
WATENDAJI serikalini pamoja na mawaziri wametakiwa
kupunguza
safari za nje ya nchi, badala yake waende vijijini kusikiliza na kutatua
matatizo ya wananchi.
Katibu
wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape
Nnauye
alitoa tamko hilo juzi mjini Masumbwe, wilayani Mbogwe wakati akihutubia
mkutano wa hadhara.
Nape
ambaye pamoja na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana
wako
mkoani Geita kuangalia utekelezaji na uhai wa chama, alisema ambaye hatasikia
agizo hilo, atashughulikiwa mambo yaende sawa katika chama.
Akisisitiza
viongozi hao kutoka maofisini kwenda kwa wananchi, alisema viongozi
wakiacha kukaa Dodoma, na Dar es Salaam wakaenda vijijini, maendeleo ya wananchi
yatakwenda haraka.
“Nataka
nitoe mwito kwa watendaji wa serikali kuanzia huko juu, tusianzie huku chini,
Mawaziri watoke maofisini wapunguze safari za kwenda Ulaya, waje Mbogwe
washughulikie matatizo ya watu,” alisema Nape.
Alisisitiza,
“Kama sisi tuliopewa dhamana na wananchi tunazunguka, basi tunawataka na
Mawaziri wazunguke washughulikie matatizo ya watu.”
Alisema
yako matatizo mengi ya wananchi waliyobaini kupitia ziara hizo za Katibu Mkuu
Kinana ambazo kama Mawaziri watakwenda kuyasikiliza, ufumbuzi wake utapatikana
mara moja.
Alisema,
“Na sasa kwa kuwa masikio hayavuki kichwa, naamini watatusikia, asiyetusikia
tutashughulika naye ili mambo yetu yaende sawasawa.”
Kwa
mujibu wa Nape, tangu waanze ziara kuanzia mkoani Kagera na sasa
Geita,
kila wanakopita, yako mambo kadhaa ambayo yanakwenda taratibu kutokana na
wenye dhamana ya utatuzi kutozuru mikoani.
Alisisitiza
lengo la ziara ya Kinana ni kuongeza kasi ya kutatua matatizo ya
wananchi. “Watoke maofisi waje washughulikie matatizo ya watu,” alisema Nape na
kuongeza kwamba chama kikiendelea kushughulikia matatizo ya watu,
Watanzania wataendelea kukiamini.
Hata
hivyo, alisema wameendelea kushughulikia matatizo ya watu, hali ambayo
inaifanya CCM kuwa madarakani. Wakati huo huo, Nape aliendelea
kuhadharisha juu ya watu wenye mwelekeo wa kuvunja amani ya nchi na kuwataka
vijana kuepuka kuingia mtego huo.
Katika
ziara ya Katibu Mkuu wa CCM mkoani Kagera na Geita, amebaini kero
mbalimbali zinazokabili wananchi miongoni mwake ikiwa ni migogoro ya ardhi, matatizo ya maji, utitiri
wa vizuizi barabarani, bei ya chini ya mazao hususani kahawa na pamba na kodi
nyingi.
Katika
mikutano mbalimbali ya hadhara aliyoifanya kwenye mikoa hiyo,
Kinana
ameahidi kukutana na mawaziri wenye dhamana kwa ajili ya kutafuta ufumbuzi wa
matatizo hayo yanayokwamisha maendeleo ya wananchi.
No comments:
Post a Comment