NI
ZAIDI ya kujikuta juu ya kitanda na msichana unayempenda kuliko wote
duniani. Ni zaidi ya kutazama bao la ushindi la timu yako katika dakika
za majeruhi katika mechi muhimu. Yote haya hayazidi starehe ya kubwia
unga.
Sahau
kuhusu bia, sigara, Sahau kuhusu kila starehe. Inatajwa kuwa hakuna
starehe kama unga. Na sasa Watanzania wanaendelea kumshangaa mtu
anayeitwa Chid Benz. Mwanamuziki hodari wa kizazi hiki katika zile
staili za vijana za muziki wa kufokafoka.
Chid
anateketea. Mwili wake kwa sasa ni kama mahindi ya shambani yaliyoliwa
na nzige. Mwili wake ni kama kama gari lililoungua likaisha. Amebaki
mifupa tu. Unaweza kupishana naye bila ya kumfahamu kama bado kichwani
unatembea na taswira ya yule Chid Benzino mwenye mashavu manene, miwani
usoni, na taulo shingoni.
Wasichofahamu
watu wengi ni ukweli kwamba wakati sisi tukiendelea kumshangaa Chid,
kumbe yeye ndiye anatushangaa zaidi sisi. Anatushangaa kwanini
hatuungani naye katika starehe yake tamu. Anatushangaa kwanini hatupo
katika safari yake ya kubembea.
Kwanini
anatushangaa? Ninesema hapo juu hakuna starehe tamu zaidi ya unga. Kitu
cha muhimu hili ni kutoonja starehe yenyewe. Ukionja hautabaki. Hata
Chid si ajabu zamani alikuwa analaani wala unga. Kosa kubwa alilifanya
katika kuonja tu. Ukionja ni vigumu kutoka katika mtego.
Ni
hapo ndipo lilipo tatizo la Chid na watumiaji wengine. Kikubwa
wanachotakiwa kukifanya kuachana na unga hawawezi kukifanya. Kitu cha
kwanza kabisa ni kuukana utamu wake. Kuukana utamu wake ni kama kuikana
nafsi yako. Hapa ndipo ilipo vita kubwa ya kuacha.
Kwanza
inabidi uone mapungufu makubwa ya unga lakini kama ukilegeza moyo kamwe
hauwezi. Kwa mfano, leo Chid hajioni mchafu, hajioni amekonda, hajioni
amepoteza nuru. Utamu wa unga umezidi akili ya kujitafakari (self
assessment). Ikifika hapo kazi inakuwa nzito zaidi.
Kumpeleka
Chid katika vituo vya matibabu (rehabilitation centres) ni kupoteza
muda mpaka pale moyo wake utakapoanza kujifanyia self assessment kuwa
amepotea, anahitaji msaada na anachukia unga. Akifika hapo atashinda
vita.
Chukulia
kwamba familia yako imekuomba mtoke out na uwape muda wa kuwa na wewe.
Wanaweza na tabia yako ya kupenda mpira kuliko wewe. Unawakubalia
walichokuomba. Lakini wanakupeleka katika hoteli ambayo watu wanatazama
mpira. Lazima moyo wako utakuwa unafuatilia kwa karibu matokeo huku
mwili wako ukiwa mezani na familia.
Kitu
cha aina hiki kinaitwa addiction. Ndipo alipofika Chid. Kama ambavyo
wewe unashangaa kwanini mtu hapendi mpira au muziki, basi na ndivyo Chid
anavyotushangaa kwanini na sisi wengine hatupendi unga. Alipofikia yeye
na sisi wengine wote tumefika ingawa sisi tuna starehe tofauti na yeye.
Kabla
ya matibabu kitu cha msingi kwa Chid ni kukutana na mwanasaikolojia wa
kumshawishi aelewe kwamba kitu anachokiona kitamu kumbe sio kitamu. Nani
anaiweza kazi hii? Ni kazi ngumu. Ndio maana washkaji zake
walipompeleka Bagamoyo alitoroka na kuendelea na starehe yake kwa sababu
hakuwa tayari kuona utamu wake unaitwa uchungu.
Mwisho
wa Chid? Sitaki kuingilia kazi ya Mwenyezi Mungu lakini mwisho wake
unatabirika kiurahisi zaidi pengine kuliko mwisho wa watu wengi
tunaomshangaa. Sisi tuna siku zetu za ahadi na tunaweza kuondoka mapema
hapa duniani kuliko yeye, hata hivyo tutaondoka kwa vifo
visivyotabirika.
Chid
anaweza kufuata njia za akina Whitney Houston tu. Watu wengi wa aina
yake huwa inatokea tunawaokota mtaroni au chumbani wakiwa wametangulia
Mbele ya haki. Inatokea huwa wanajidunga kupitiliza, au kuliko miili yao
inavyoweza kuhimili uzito wa dawa aliyotumia siku hiyo. Kwa kiingereza
cha matumizi ya unga wanaita overdosing.
Hili
sio la kuombea lakini maisha ya kufichana yamepita zamani jamani. Kama
tunahitaji lisitokee basi ni kwa Chid mwenyewe kumjua adui yake na
kupambana naye. Adui wa Chid sio unga. Adui wa Chid ni akili yake
mwenyewe. Unga upo tu, lakini mbona wengi hatutumii?
Ana
bahati mbaya ameangukia katika starehe ambayo inammaliza. Sisi wengine
tuna matatizo kama yake ya kuendekeza starehe lakini bahati nzuri huwa
hazitumalizi. Starehe ya kubishana nani zaidi ya Lionel Messi na Ronaldo
haiwezi kutumaliza kwa urahisi.
No comments:
Post a Comment