MMOJA wa makada wa CCM
waliojitokeza kuchukua fomu za kuwania urais wa chama hicho, Profesa Sospeter Muhongo amesema pamoja na utiriri wa
wagombea kutoka chama hicho tawala, mwisho wa siku nchi inapaswa kuongozwa na
mtu mwenye kuielewa vyema Tanzania na ambaye atakuwa tayari kuivusha nchi
kiuchumi.
Aliyasema hayo akiwa
Musoma, mkoani Mara wakati akiwashukuru wanaCCM waliojitokeza kumdhamini katika
harakati zake za kuisaka Ikulu baadaye mwaka huu, huku akisema pamoja na
utayari wake, wamwombee apitishwe na CCM.
“Nchi ni tajiri na hakuna
sababu ya kuendelea kuwa masikini. Gesi tutauza nje, madini tutauza nje, nyama
na maziwa vyote tutauza nje, tukifanya hivyo itatusaidia kuinua kipato chetu…,”
alisema.
WASSIRA

MGOMBEA wa nafasi ya
urais ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Stephen Wassira amesema kujitokeza kwa idadi kubwa ya
wanaoomba nafasi hiyo kwa tiketi ya chama hicho inatokana na ukubwa wa CCM,
ambayo ina hazina kubwa ya viongozi.
Akichangia hotuba ya Bajeti
ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2015/2016 bungeni mjini Dodoma jana kwa kujibu
baadhi ya hoja zilizojitokeza wakati wa mjadala, Wassira ambaye pia ni Waziri
wa Kilimo, Chakula na Ushirika, alisema CCM ni tofauti na vyama vingine ambavyo
idadi ya viongozi wao wakishapanda helikopta hakuna mwingine anayebaki chini.
Alisema CCM ni chama
kikubwa chenye demokrasia na wala wananchi wasitishwe na idadi kubwa ya wawania
urais CCM ambao sasa wanakaribia 40 na kusisitiza kuwa chama hicho kina
utaratibu mzuri unaokubalika na wenye kueleweka kwa jamii kuhusu namna ya
kupata viongozi.
“Wingi wa wagombea urais
ndani ya CCM unatokana na ukubwa wa chama na kukubalika kwake, tofauti na vyama
vingine ambavyo viongozi wake wakishapanda helikopta hakuna tena mwingine
anayebaki chini,” alisema Wasira.
NYALANDU

WAZIRI wa Maliasili na
Utalii, Lazaro Nyalandu amesema ni lazima Watanzania wanufaike na rasilimali za
taifa kabla ya wengine kwa kuwa Mungu amezishusha kwa ajili yao.
Amesema rasilimali hizo
ndizo zitatumiwa kuwaendeleza vijana kuongoza na kushika uchumi wa taifa, kwani
vijana ndio dili na si bomu kama baadhi wanavyodai.
Nyalandu aliyasema hayo
juzi wakati akizungumza na mamia ya wanachama wa CCM waliojitokeza kumdhamini
katika ofisi za CCM Mkoa wa Kilimanjaro.
Alisema ni lazima jimbo
la Moshi Mjini lirudi mikononi mwa CCM kwa kuwa hakuna sababu ya kushikiliwa na
wapinzani.
No comments:
Post a Comment