MBUNGE wa
Singida mjini na mfanyabiashara maarufu nchini, Mohammed Dewji, amesema hatagombea ubunge wa jimbo hilo tena
baada ya kulitumikia kwa miaka 10 na kuwezesha maendeleo makubwa katika sekta
za elimu na afya.
Mbunge
huyo alisema hayo akihutubia maelfu ya wananchi waliokusanyika katika uwanja wa People's Club wakati wa
uwasilishaji wa utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya mwaka 2005/ 2010 na 2010/
2015 kwenye mkutano mkuu wa jimbo.
Katika
utekelezaji huo ametumia Sh bilioni 5.
Miradi
hiyo ni pamoja na kusaidia kuongeza shule za sekondari kutoka mbili hadi 15,
kuwapo kwa vituo vya afya na kupeleka shule watu wenye mazingira magumu 15,000.
Kauli
yake hiyo iliyowaliza baadhi ya wapiga kura wake aliitoa huku akisema amechukua uamuzi huo ili kutoa fursa kwa
makada wengine wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kugombea jimbo hilo.
Tamko
hilo la Dewji lilipokelewa kwa masikitiko makubwa kwani hata alipofikia nukta
ya tamko hilo na kutoa salamu ya Chama
hicho; yaani “CCM Oyee” hakuna aliyeitikia inavyostahili zaidi ya
kusema “Hatutakiiii”.
Alisema
kuwa alipoanza safari yake ya kisiasa miaka 10 iliyopita, lengo lake kuu
lilikuwa kuleta maendeleo kwa wananchi wa jimbo hilo. “Pamoja na uamuzi wangu
wa kutokugombea, lengo langu linabaki pale pale”, alisema huku umati
ukimwangalia kwa mshangao mkubwa.
Alisema
ametekeleza majukumu yake ya kusukuma maendeleo katika jimbo lake la uchaguzi
kwa ushirikiano mkubwa na kufanikisha vipaumbele vya wakati huo ikiwamo elimu na Afya.
Alisema
kwamba kujiondoa kwake katika siasa za
jimboni kunatokana na majukumu ya biashara zake kuwa makubwa pamoja na kutaka kuwa karibu na familia yake baada
ya miaka 10 ya kuwatumikia wananchi wa Singida.
"Ukichukulia
kuongezeka kwa-mvi kichwani, ukilinganisha wakati wa awamo ya kwanza, nafikiri
ni busara sasa kutimiza majukumu haya ya familia ambayo niliyabania nafasi yake
kwa kipindi cha miaka 10.
"Pia
siyo siri kwamba majukumu ya biashara zangu yamebadilika katika kipindi cha
miaka ya hivi karibuni. ukuaji wa biashara zangu umeambatana na kuongezeka kwa
majukumu, hususan mahitaji ya muda zaidi," alisema.
Akizungumzia
sekta ya afya alisema wananchi wa Singida walifanikiwa kukabiliana vilivyo na
ugonjwa hatari wa malaria kwa kugawa vyandarua zaidi ya vyandarua 6,000 kwa
mama wajawazito na watoto chini ya miaka 5.
"Kwa
kusambaza vyandarua hivi, tulifanyikiwa kupunguza vifo vya watoto chini ya
miaka 5 kwa asilimia hamsini" alisema akishangiliwa.
Aidha
alishirikiana na mamlaka husika kupambana na ugonjwa sugu wa mtoto wa jicho kwa
kupeleka madaktari bingwa na kufanya kambi kwenye hospital ya mkoa, waliotoa huduma ya upasuaji wa jicho
na kutoa miwani kwa zaidi ya wananchi 1,000.
"Tulifanikiwa
kujenga wodi ya macho, ndani ya hospitali yetu ya mkoa. Tulifanikiwa kuchangia ujenzi, wa zahanati za
Mungumaji, na Manga ambazo zimekamilika! na zahanati ya kijiji cha Ititi ambao
bado ujenzi unaendelea," alisema.
Pamoja
na ujenzi huo pia alielezea kusaidia baiskeli kwa walemavu na kufunga nishati
ya umeme jua, pamoja na majokofu ya kutunzia dawa, kwenye zahanati za Manga na
Unyambwa!
Akifafanua
zaidi katika sekta ya elimu alisema kwamba walijenga vyumba vya madarasa,
kuweka matangi ya maji ya kuvunia maji ya mvua, vyoo, na kusambaza madawati
katika shule mbali mbali za msingi na sekondari
jimboni Singida mjini.
Aidha
alichangia vitabu zaidi 1000, vya masomo ya sayansi na sanaa, kwa shule za
serikali ndani ya manispaa ya Singida.
Akizungumzia
sekta ya maji walifanikiwa kuchimba visima viwili kwenye mtandao wa Suwasa na
vingine 45 ndani ya baadhi ya vitongoji vyetu vya manispaa ya Singida.
Aidha
alisema alifanikiwa kusukuma mradi wa visima 10, unaofadhiliwa na benki ya
dunia, akisisitiza kuwa wakati akiingia mwaka 2005 upatikanaji wa maji safi na
salama ulikua asilimia 23 na sasa upatikanaji wa maji umefikia asilimia 81.
Pia
alisema amefanikiwa kuisukuma serikali, kujenga barabara za kiwango, cha
changarawe ndani ya manispaa na kufanya manispaa kuwe na barabara zinazopitika
kwa kipindi chote!
Akiwashukuru
wananchi wa Singida alisema kwamba: "kuwatumikia ninyi imekuwa ni tunu
kubwa sana niliyobarikiwa katika kipindi hiki cha miaka 10, na najisikia kuwa
nimependelewa kwa kujifunza mambo mengi yanayohusu Singida na uongozi bora, na
hususan mapungufu yake, ikiwemo mimi mwenyewe."
Alisema
dhamira yake kwa wananchi haitokani na nafasi yangu kama mbunge ama mwanasiasa,
akisisitiza kuwa dhamira yake ya uzaliwa inayotokana na mapenzi aliyonayo kwao
na imani aliyonayo juu ya uwezo wa kuijenga Singida.
Mkutano
huo mkubwa wa aina yake ulipambwa na mwanamuziki nyota wa kizazi kipya nchini,
Nasib Abdul maarufu kama “Diamond Platinum”.
No comments:
Post a Comment