Waziri Mkuu , Kassim Majaliwa amemwagiza Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa
Ruvuma, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Zuberi Mwombeji awakamate maafisa
wanne na kuhakikisha wanapelekwa Masasi chini ya ulinzi ili wajibu
tuhuma za upotevu wa tani 2,138 za korosho
Maafisa hao ni Kaimu Meneja Mkuu Chama Kikuu cha Ushirika cha Masasi
(MAMCU), Bw. Kelvin Rajab na Meneja Tawi wa MAMCU, Bw. Lawrence Njozi.
Wengine ni wakurugenzi wa kampuni ya YURAP ya Masasi inayohusika na
uhifadhi wa mazao kwenye maghala, Bw. Yusuph Namkukula na Bw. Ramadhani
Namakweto.
Waziri Mkuu alifikia uamuzi huo kwenye kikao alichokiitisha Songea mjini
jana jioni, baina ya watendaji kutoka Bodi ya Korosho Tanzania, MAMCU,
wamiliki wa ghala la BUCO - Masasi na kikundi cha wakulima sita
waliowawakilisha wenzao kutoka vyama vya msingi (AMCOS) vya wilaya za
Mtwara na Masasi.
Katika kikao hicho, Waziri Mkuu alitaka apatiwe maelezo ya kina ni wapi
zilipo hizo tani 2,138 za korosho wakati taarifa waliyompatia viongozi
hao jana inaonesha kwamba, waliuza korosho zote na hakuna hata kilo moja
ambayo haijanunuliwa katika mnada wa tano uliofanyika Novemba 10, mwaka
jana.
Kaimu Meneja Mkuu wa MAMCU, Bw. Kelvin Rajab alikiri mbele ya Waziri
Mkuu kwamba korosho zote ziliuzwa na zilishalipwa na wanunuzi wa mnada
wa tano lakini akadai hakupewa taarifa ya kukosekana kwa kiasi hicho cha
korosho.
Naye mmiliki wa ghala la BUCO, Bw. Ramadhan Namakweto alikiri kupokelewa
kwa korosho hizo ghalani kwake lakini akashindwa kutoa maelezo ni kwa
nini hazionekani zilipo.
“Tangu mnada wa tano, mmekwishafanya minada mingine mitano hadi kufikia
mnada wa 10. Kama kweli hizo korosho zipo ghalani, ni kwa nini korosho
za hawa wakulima hazijatolewa ghalani na kuuzwa katika minada iliyofuata
huku taarifa yenu ya fedha kuwa mlishazipokea na kuziuza?” alihoji
Waziri Mkuu bila kupata majibu ya kueleweka.
Tuhuma zinazowakabili maafisa hao wanne ni kuwalipa kilo pungufu ya zile
zilizowasilishwa ghalani, wakulima wa korosho katika wilaya ya Masasi
na kutowapa maelezo yoyote juu ya upungufu huo. Mfano ni kufanya makato
ya unyaufu kwa wakulima wa chama cha msingi CHAMALI kinyume na maagizo
ya Serikali.
Nyingine ni kutowalipa fedha kwa wakati wakulima waliouza korosho kwenye
mnada wa tano wa tarehe 10 Novemba 2016 na kutokutoa maelezo yoyote
licha ya kuwa MAMCU ilishauza korosho hizo kwenye minada iliyofuatia na
kupokea malipo.
Nyingine ni kutopelekwa mnadani kwa makusudi kwa tani 2,138 za korosho
zilizokuwa katika maghala ya Mtandi na BUCO tangu Novemba 11, mwka jana;
kutokutolewa taarifa ya kuwepo korosho hizo kwa mamlaka husika na
kuwasababishia hasara wananchi.
Tuhuma nyingine ni kushindwa kufuatilia malipo ya korosho ya tani
1,156,262 ambazo ziliuzwa kwenye mnada wa 10 uliofanyika Desemba 21,
2016. Korosho hizo zilinunuliwa na Maviga East Africa (tani 503,297);
Machinga Transport (tani 104,200); Tastey (319,576) na Saweya Impex
(tani (229,189).
Kutokana na mapungufu hayo, Waziri Mkuu aliagiza watu hao wapelekwe
Masasi chini ya ulinzi ili uchunguzi ufanyike na pia amemuagiza Mdhibiti
na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) afanye ukaguzi wa hesabu za
MAMCU na kujiridhisha kiasi cha korosho kilichonunuliwa; fedha
zilizolipwa na kuingia akaunti za MAMCU; kiasi cha fedha zilizolipwa kwa
vyama vya msingi na wananchi kwa ulinganifu na bei ya korosho kwa kila
mnada husika.
Post Top Ad
Responsive Ads Here
Sunday, January 8, 2017
Home
Unlabelled
WAZIRI MKUU AGIIZA MAOFISA WANNE WAKAMATWE
WAZIRI MKUU AGIIZA MAOFISA WANNE WAKAMATWE
About Unknown
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Post Top Ad
Responsive Ads Here
No comments:
Post a Comment