MBIO ZA URAIS 2015: WALICHOKISEMA LOWASSA, PROF. MWANDOSYA, DK MWAKYEMBE - KATUMA BLOG tz.

HABARI ZA HIVI PUNDE

KWA HABARI ZA UHAKIKA NA KUAMINIKA


Post Top Ad

Responsive Ads Here

Monday, June 22, 2015

MBIO ZA URAIS 2015: WALICHOKISEMA LOWASSA, PROF. MWANDOSYA, DK MWAKYEMBE

LOWASSA 
Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, akizungumza na Wanachama wa CCM na wananchi katika Uwanja Samora Mjini Iringa  baada ya kukabidhiwa majina ya wanaCCM zaidi ya 58 elfu waliomdhamini kugombea urais katika Mkoa huo
 
ASKOFU wa Kanisa la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Iringa, Dk Owdenburg Mdegella ameungana na maelfu ya wakazi wa mkoa wa Iringa kumuunga mkono Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa katika harakati zake za kutafuta ridhaa ya  CCM ili awanie urais katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.  


Zaidi ya wanaCCM 58,000 wakiwemo zaidi ya 23,000 wa Manispaa ya Iringa ambayo  mwaka 2010 ilipoteza jimbo la Iringa Mjini kwa Mchungaji Peter Msigwa wa Chadema, walitangazwa na Katibu Mwenezi wa CCM Manispaa ya Iringa, Thobias Kikulacho kumdhamini mgombea huyo.

Mbali na Askofu Mdegella viongozi wengine wa dini waliojitokeza kuiombea mema  Safari ya matumaini ya Lowassa ni pamoja na Askofu Mkuu wa Makanisa ya End Time and Harvesting, Dk Boaz Sollo na baadhi ya mashehe wa mjini Iringa......


Wingi wa wadhamini hao pamoja na mamia ya wananchi waliojitokeza juzi kushuhudia tukio la Lowassa kudhaminiwa ulisababisha shughuli hiyo kufanyikia Uwanja wa Michezo wa Samora, badala ya ofisi CCM mkoa.
   
Akiiombea mema safari ya Lowassa, Askofu Mdegella alisema “Hata kama wanaoamua nani awe kiongozi ni wachache ni lazima wasikilize watu wanataka nani, mimi naamini wanaCCM wote ni wasikivu kwa watu; Iringa na kwingineko watu wameongea si kwa maneno ila kwa matendo.”

MEMBE


KATIKA hali inayoweza kuhitimishwa kama ukomavu wa kisiasa, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe amemmwagia sifa mwanasiasa mwenziwe Makongoro Nyerere akimpambanua na sifa ya ujasiri wa kukemea maovu  bila kuogopa.

Membe amesema Tanzania inahitaji viongozi aina ya Makongoro Nyerere kukemea madhambi ndani na nje ya Chama Cha Mapinduzi, CCM.

“Ninavutiwa sana na ujasiri alionao mwanasiasa na mgombea mwenzangu Makongoro Nyerere kwa kukemea ufisadi waziwazi bila hofu yoyote, ninaunga mkono ujasiri huo maana hata mimi ninachukiwa sana na wapenda rushwa na ufisadi ndani na hata nje ya chama chetu.”

Waziri Membe aliyasema hayo juzi wakati akitoa shukrani kwa wanachama zaidi ya 1900 wa chama hicho waliojitokeza kumdhamini kutoka wilaya zote za mkoa wa Mara.

“Mkoa wa Mara ni mkoa wenye heshima kubwa maana ni katika ardhi hii Mwalimu Julius Nyerere alizaliwa akiwa ni mtu aliyechukia dhuluma, rushwa na ufisadi na mwanawe, mgombea mwenzangu naye kachukua nyayo hizo, anakemea wazi wazi vitendo vya rushwa,” alisema.

PROFESA MWANDOSYA
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi Maalumu, Profesa Mark Mwandosya amemuomba mgombea mwenzake katika kinyang’anyiro cha kutafuta ridhaa ya kuteuliwa kuwa mgombea kupitia CCM, Edward Lowassa asisite kumuunga mkono kama walivyofanya watangaza nia wengine ili mambo yaishe mapema.

Aidha, amewaonya wanaotishia kukihama chama endapo hawatapitishwa, akisema huo ni upuuzi na pia vitisho kwa Mwenyekiti wa Chama na wanaCCM kwa ujumla, hivyo wanaojiona wao ni maarufu kuliko chama wanajidanganya.

Mwandosya alitoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki wilayani Mbozi alipokuwa akizungumza na wanaCCM waliomdhamini katika mbio zake za urais, pamoja na wanachama wengine waliojitokeza katika Ofisi za CCM Wilaya.

Mgombea huyo alisema amefarijika  kusikia anaungwa mkono na wagombea wenzake, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Waziri wa Mambo ya Nje na  Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe pamoja na kupata taarifa za Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wassira naye kusema anamuunga mkono.



Alisema pamoja na kuungwa mkono na wenzako hao watatu, anamuomba pia Lowassa naye kumuunga mkono ili kuipunguzia kazi Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM).



“Nimesikia Membe amesema hapa Mbeya asipopitishwa yeye basi atamuunga mkono Profesa Mwandosya, nikasikia tena na Waziri Mkuu akisema hata kama asipopitishwa yeye atafarijika kama Profesa Mwandosya atakuwa mgombea, nikasikia tena na Wassira naye kupitia kwa mtu wake wa karibu ataniunga mkono, sasa namuomba mwenzangu naye Edward au maarufu kama Edo naye aseme  Profesa ndiyo wangu, ili kazi iishe na tuipunguzie kazi Halmashauri Kuu,” alisema Profesa na kushangiliwa.



Awali Profesa Mwandosya aliwaeleza wanachama hao kuwa mwaka huu wa uchaguzi ni mwaka mgumu sana kwa CCM na kuwataka wanachama kutofanya mchezo katika kujibu mapigo ya wapinzani.



“Watatuuliza kuhusu EPA, wataendelea kutuuliza kuhusu Richmond, watatuuliza kuhusu Escrow, kubwa zaidi watatuuliza kuhusu Vodacom ingawa hili halizungumzwi lakini linakuja, lazima tujitayarishe.



“Sasa nani huyo ataweza kutusafisha, wananchi wakimtazama watasema huyu atatusaidia na atajibu, kila ninakopita naambiwa na wananchi  kuhusu ufisadi na rushwa vinatuumiza. Kama chama lazima tukabiliane na hilo na hapa hatumzungumzii mtu lazima kama chama tuyaeleze kwa wananchi. Nani atafanya hivyo wakubwa wanajua,” alisema  Profesa.



Akizungumzia wanaotishia kuhama chama, alisema wanajidanganya kwani CCM ni maarufu zaidi ya mtu mmoja mmoja, akisema mtu pekee aliyewahi kuhama na kukitikisa chama alikuwa Augustine Mrema, Waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani.

  DK MWAKYEMBE
WAZIRI  wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dk Harrison Mwakyembe amesema kati ya mambo anayoweza kujivunia wakati wa utawala wa serikali ya awamu ya nne ni kuwa miongoni mwa washauri wazuri wa Rais Jakaya Kikwete.

Alisema ni mmoja wa mawaziri wanaomshauri katika kusimamia na kutekeleza mambo ya maendeleo ambayo yamewezesha kuboresha huduma mbalimbali za kijamii.

 Aidha, amesema ni jambo la kusikitisha kuona kuna watu tena baadhi yao wako ndani ya CCM wanajifanya  hawajaona maendeleo ikiwemo kukamilika kwa ujenzi wa barabara za lami zinazounganisha kati ya mkoa mmoja na mwingine, maji, afya, elimu na mingineyo. 

Alisema, serikali ya awamu ya nne inapaswa kupongezwa kutokana na utendaji wake mzuri katika kubuni, kutekeleza na kufuatilia miradi yote iliyopangwa na hiyo inampa sifa kubwa yeye na kumfanya kuwa miongoni mwa watu wenye uwezo wa kugombea Urais wa Tanzania kupitia CCM.



Aliyasema hayo jana mjini Songea wakati akiwashukuru wanachama wa CCM waliomdhamini katika harakati zake za kuomba ridhaa ya CCM ili awe mgombea wake, huku akisisitiza kuwa anajiona ana sifa nyingi, ndiyo maana amejitokeza aweze kuendeleza mema yaliyofanywa na Serikali ya Rais Kikwete.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Responsive Ads Here