VIONGOZI
wa Chama cha ACT Wazalendo wanatarajia kutoa msimamo wa chama hicho katika
masuala mbalimbali ya kitaifa katika mkutano wa hadhara utakaofanyika kesho
katika viwanja vya Mwembe Yanga.
Akizungumza
na waandishi wa habari kuhusu mkutano huo, Katibu wa Mipango na Mikakati
(Taifa), Habibu Mchange alisema, mkutano huo ni kwa ajili ya kukikabidhi chama
kwa wakazi wa jiji hilo kama walivyofanya katika mikoa mingine.
Alisema
mkutano huo pia utatumika kuwatambulisha wanachama na viongozi wa vyama
mbalimbali waliojiunga na chama hicho.
"Mkutano
huu utatumika kutangaza na kusisitiza dhamira yetu ya kuwataka Watanzania
kuishi katika misingi ya haki, undugu, umoja na mshikamano kwa kutumia miiko
iliyowekwa katika Azimio la Tabora linalohuisha Azimio la Arusha," alisema
Mchange.
Kwa
upande wake, Katibu wa Mambo ya Nje wa chama hicho, Venance Msebo alisema,
katika mkutano huo viongozi wa kitaifa wa chama hicho wakiongozwa na Zitto
Kabwe watasisitiza msimamo wao wa kushiriki Uchaguzi Mkuu kikamilifu.
"Tumejipanga
kusimamisha wagombea katika ngazi zote kuanzia udiwani hadi urais, lakini
litatolewa ufafanuzi zaidi katika mkutano huu wa kihistoria utakaofanyika
Jumamosi," alisema.
Alisema
pia watatoa tamko kuhusu maendeleo ya uandikishwaji wa wananchi katika Daftari
la Kudumu la Wapiga Kura unaondelea
nchini.
No comments:
Post a Comment