NAMNA YA KUJIEPUSHA NA HARUFU YA MWILI ISIYOPENDEZA - KATUMA BLOG tz.

HABARI ZA HIVI PUNDE

KWA HABARI ZA UHAKIKA NA KUAMINIKA


Post Top Ad

Responsive Ads Here

Friday, April 22, 2016

NAMNA YA KUJIEPUSHA NA HARUFU YA MWILI ISIYOPENDEZA

KATIKA maisha tunayoishi, hasa mijini, watu wengi hukutana maofisini, kwenye daladala, vyuoni na kadhalika. Lakini katika kukutana huko, baadhi ya watu hutoa harufu ya mwili isiyopendeza. Makala haya yaliyokusanywa na MWANDISHI WETU kwa msaada wa mtandao wa kompyuta inajaribu kuangalia asili ya tatizo hili linalokera na namna ya kuondokana nalo.

Huwa inatokea mwili wako kutoa harufu ambayo inakera kwa wengine au kwako mwenyewe kuivuta puani. Harufu hii inafanya hata nguo ulizovaa zitoe harufu, inaharibu uhusiano na kufanya watu wengine wakuepuke.

Sikiliza hii nukuu: "Wakati mwingine, mtu mwenye tatizo linalokera, si yeye anayekereka, badala yake wanaokereka ni wale watu anaoishi nao ama kufanya nao kazi."


Mwili wako unapotoa harufu isiyopendeza, utawaudhi watu kila unapokwenda, iwe kwenye basi, kwenye maduka yaliyojazana watu au hata kwenye sehemu za vinywaji kama vile baa. Na hasa utamuudhi kabisa mpenzi wako kama si mke wako.

Mara nyingi harufu ya mwili, uchunguzi unaonesha, inawatoka sana wanaume kuliko wanawake (tutaangalia hili baadaye).

Kama harufu unagundua kwamba inatoka kwenye mwili wako, wewe mwenyewe utapatwa na mteru (panic) kidogo. Kama inatoka kwa mtu mwingine, atakukera lakini wewe utajisikia hauna balaa. Mara nyingi kama inatoka kwa mtu unayemheshimu, kiustaraabu utaogopa kumwambia lakini unaweza kuwaambia wengine kuhusu huyo mtu.

Harufu inatokana na nini?
Harufu hii mara nyingi inatokana na jasho. Ni vyema ieleweke kwamba kiuhalisia jasho halina harufu kabisa. Kinacholeta harufu ni bakteria ambao huishi kwenye ngozi na ndio wanaobadilisha jasho hili na kuwa harufu isiyopendeza.

Mtu huzalisha jasho la aina mbili, apocrine na eccrine.
Jasho aina ya eccrine hufanya kazi ya kurekebisha ama kupunguza joto mwilini, na hutokea wakati mtu anapofanya mazoezi, kazi ngumu ama kunapokuwa na joto jingi kama ilivyo kwa jiji kama Dar es Salaam sasa.

Apocrine ni jasho maalumu analotoa mtu katika baadhi ya maeneo, kama vile katikati ya vidole vya mikono ama miguu, sehemu za siri hususani katikati ya mapaja au kwenye korodani kwa wanaume, kwenye makwapa au hata kwenye mfereji uliopo karibu na tundu la haja kubwa.

Ingawa majasho yote haya huweza kumletea mtu taabu, lakini jasho hili la apocrine ndilo tishio zaidi kwa harufu.

Kinachotokea, kama ambavyo tumeshadokeza hapo juu ni kwamba baadhi ya bakteria wa asili katika mwili hula jasho la apocrine na wanapokuwa katika harakati za kula jasho hilo huzalisha kemikali ambazo ndizo hutoa harufu isiyopendeza.

Kuwa na uzito mwingi, kula chakula kama vile chenye vitunguu zaidi, samaki na viungo vingi husababisha jasho hili kuongezeka.

Kutoosha ama kuvaa nguo ambayo ni chafu siku baada ya siku, hufanya jasho kuganda kwenye nguo, hali ambayo huvutia bakteria wengi zaidi na kusababisha harufu kali zaidi.

Kwa nini wengine miili hainuki?
Sababu kubwa ya mwili kutoa harufu, kitu ambacho pia kinaweza kuvutia magonjwa mengine, hususani ya ngozi, ni mtu kutokuwa msafi. Kuna wale ambao hawafui nguo na hawaogi kadri inavyostahili.

Kwa mantiki hiyo usafi hauishii katika kuoga tu asubuhi na jioni, bali pia kufua nguo zako kila baada ya kuzivaa mara moja.

Pia nguo za pamba zinaaminika kuwa nzuri zaidi ya zingine kwa sababu zinaweza kumeza harufu mbaya kirahisi na kupunguza joto.

Vile vile watu wanapishana kuhusu idadi ya bakteria walio nao katika miili yao. Kuna watu wana bakteria wengi wanaokula jasho na kuzalisha kemikali zinazonuka kuliko watu wengine. Hili ni suala la maumbile. Hata hivyo, wote hawa wanatakiwa kuimarisha usafi.

Sababu nyingine ya kupisha harufu mwili ni mambo yanayosababisha jasho. Kuna watu wanafanya kazi zenye kutoa jasho zaidi kuliko wengine ama wanafanya kazi kwenye mazingira ya joto kuliko wengine na pia wengine hufanya mazoezi ya kutoa jasho na wengine hawafanyi.

Watu wengine mijini, wanakuwa na muda mwingi wa kufanya kazi kuliko ule wa kupumzika kwa hiyo unakuta hawapati ama wanakuwa wavivu kuangalia suala la usafi wa miili yao au nguo zao.

Kitu kingine kinachoudhi ni muguu inayonuka, na hasa mwenye kunuka miguu anapovua soksi. Hili ni tatizo wanaloita la kawaida la mwili ingawa pia harufu kutoka mtu mmoja hadi mwingine hupishana pia. Tatizo hili hukabili theluthi moja tu ya wanawake lakini karibu asilimia 50 ya wanaume hunuka miguu yao na wakivua soksi na viatu vyao, mh... ni hatari!

Kutokana na mwili kuwa na mamilioni ya tezi zinazozalisha jasho, miguu yetu hutoa hadi lita nne na nusu ya jasho kila wiki!

Tatizo la kunuka miguu linaweza kudhibitiwa kwa njia za kawaida tu na wala si matibabu, labda kama mtu anaugua fangasi. Kubwa kuhusu kuondokana na tatizo hili ni kuosha na kukausha vidole vya miguuni, hususani nyufa zinazotenganisha kidole kimoja na chenziye na kuvaa viatu au soksi inazopitisha hewa.

Lakini pamoja na hayo, kuna vitu vingi vinatengenezwa viwandani katika kupunguza harufu ya miguuni. Tatizo linapoonesha kuwa kuna bakteria wengi wanaozalisha kemikali katika eneo hilo ambazo ndizo hunuka, mtu anashauriwa kumuona daktari. Anaweza kupewa dawa za krimu, antibiotics na kadhalika.

Wanaume na wanawake
Tafiti zinaonesha wanaume wengi huwa na harufu mwilini isiyopendeza kulinganisha na wanawake. Sababu kubwa ni wanaume kujishughulisha na mambo mengi ya kutoa jasho kulinganisha na wanawake.

Pia tafiti zinaonesha kwamba wanaume si watu wa kujishuku sana kama wanatoa harufu kulinganisha na wanawake.

Kadhalika maumbile ya wanawake huwalazimisha kuoga mara kwa mara kulinganisha na wanaume.

Tafiti pia zinaonesha kwamba wanawake hupendelea sana kutumia manukato ya kuondoa harufu ya mwili kuliko wanaume.

Mambo muhimu ya kufanya
Tumeona kwamba kimsingi jasho la mtu halinuki lakini husababisha harufu linapoliwa na bakteria, kwa hiyo njia kubwa ya kufanya mwili usinuke ni ama kuondokana na jasho, kuliondoa haraka mwilini ama kuua bakteria walioko kwenye mwili.

Kwa vile mazingira yanatulazimisha kutoka jasho, ni muhimu kuliondoa jasho kila mara kwenye miili yetu, na hivyo tunapaswa kuzingatia usafi.
Maeneo muhimu ambayo yanasisitizwa kufanyiwa usafi ili kuondoa jasho na bakteria ni yale ya kwenye kwapa, vidole vya miguu ama maeneo ya sehemu za siri.
Katika kwapa, pia inashauriwa mtu kunyoa nywele za eneo hilo mara kwa mara kwa sababu hazina lolote zaidi ya kufuga bakteria na kuwapa mahala pazuri pa kuzaliana pamoja  na kukaribisha jasho zaidi.

Pili, ni muhimu sana kufua nguo zako vizuri kabisa kwa sabuni, hasa zile ambazo zinavaliwa katika maeneo yenye jasho jingi kama vile soksi, nguo za ndani na fulana. Usivae nguo uliovaa jana hata kama unadhani bado inafaa kwa sababu lazima nguo hiyo ina kijiharufu kilichotokana na jasho la jana.

Tatu, inatakiwa mtu aoge  mara mbili au zaidi kwa siku, hususan katika jiji lenye joto kama Dar es Salaam. Pia inatakiwa kujali sabuni zinazoaminika kuua bakteria kwenye mwili. Hizi husaidia kupunguza bakteria ambao huozesha jasho haraka.

Nne, ni vizuri kutumia manukato ya kawaida kwa sababu yanakufanya unukie vyema na watu kupenda kuwa nawe karibu. Lakini jihadhari kama manukato hayo yanawakera wengine mnaokuwa nao maofisini. Wengine wana mzio na manukato.

Tano, jikaushe vyema kwa taulo kila unapotoka bafuni na mwisho epuka kula vyakula vilivyoungwa sana ama vinavyotoa haufu kali.

Kumuona daktari
Kuna wakati jasho linalomtoka mtu ni jingi mno na si la kawaida. Hapo mtu anaweza kumuona daktari ili kupunguza jasho hilo lisilo la kawaida. Mtu wa aina hii pia anaweza kufanyiwa upasuaji ili kuondolewa idadi ya tezi zinazozalisha jasho jingi mwili mwake.

Kama mtu ana magonjwa ya ngozi katika maeneo yenye jasho jingi, yaani makwapani, vidoleni na sehemu za siri, pia anatakiwa kumuona daktari haraka.

Kumbuka pia kwamba harufu fulani inaweza kuonesha kuwa mhusika anasumbuliwa na ugonjwa fulani. Kwa mfano, harufu kama ya bia inaonesha kuwa mtu huyo ana fangasi wengi na hawa mara nyingi hukaa ukeni.

Harufu kama ya polish inaweza kuonesha kuwa mhusika ana ugonjwa wa kisukari na harufu kama ya ammonia, inaweza kuonesha kuwa mhusika ana tatizo la ini.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Responsive Ads Here