![Image result for DAWASCO](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEjfTWFHeafdkIT_kBOsz830CDv9CA2SNrRYR0O8ZeQPK4Decplz0pQLCEhKuYsUwt-gYN4LG40La5e_leMsxejZAehcLnjQ63TKobx-lmIjfovRhLx5IHXfBzkTWBLbqyTUCeI1iD8BM2A/s1600/Untitled.png)
Shirika
la Majisafi na Majitaka jijini Dar es Salaam (DAWASCO) limeanza zoezi maalum la
kuondoa mita za Maji zote chakavu na za muda mrefu katika maeneo mbalimbali ya
jiji la Dar es Salaam pamoja na miji ya Kibaha na Bagamoyo mkoani Pwani ili
kuweza kuongeza ufanisi katika usomaji wa Mita, kupunguza kiasi cha Maji kinachopotea
na kutoa matumizi halisi ya Maji yanayotumiwa na mteja.
Akizungumzia
wakati wa zoezi hilo hilo, Kaimu Meneja Uhusiano wa Dawasco, Bi. Everlasting
Lyaro ameeleza kuwa shirika linaendelea
na zoezi la kubadilisha mita za Maji zote ambazo ni mbovu na zenye umri mkubwa
kwenye maeneo yote ya Jiji la Dar es Salaam pamoja na maeneo ya mkoa wa pwani
ambapo mita takribani 25,000 zimekwisha badilishwa hadi kufikia sasa.
“Shirika
linaendelea na zoezi la kuondoa mita za Maji ambazo ni chakavu na za muda
mrefu, tayari tumefanikiwa kubadilisha Mita mpya za Maji zipatazo 25,000 katika
makazi ya watu, taasisi pamoja na viwanda na lengo letu mi kuweza kubadilisha Mita za
Maji zipatazo 85,000 hadi kufikia mwisho wa mwaka huu ili kusaidia kutoa
matumizi halisi ya Maji yanayotumiwa na mteja wetu” alisema.
Alitumia
nafasi hiyo kuwaomba wananchi kutoa ushirikiano kwa wafanyakazi wanaofanya
zoezi hilo na endapo watapata wasiwasi basi waulize vitambulisho vya kazi ili
kuepuka utapeli.
“Wananchi
watupe ushirikiano ili zoezi hili lifanikiwe na kukamilika kwa wakati kwani
lina faida kwetu sisi kama shirika na kwa mteja. Pia tukumbuke kuwa zoezi hili
ni bure hivyo wananchi wasidanganywe kuchangia hela yoyote” alimalizia Bi Lyaro
Wakizungumzia
juu ya zoezi hili wananchi wanaohudumiwa na shirika hilo akiwemo Bi. Hadija
Omary mkazi wa Mwananyamala A, amepongeza hatua hiyo iliyochukuliwa na Dawasco
kwani itasaidia kuondoa kero iliyokuwepo ya mita hizo kuvuja na kupelekea bili
Maji ya mteja kuwa kubwa.
“Tumefarijika
sana kuona Dawasco wameanza kubadilisha mita zao kwani ni za muda mrefu na zimekuwa
zikivujisha Maji na kupelekea bili zetu za maji kupanda kila wakati” alisema.
Naye,
Bw. Boniface Mwakipesile, mkazi wa
Mikocheni B, amezilalamikia mita hizo mpya na kudai kuwa tangu
zilipofungwa bili yake ya Maji imepanda ikilinganishwa na siku za nyuma, hivyo
ameshauri elimu zaidi itolewe kuhusiana na mita hizo.
“Mita
hizi mpya za Maji mimi binafsi sizielewi kabisa, tangu zilipofungwa nashangaa
bili yangu ya Maji inakuja tofauti, imekuwa kubwa sana ikilinganishwa na zamani
hivyo Dawasco wazidi kutuelimisha zaidi maana wengi wanaziona kama mita za
mwendo kasi” alisema.
No comments:
Post a Comment