbo la Mufindi Kusini Mkoani Iringa kwa tiketi ya Chama Cha
ACT-Wazalendo Salim Nyomolelo amesema wananchi wa jimbo hilo wasitegemee
maendeleo kuletwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutokana na chama hicho kuwa
chanzo kikuu cha rushwa na ufisadi.
Anasema sababu kubwa ya wananchi kuendelea
kukabiliwa na changamoto nyingi za kiuchumi na huduma za jamii ni kutokana na
ufisadi ambao upo ndani ya jimbo hilo na njia pekee ni kuitoa CCM katika
uchaguzi kwa njia ya sanduku la kura Octoba 25 mwaka huu.
Anasema
kuwa jimbo la Mufindi kusini lina fursa nyingi za kiuchumi lakini
zinawanufaisha watu wachache kutokana na mianya mingi ya ufisadi inayofanywa na
viongozi huku wawakilishi wa wananchi ambao ni madiwani wabunge wakikaa kimya
na kuacha wananchi wakiendelea kuteseka.
“Halmashauri
ya wilaya ya Mufindi kumekuwa na ufisadi mkubwa ambao unawashirikisha viongozi
wa kisiasa wa CCM kwa kufuja fedha ambazo zinatakiwa kutekeleza miradi ya wananchi
na ndio sababu kubwa ya madiwani na Mbunge kushindwa kuzungumzia kuhusu ufisadi
kwa kuwa nao ni wahusika wakuu,” alisema.
Nyomolelo
anasema licha ya viongozi mbalimbali katika Halmashauri hiyo kuhusika na
ufisadi lakini wamekuwa wakihamishwa vituo vya kazi kutokana na kuwa na mtandao
mkubwa kuanzia ngazi ya wilaya, Wizara ya Tamisemi pamoja na Hazina.
Anasema
kuwa ripoti ya kamati ya kudumu ya Bunge ya hesabu za serikali za mitaa ya
mwaka 2012/2013 iliyokuwa ikiongozwa na Mohamed Mobarock (CCM) ilionesha jumla
ya Halmashauri 70 kati ya 134 zilikuwa na ubadhilifu ikiwamo Mufindi ambapo
ubadhilifu huo ulishirikishwa na viongozi wasiowaaminifu katika wizara ya
Tamisemi na Hazina.
Aliongeza
kuwa CCM iliongoza jimbo hilo tangu Uhuru lakini imeshindwa kukidhi matakwa ya
wananchi licha ya halmashauri hiyo kuwa ya pili katika kuchangia pato la taifa
lakini wananchi hawanufaiki na mapato hayo kutokana na huduma za jamii
kuendelea kuwa mbovu hivyo wananchi wasitegemee jipya kutoka CCM zaidi ya
kuendeleza ufisadi.
Hata
hivyo, Nyomolelo alisema njia pekee ya kuwawajibisha viongozi wa aina hiyo
dhidi ya ufisadi ni kukichagua chama cha ACT-Wazalendo ambao kinaongozwa na
mtetezi wa wanyonge katika nchi hii Zitto Kabwe ambapo pia chama hicho pia
kinaongozwa na misingi na miiko ya viongozi ili kukabiliana na ufisadi
uliokithiri hapa nchini.
No comments:
Post a Comment